Waliyaeleza hayo kwenye siku ya kumbukumbu ya mashujaa waliopigana vita hivyo katika Uwanja wa Mashujaa, mjini hapa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Shaban Ngasa (94) mkazi wa Kikuyu mjini hapa, alisema alifuatilia malipo yake miaka ya nyuma akiwa bado ana nguvu lakini hakufanikiwa kulipwa hadi sasa na kuamua kukata tamaa ya kupata malipo hayo.
“Niliwahi kufuatilia malipo yangu wakati Rais akiwa Julius Nyerere pale Ikulu ya Dar es Salaam alimanusura nifungwe jela, maana niliambiwa nimeleta fujo Ikulu, niliamua kuacha na kukaa kimya nimemwachia Mungu,” alisema.
Akielezea Vita vya Pili vya Dunia, alisema mwaka 1937 alichukuliwa pamoja na wenzake 26 kutoka Mkoa wa Dodoma walihamishiwa Arusha na baadaye kupelekwa Nairobi nchini Kenya ambapo waliunganishwa na wengine kutoka nchi mbali mbali na walikaa siku tano.
Alisema kutoka Nairobi walihamishiwa Mombasa na kwenda kuingizwa kwenya meli za kivita ambazo zilikuwa zimeegeshwa pwani ya huko.
Ngasa alisema wakiwa kwenye meli hizo walipelekwa kupigana vita katika maeneo mengi na kufanikiwa kushinda baadhi ya maeneo kwa taabu.
Alisema alipigana vita hivyo nchi mbali mbali ikiwemo Mali, Afrika Kusini na nchi za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Alisema katika idadi ya askari 26 waliochukuliwa Dodoma miaka hiyo ni yeye pekee ndiye alirejea salama huku wengine wakipoteza maisha katika vita hivyo vya pili.
Alisema wazungu walimtunukia cheo cha nyota mbili (luteni) kutokana na uhodari wake wa kuongoza vita katika maeneo mbalimbali aliyopelekwa hadi kustaafu.
Naye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Kaimu mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Fransis Mwonga, aliwashauri wanasiasa wanaowania uongozi mwaka huu waangalie wasiitumbukize nchi kwenye machafuko.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment