dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, July 7, 2015

Kiunzi cha kwanza urais CCM kesho



Habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete wakati mwingine hukasimisha shughuli zake kwa kamati ndogo inayoketi chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Dodoma. Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM itakutana kesho mjini Dodoma kuanza shughuli yake ya kupitia taarifa za wagombea 38 wanaoomba kuwania urais na kisha kuwasilisha ushauri wake kwenye kikao cha Kamati Kuu inayokutana keshokutwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete wakati mwingine hukasimisha shughuli zake kwa kamati ndogo inayoketi chini ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Mangula amekaririwa mara kadhaa akisema chama hicho kitatumia vigezo 13 vilivyowekwa na chama kuwachuja wagombea hao, akisisitiza kuwa watateua mgombea mwadilifu, mwenye uzoefu na atakayeuzika kwa wananchi.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walioko tayari mjini hapa kwa kazi hiyo walilieleza gazeti hili kuwa jukumu kubwa la kamati hiyo ni kuishauri Kamati Kuu juu ya masuala yote yanayohusu maadili ya wanachama na wagombea wa nafasi mbali ndani ya chama na kwenye vyombo vya Dola.
Mjumbe mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji alieleza kuwa kama kuna jambo kubwa, kamati ndogo huwa haikutani, badala yake kamati kubwa ikiwa chini ya Rais ndiyo hukutana na kuandaa taarifa za kuwasilisha kwenye Kamati Kuu.
Alitolea mfano wa mambo makubwa kuwa ni kama vile kupitia majina ya wanaowania kuteuliwa kugombea urais, kwamba kazi ya kamati ni kueleza taarifa za kila mwombaji, mazuri yake, mabaya yake na ushauri inaoutoa kwa wajumbe wa Kamati Kuu.
Mjumbe huyo alisema, Kamati ya Maadili na Usalama haina mamlaka ya kukata au kuongeza majina ya wagombea na kwamba mambo yanayopelekwa kwenye Kamati Kuu ni yale mazito tu.
Kuhusu mambo ya madogo yanayoishia kwenye kamati ndogo, alisema ni yale yanayoonekana yana viashiria vya majungu.
Mangula hakupatikana jana kuzungumzia majukumu ya kamati hizo lakini Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alipoulizwa kwa simu alisema majukumu na mipaka ya Kamati ya Maadili na Usalama vimeelezwa ndani ya Katiba ya CCM.
Hata hivyo, katika katiba ya CCM matoleo ya 2005 na 2010 kamati hiyo haikuonekana na mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ambaye pia hakupenda kutaja jina lake, alisema haijatajwa kwenye kanuni za uchaguzi wala katiba ya CCM.
Alisema badala yake mchakato wa kumteua mgombea urais kwa mujibu wa kanuni na katiba unaanzia kwenye Kamati Kuu ambayo hata hivyo, haiwezi kufanya kazi ya kutoa na kupokea fomu za wagombea urais, badala yake kamati kama hizo (za maadili) zikawepo kwa ajili ya kuisaidia Kamati Kuu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alipotafutwa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo, alijibu kwa mkato kuwa yuko kwenye kikao.
Wajumbe wa kamati
Wajumbe wanaotajwa kuwamo kwenye Kamati ya Maadili na Usalama ni Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete, Makamu wenyeviti, Philip Mangula (Bara) na Dk Ali Mohamed Shein (Zanzibar), Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, Naibu makatibu wakuu, Vuai Ali Vuai (Zanzibar) na Rajabu Luhwavi (Bara), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana na Shamsi Vuai Nahodha.
Wajumbe wa Kamati Ndogo ya Maadili na Usalama wanaotajwa ni Mangula ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo.
Wengine ni Kinana, Vuai, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu, Anamringi Macha, Dk Maua Daftari, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Chana na Mzee Masoud.
Baada ya kazi ya wajumbe hao kukamilika taarifa itawasilishwa kwenye Kamati Kuu ambayo inaweza kuzitumia au kuziacha wakati wa kufanya mchujo na kupata wagombea wasiopungua watano watakaopelekwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa Ijumaa.
Halmashauri Kuu ya Taifa nayo itawachuja tena na kubakiza watatu watakaopelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa Jumamosi na Jumapili ili kupata mgombea urais wa CCM.
/Mwananchi
.

No comments :

Post a Comment