AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, July 7, 2015

Mramba na Yona jela miaka mitatu.

  Walipata kuwa mawaziri wa Fedha, Walishtakiwa kwa makosa 11,Waweka historia kwa mawaziri kufungwa.

Mawaziri wa zamani wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba (kulia) na Daniel Yona, wakipanda gari la polisi kupelekwa gerezani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi. Picha: Tryphone Mweji.
Vilio jana vilitawala katika Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam baada ya mawaziri waandamizi wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona, kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
 
Hukumu hiyo ilitolewa jana kwa nyakati tofauti na Jaji Samu Rumanyika, ambaye alianza kusikiliza kesi hiyo kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji akisaidiana na Hakimu Saul Kinemela.
 
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mahakama hiyo kuwatia hatiani washtakiwa kwa makosa ya 11 kati ya hayo 10 ni ya matumizi mabaya ya madaraka na moja la kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.
 
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alisema baada ya mahamaka hiyo kupitia ushahidi wa mashahidi 13 wa upande wa Jamhuri na wa utetezi wa mashahidi sita, imewaona mshtakiwa wa kwanza, Mramba na wa pili Yona, kuwa wanahatia dhidi ya mashitaka hayo.
 
Alisema mahakama hiyo imebaini kuwa pamoja na Mramba kuwa Waziri wa Fedha, hakustahili kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya kufanya ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini kwa kuwa hakuwa na mamlaka hayo.Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Andrew Chenge, pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), walimshauri Mramba wakati akiwa Waziri wa Wizara ya Fedha afanye uchunguzi katika nchi nyingine jinsi wanavyotoa misamaha ya kodi.
 
Jaji huyo alisema ushahidi uliotolewa na Jamhuri umeithibitishia mahakama kuwa hasara hiyo ilisababishwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
 
Aliongeza kuwa washtakiwa hao wamekutwa na hatia kwa kuanzia kosa la kwanza hadi la 11, hivyo wanastahili adhabu.
 
Baada ya kutamka hivyo, Jaji Rumanyika alitoa fursa kwa mawakili wa Jamhuri na utetezi kutoa hoja ili mahakama hiyo itoe adhabu dhidi ya washtakiwa hao.
 
Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, aliiiomba mahakama hiyo kutoa adhabu dhidi ya washtakiwa kulingana na vifungu vya sheria ya mashitaka hayo.
 
Kweka aliiomba mahakama hiyo kutoka adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao kwa wao walikuwa viongozi wa serikali hivyo walitakiwa kuonyesha maadili mema kwa jamii.
 
Alidai hukumu hiyo itakuwa ni fundisho kwa viongozi wengine wa serikali walioko madarakani kutojihusisha na vitendo hivyo.
 
Kwa upande wake, Wakili wa Mramba, Peter Swai, aliiomba mahakama hiyo imuonee huruma mteja wake kwa madai kuwa hana historia ya kufanya makosa ya jinai,  ni mtu mwenye umri mkubwa na akifungwa yeye na familia yake watateseka. 
 
Naye wakili wa Yona, Elisa Msuya, aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu mteja wake kwa madai kuwa hana historia ya makosa na ana familia inayomtegemea.
 
Baada ya dakika 10, mahakimu wawili kati ya watatu walitoa adhabu dhidi ya washtakiwa hao.
 
Akisoma hukumu dhidi ya Mramba, Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa huyo atatumikia kifungo hicho kwa kosa la kwanza hadi la 10 ya matumizi mabaya ya madaraka na kulipa faini ya Sh. milioni tano au kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la 11.
 
Kadhalika, Yona alihukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kwanza, la pili, la tatu na la tano huku la 11 akitakiwa kulipa faini ya kiasi hicho cha fedha au kwenda jela miaka mitatu.
 
Kwa upande wa aliyekuwa Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja, Mahakama hiyo ilimfutia mashitaka na kumuachia huru baada ya kukosa ushahidi wa kumtia hatiani.
 
Hata hivyo, Jaji John Utamwa, katika hukumu yake aliwaona washtakiwa hao hawana hatia dhidi ya mashitaka hayo.
 
Baada ya mahakama kutoa hukumu, ndugu na jamaa wa washtakiwa hao waliangua vilio huku wakiwafuata Mramba na Yona kizimbani.
 
Miongoni mwao ni mke wa Yona aliyepanda kizimbani na kuangua kilio kisha kuishiwa nguvu na kusaidiwa na ndugu na jamaa kuondolewa kizimbani hapo.
 
Baada ya hukumu, Mgoja alitoka kizimbani na kuelekea kwenye maegesho ya magari mahakamani hapo na kupanda gari kisha kuondoka.
 
NIPASHE liliwashuhudia Mramba na Yona ambao walifika mahakamani hapo saa 6:00 mchana na kusomewa hukumu kuanzia saa 7:30 mchana, wakipandishwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili Z524DK na kupelekwa gerezani kuanza kutumikiaa vifungo hivyo.
 
Hukumu hiyo ilitolewa jana baada ya kuahirishwa mara mbili kati ya Juni 30 na Julai 3, mwaka huu lakini iliahirishwa kutokana na mmoja wa mahakimu hao kukosekana na Mwenyekiti wa jopo hilo, Jaji Utamwa kuwa mgonjwa.
 
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa wakiwa watumishi wa serikali, Oktoba 10, mwaka 2003, walikaidi ushauri wa TRA wa kuwataka wasitoe msamaha kwa kampuni hiyo.
 
Washtakiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo Novemba 25, mwaka 2008, mbele Hakimu Mkazi Mwandamizi Hezron Mwankenja na kusomewa mashitaka 13.
 
Kesi hiyo ilipangiwa jopo hilo na kuanza kusikilizwa mwaka 2009.
 
Katika shitaka la kwanza, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Joseph Ole, kuwa kati ya Agosti, mwaka 2002 na Juni 14, mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri walitumia vibaya madaraka.
 
Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni hiyo ya Uingereza iliingia mkataba wa kudhibiti madini kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation  kukagua uzalishaji wa madini ya dhahabu, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
 
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mramba na Yona wanadaiwa kuwa Mei 28, mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma jijini Dar es Salaam, wakiitumikia serikali katika nafasi za Uwaziri wa Fedha na Nishati na Madini, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mikataba ya kuiongezea kampuni hiyo muda wa miaka miwili wa kuendelea kukagua madini kuanzia Juni 2005 hadi Juni 2007 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
 
Ole aliendelea kudai kuwa, katika shitaka la tatu wote wawili wanadaiwa kuwa kati Machi na Mei mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao kwa kumualika Dk. Enrique Segura wa M/S Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation kuja kusaini mkataba wa nyongeza wa miaka miwili kabla timu ya majadiliano ya serikali haijaanza kulifanyia kazi suala hilo.
 
Katika shitaka la nne, kati ya Machi na Mei mwaka 2005, washitakiwa wanadaiwa kuwa walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kukaidi kupeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali suala la kodi kama ilivyopendekezwa na Timu ya Serikali ya Majadiliano, jambo ambalo lilisababisha mkataba uongezeke kwa miaka miwili bila kupitishwa na timu ya majadiliano.
 
Shitaka la tano, ilidaiwa kuwa Oktoba 10, mwaka 2003, Mramba akiwa Waziri wa Fedha, alidharau mapendekezo ya TRA ya kutotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
 
Katika shitaka la sita, Mramba anadaiwa kati ya 18 na 19 Desemba mwaka 2003, akiwa Waziri wa fedha, alitoa kibali namba GN 423/2003 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo yaliyopendekezwa na TRA.
 
Shitaka la saba, anadaiwa kuwa Desemba 19, mwaka 2003  akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka vibaya kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
 
Shitaka la nane, Oktoba 15, mwaka 2004 akiwa Waziri wa Fedha, alitoa kibali namba GN 497/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.
 
Shitaka la tisa, anadaiwa kuwa kati ya Oktoba 14 na 15, 2004, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 498/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.
 
Shitaka la 10, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, mwaka 2005 alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 377/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo ya TRA.
 
Shtaka la 11, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, 2005, alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 378/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.
 
Shitaka la 12, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni, 2003 na Mei, 2005, wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri, kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea kampuni hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 11,752,350,148.00.
 
Katika shitaka la mwisho, Mramba anadaiwa kuwa kati ya 2003 na 2007, akiwa Waziri wa Fedha, kwa makusudi alishindwa kuwa makini au kutotimiza wajibu wake kwa kusaini vibali vilivyotajwa katika mashitaka hayo kuruhusu kampuni hiyo kutokulipa kodi na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.
 
Washtakiwa kwa nyakati tofauti walikana mashitaka yote na kupelekwa rumande katika Gereza la Keko baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
 
Masharti hayo ni kujidhamini kwa kiasi cha Sh. bilioni 3.9 kila mmoja, kuwasilisha mahakamani zao za kusafiria na kutokutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama hiyo.
 
Pia, walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminiwa kwa kila mshtakiwa.
Hata hivyo, baada ya kutimiza masharti yao, waliachiwa kwa dhamana hadi jana iliposomwa hukumu hiyo dhidi yao.
 
WADAU: NI FUNDISHO
Wadau kadhaa wamesema hukumu hiyo ni fundisho kwa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia ofisi za umma.
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema ni ya kihistoria nchini kwa kuwa sheria imechukua mkondo wake.
 
“Hukumu hii imeonyesha kuwa mahakama imefanya kazi yake bila ya kuingiliwa na kwamba kumbe Mahakama za Tanzania bado ziko huru, zinaweza kuendesha mashauri na kutoa hukumu wakati wowote bila ya kuingiliwa,” alisema.
 
Dk. Bana alisema hukumu hiyo inatoa fundisho kwa viongozi wote walioko madarakani na wale walio kwenye ofisi za umma kuwa watafungwa iwapo watazitumia vibaya ofisi za umma kwa maslahi yao binafsi.
 
 Alipoulizwa iwapo kufungwa kwa viongozi hao waandamizi wa serikali wa zamani kama ni kafara ya kuonyesha uhalali wa serikali ya sasa dhidi ya ufisadi hasa ikichukuliwa kuwa bado kuna viongozi waliotuhumiwa kwenye sakata  la Richmond, Dowans, Epa, Meremeta na hivi karibuni Escrow, alisema:
 
“Kila shauri na mazingira yake na hukumu hii inatoa ujumbe ule ule kwamba viongozi na watu wote walio na tuhuma za ufisadi zenye ushahidi, iwapo watafikishwa mahakamani na ushahidi ukabainishwa, ni lazima watahukumiwa bila ya kujali vyeo ama nafasi zao serikalini.” 
 
Hata hivyo, aliiasa serikali kuwafikisha wote wenye tuhuma za ufisadi mahakamani ili sheria ichukue mkondo isije kuonekana kuwa akina Mramba wametolewa kafara.
 
Naye  Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema hukumu hiyo ni fundisho kwa viongozi wengine wa serikali ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kutumia vibaya mali za umma.
 
Alisema  wao kama viongozi wamewajibishwa si tu kwamba wao ndiyo wenye makosa pekee waliofanya vibaya kati ya viongozi waliopo katika sekta ya umma, lakini  wamepewa onyo hiyo kama chambo kwa viongozi wengine wenye tabia kama hiyo.
 
“Unapopewa madaraka ya kutumikia wananchi, ni vema ukayafanya kwa uaminifu na weledi, kina Mramba na Yona walikuwa ni viongozi wa wenzao, lakini walijisahau na kufanya makosa ama moja kwa moja ama kwa kuzembea kuwasimamia walio chini yao,  hiyo ni fundisho kwa wengine na wamewajibika kama  chambo kwa viongozi wengine,” alisema na kuongeza:
 
“Kazi hiyo isiishie kwa viongozi hao tu, inatakiwa ifanyike na kwa wengine ambao kwa namna moja ama nyingine wanashindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kujisahau kutumia mali ya umma kama ya kwao, pia wanatakiwa kutambua kuwa ni lazima kiongozi wa umma unapopewa madaraka ukatumia vibaya wananchi wanakwa wanakuangalia.”
 
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS),  Charles Rwechengura, alieleza kuhuzunishwa na hukumu hiyo, huku akipendekeza kesi za jinsi hiyo ziwe zinatumia muda mfupi.
 
“Kwa kweli inanisikitisha mimi binafsi kwa jinsi ambavyo nawafahamu. Sijui hasa sababu ipi iliyowafanya wahukumiwe, ni kesi iliyochukua muda mrefu…kesi kama hizi ziwe zinatumia muda mfupi,” alisema.
 
Hata hivyo, alisema hawezi kuelezea zaidi juu ya hukumu hiyo kutokana na kanuni za kisheria za taaluma yake kumzuia kutoa maoni kuhusu hukumu iliyotolewa na mahakama hadi pale atakapopata maelezo kamili ya hukumu hiyo.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus Mgaya, alisema hukumu iliyotolewa anaamini mahakama imetenda haki kulingana na kosa walilofanya.
 
Alisema anafikiri adhabu hiyo inastahili kwa makosa waliyofanya na kwamba hilo litakuwa funzo kwa viongozi na watendaji wa serikali wanaokiuka kanuni na sheria za utumishi wa umma.
 
“Nafikiri mahakama ambayo ni muhimili ambao unajitegemea kwa kutumia sheria na kanuni, imetoa adhabu hiyo kulingana na kosa walilotenda, nafikiri hili sasa litakuwa funzo kwa watendaji wasio waadilifu,” alisema Mgaya.
 
Alisema kuchelewa kwa hukumu ya kesi hiyo inatokana na changamoto za fedha za kutosha, vifaa na uhaba wa mahakimu, hivyo ni wakati wa serikali kuutengea muhimili huo fedha za kutosha.
 
Alifafanua kuwa kama ilivyo mihimili ya Bunge na Utawala yaani serikali kutengewa fedha za kutosha, ni vyema mahakama nayo ikatengewa fedha nyingi, serikali kuajiri mahakimu wengi ma kuweka vifaa vya kutosha ili kutenda haki na kushughulikia kesi kwa wakati.  

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment