Mbinu hizo zimetokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuruhusu wanawake wajawazito, wenye watoto, wazee na wagonjwa kupewa kipaumbele kwenye zoezi hilo.
ALIYEKUTWA NA MASHINE NYUMBANI AKAMATWE
Katika tukio lililoripotiwa jana la mashine ya BVR kukutwa kwenye nyumba ya mtu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, ameagiza akamatwe mara moja na kuchukuliwa hatua.
Mashine hiyo ilidaiwa kufichwa nyumbani kwa mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Baba Furaha kwa mkakati wa kuandikisha watu nyakati za usiku.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Sadiki alisema kuwa mtu huyo aliyekutwa na mashine hiyo nyumbani kwake ni kinyume cha utaratibu uliowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kuagiza akamatwe.
Alisema mtu huyo anatakiwa kuchukuliwa hatua mara moja ili iwe fundisho kwa wengine.
“Sijapata taarifa rasmi, lakini kama tukio hili lipo na mtu huyu akakutwa na mashine nyumbani kwake, kwanza anatuvurugia utaratibu uliowekwa na anatakiwa kukamatwa mara moja,” alisema.
Kuhusu taarifa za baadhi ya maeneo watendaji wa mitaa kudaiwa kuorodhesha majina ya wana-CCM usiku kinyemela mtaani kisha kuyapeleka vituoni ili wapewe kipaumbele kwenye uandikishaji, Sadiki alisema nao wachukuliwe hatua.
Sadiki alisema inawezekana matukio hayo yapo na kuwataka wananchi na viongozi ngazi za chini, wanapowabaini wahusika wafikishwe polisi.
“Hatuwezi kuvumilia watu wanaovuruga utaratibu kwa sababu haya sio maelekezo ya Nec, kuandikisha ni asubuhi hadi saa 12:00 jioni zaidi ya hapo ni kuvunja sheria,” alisema.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Julius Mallaba, alipoulizwa kama Tume ina taarifa ya matukio hayo alisema bado hayajafika Nec.
Alisema mawakala waliopo vituoni hawajawajulisha kama kuna watu wanafanya hivyo na kumtaka mwandishi awaulize viongozi wa chama husika.
“Sisi hatufanyi kazi mtaani, tupo kwenye vituo maalum vilivyotengwa, kuhusu hiyo mashine hatujapata taarifa rasmi, nitafuatilia kwa sasa sina majibu na siwezi kusema chochote,” alisema.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, alipoulizwa kuhusiana na za CCM kuandikisha watu kinyemela mtaani pamoja na mashine iliyokutwa nyumbani kwa mtu, alisema yupo nje ya mkoa hawezi kulizungumzia hilo.
“Masuala hayo siwezi kuyaongelea nikiwa huku, watafuteni viongozi wengine au mkuu wa mkoa,” alisema na kuongeza:
“Kauli yangu kwa sasa ni kwamba Chadema kina hali mbaya kwa sasa hivyo wanaweza kufanya chochote,” alisema na kukata simu.
WANAUME WATUMIA MBINU KUJITANDA KHANGA
Baadhi ya wanaume walilazimika kutumia mbinu ya kujitanda khanga ili waonekane wanawake wakati vituo vingine wapo waliojitengenezea cheti ili waonekane wagonjwa.
Wananchi hao walikuwapo vituoni wakilalamikia kufika kituoni hapo siku tatu bila ya kupata vitambulisho huku wengine wakipata bila ya kukaa foleni. Kitendo hicho kilichowafanya baadhi yao kutumia njia mbadala ikiwamo kutoa rushwa ili wapitishwe haraka kujiandikisha.
Katika kituo cha Kisiwani, Tabata, Amina Abdallah alilalamikia kitendo cha mashine hizo kuharibika kila wakati na kusababishia foleni kuwa kubwa.
Alisema juzi mwanamke mmoja alipatwa na shinikizo la damu na kuanguka kutokana na kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na kituo hicho, katika vituo vingine changamoto zilikuwa zikijirudia kwa kueleza kuwapo na urasimu wa kupendeleana wakati waliowahi wakinyimwa kuandikishwa.
Baadhi ya vituo ambavyo NIPASHE ilishuhudia zoezi hilo likiimarishwa kwa kuongezewa mashine ili waweze kupunguza msongamano ni Tabata Kisiwani, Kituo cha Afisa mtendaji kata Vituka na Shule ya Msingi Vituka.
Maeneo mengine imedaiwa kuangalia uchama katika uandikishwaji na wengine kujaziwa fomu usiku ili inapofika asubuhi waonekane kama walikuwapo vituoni.
KINYEREZI
Katika kituo cha Kinyerezi Kanga hali ilikuwa mbaya baada ya wakazi wa kata hiyo kugomea utaratibu wa mwenyekiti wa mtaa wa kuandikisha majina ya watu waliokwenda katika kituo hicho tangu Julai 22, na kutaka watu waanze upya.
Kufuatia malalamiko hayo, Mwenyekiti wa kata hiyo, Shamte Mkali, alijikuta akijifungia ndani ya kituo baada ya wananchi kumjia juu na kutoa amri kwa waandikishaji kusimamisha zoezi hilo.
Debora Hassan aliyefika katika kituo hicho tangu saa 9 usiku alisema mwenyekiti ndiyo chanzo cha vurugu hizo kwa kuwa alikuwa na watu wake walioandikwa majina toka juzi jioni walimpigia simu ili aende kubadilisha utaratibu.
“Sijawahi kuona kiongozi mbishi kama huyu zoezi lilikuwa limeanza vizuri kaja kuharibu na hataki kusikiliza ushauri wa watu aliowakuta, matokeo yake watu wanatukanana na kupigana kwa ajili ya kudai haki zao,” alisema.
Naye Abdallah Seif alihusisha siasa na vurugu zinazotokea katika vituo vya kujiandikisha kwa madai kuwa kuna watu wamewekwa kwa ajili ya kuharibu utaratibu ambao watu wamejiwekea ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Katika tukio lingine mtu mmoja ambaye hakufahamika jina lake alitoa rushwa ya Sh. 5000 ili apitishwe kwa kupitia msomaji majina aliyeteuliwa na wananchi katika zoezi lililoanza saa 3:45 asubuhi.
WABEBA WATOTO KUKWEPA FOLENI
Kufuatia utaratibu wa kuruhusu akina mama wajawazito, wenye watoto, na wazee kupewa vipaumbele, baadhi ya watu walitumia mwanya huo kubeba watoto wasiokuwa wao ili wapate kuandikishwa mapema.
ZANZIBAR WALALAMIKA
Wananchi wamelilalamikia zoezi hilo kutokana na utaratibu kuwa mbovu.
Baadhi ya wananchi wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti walisema, baadhi ya maeneo zoezi hilo limekwenda vizuri lakini kwingine lilikuwa la kusua sua kutokana na mashine za uandikishaji kugoma.
Hamadi Suleiman Ali aliyefika kituo cha uandikishaji cha Welezo alisema zoezi hilo katika kituo hicho lilikuwa ni la kusuasua kutokana na mashine za BVR kugoma kwa muda mrefu.
Jamila Abdallah alisema siku nzima wameitumia kwa kushinda kituoni bila ya kufanikiwa kujiandikisha, jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa kupata tena fursa hiyo ya kujiandikisha.
Msimamizi wa kituo hicho, Suhaila Juma, alisema sababu ya watu wengi kushindwa kuandikishwa ni kugoma kwa mashine za BVR.
Licha ya malalamiko ya wananchi, Naibu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, alisifu zoezi la uandikishaji katika kituo cha Kisiwandui alichojiandikisha.
Hata hivyo aliitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kuhifadhi kumbukumbu za watu waliojiandikisha ili siku ya kupiga kura wasipate usumbufu.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI


No comments :
Post a Comment