AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, July 7, 2015

Wanaopiga watu risasi katika uandikishaji BVR Zanzibar wakamatwe, washitakiwe.


7th July 2015.
Katuni.
Taarifa za kuwapo kwa vikundi vya watu wanaojifunika nyuso zao visiwani Zanzibar na kuwashambulia wananchi wanaojitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (BVR) zinazidi kushika kasi.
 
Mwishoni mwa wiki, watu wanaotenda unyama huo waliwapiga risasi raia wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa katika matukio yanayohusiana na shughuli ya uandikishaji kwa kutumia BVR inayoendelea visiwani humo. 
 
Baadhi ya wale waIiojeruhiwa walikaririwa wakisema kuwa waliowashambulia ni watu hao wanaojifunika nyuso, tena wakiwalezea zaidi kuwa hutekeleza unyama wao wakitumia magari yanayoonyesha dalili kuwa ni mali ya baadhi ya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). 
 
Wapo mashuhuda waliokaririwa wakisema kuwa wakati mwingine, wavamizi hao waliopachikwa jina la 'janjaweed' huteka raia, kuwapa mateso makali na kisha kwenda kuwatupa porini.  
 
Matukio ya kupigwa risasi wananchi mwishoni mwa wiki yalitokea katika Kijiji cha Makunduchi, eneo la kituo cha uandikishaji cha Nganani, mkoa wa Kusini Unguja.  Matukio mengine ya aina hiyo yamewahi kuripotiwa pia katika maeneo mengine kadhaa yakiwamo ya mkoa wa Mjini Magharibi, wilaya ya Magharibi A Unguja visiwani humo.Kuna taarifa vilevile za kuwahi kuwapo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani katika shughuli ya uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura katika maeneo ya Mtoni Kidatu na Shehia za Mtopepo, Mwanyanya na Bububu ambako baadhi ya nyumba za masheha zilivamiwa na watu wasiojulikana na kuchomwa moto. Yote hayo hufanyika kutokana na kile kinachoelezwa na baadhi ya waathirika kuwa ni matokeo ya chuki za kisiasa baina ya wafuasi wa vyama vikuu visiwani humo vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
 
Hakika, hizi siyo taarifa njema. Ni viashiria vya wazi vya uvunjifu wa amani visiwani Zanzibar, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. Kwa sababu hiyo, sisi tunadhani kwamba ipo haja ya kuchukuliwa hatua kali za kudhibiti mashambulizi hayo kwa raia kabla hali haijawa mbaya zaidi.  Ni imani yetu kuwa Jeshi la Polisi visiwani humo, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kulinda usalama, lingali katika operesheni maalum ya kuwanasa wahusika na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria.
 
Isitoshe, tunaamini kuwa Jeshi la Polisi Zanzibar litatoa taarifa ya kina kuhusiana na waovu hawa. Kwamba, kutokana na uchunguzi wao, wamebaini kuwa hao ni watu gani na wanafanya yote hayo kwa maslahi ya nani? 
 
Ni wapi wanakopata silaha za moto? Ni wapi wanakopata ujasiri wa kuzunguka na magari katika maeneo ya uandikishaji na kuwateka watu kabla ya kwenda kuwatesa bila vyombo vya usalama kuwabaini?  Hivi ni kweli vyombo vyetu vya usalama visiwani Zanzibar vimekosa uwezo wa kudhibiti vikundi hivi vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao kwa kuzunguka mitaani na bunduki na kupiga watu watakavyo bila ya kukamatwa? Je, huku si kuwapa kiburi wahalifu dhidi ya vikosi vyetu vya usalama ambavyo daima tunaamini kuwa viko imara na kamwe haviwezi kutikiswa na vikundi vya wahuni wa namna ya ‘janjaweed’ kwenye eneo dogo la Zanzibar?  
 
Hakika, maswali ni mengi. Na ndiyo haya yanayotoa mwanya wa kuibuliwa hisia mbaya kuwa 'janjaweed' huungwa mkono na baadhi ya maafisa wa vikosi vya SMZ na kwamba ndiyo maana hufanya watakavyo bila ya kukamatwa. 
 
Katika mazingira kama hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa sasa kuna haja ya Jeshi la Polisi kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya usalama na pia raia wa kawaida kupitia dhana ya 'ulinzi shirikishi jamii' kuhakikisha kuwa uovu huu unakomeshwa mara moja visiwani Zanzibar na kwingineko nchini.
 
Kinyume chake, kama hakutakuwa na hatua madhubuti za kuwadhibiti waovu hawa wanaojifunika nyuso na kutamba mitaani wakiwa na magari na silaha za moto, ni wazi kuwa wananchi wengi wataendelea kuishi kwa hofu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Hili halipaswi kuachwa litokee kwani mwisho wa siku, amani na utulivu vilivyodumu Zanzibar tangu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa 2010 vitapata mtikisiko mkubwa. 
 
Kadhalika, hali inayoendelea sasa inahatarisha jitihada za upatanishi zilizozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010 baada ya maridhiano baina ya CCM na CUF. Matokeo yake, tishio la kutokea uhasama zaidi kama ilivyowahi kushuhudiwa katika chaguzi za1995, mwaka 2000 na 2005 linaweza kurudi na kuathiri watu wengi wasio na hatia.  Shime, wahalifu hawa wanaojifunika nyuso na kushambulia raia visiwani Zanzibar wasakwe, wakamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment