Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, July 6, 2015

Watanzania tuungane pamoja kuutafuta uhuru mpya wa taifa letu!




Na Fred Mpendazoe
MWAKA 1961
, Tanganyika ilipata Uhuru na mwaka 1964 iliungana na Zanzibar na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu nchi yetu ipate uhuru dhamira kuu ya waasisi wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Karume ilikuwa ni kupambana na umaskini, ujinga, maradhi na dhuluma.
Ni ukweli usiopingika kwamba awamu ya kwanza ya utawala wa nchi yetu ulikuwa na uongozi adilifu. Awamu hii ya kwanza ilitilia mkazo “maendeleo ya watu na siyo vitu” kwani ukiwaendeleza watu unawaondoa ujingani na kuwaweka kwenye nuru.
Kwa njia hiyo unawaongezea uhuru wa kutetea haki zao na kujiamulia mambo yao wenyewe ambayo yako au yanafanyika kwa maslahi yao.
Dhana hii imefafanuliwa katika Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971, unaotamka kwamba, “Kitendo chochote kinachowapa wananchi uwezo wa kuamua mambo yao wenyewe, ni kitendo cha maendeleo japo hakiwaongezei afya wala shibe” Maneno haya maana yake ni kupata uhuru au kujitawala.
Maana yake ni kwamba unatawala mazingira yako mwenyewe na kuamua mwenyewe kitu gani kifanyike kwa ajili ya maslahi yako
Katika kitabu cha Uhuru na Maendeleo, Hayati Mwalimu Nyerere alieleza bayana uhusiano uliopo kati ya kuku na yai na jinsi uhusiano huo unavyofanana na uhusiano uliopo kati ya uhuru na maendeleo. Nyerere alisema,“ bila kuku hupati mayai, na bila mayai kuku wote watakwisha”.
Adha, Nyerere alisema, ”bila uhuru (kujitawala) hakuna maendeleo, na bila maendeleo uhuru utapotea”. Aidha, katika kitabu hichohicho, Nyerere alisema, “Kuna uhuru wa kutosumbuliwa na njaa, maradhi na umaskini. Kuna uhuru wa mtu binafsi yaani haki yake ya kuishi, akiheshimika sawa na wengine wote.
Uhuru wake wa kusema na uhuru wake wa kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayoyogusa maisha yake, na uhuru wa kutokamatwa na kuwekwa ndani kwa kuwa tu kamuuzi mkubwa, japo hakuvunja sheria yoyote. Yote hayo yanahusu uhuru, na hatuwezi kusema wananchi wa Tanzania ni huru mpaka tuwe tuna hakika kwamba wanao uhuru wa mambo yote hayo”.Serikali ya Tanzania imekuwa katika mapambano dhidi ya maadui umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma ili kuulinda uhuru wa Watanzania. Katika makala hii, nitaeleza mambo machache yanayohusiana na uhuru na maendeleo (maendeleo ya watu siyo vitu) kama yalivyobainishwa na Nyerere.
Moja ya tishio kubwa kwa Watanzania kwa sasa ni umaskini. Utafiti unaonyesha kwamba kwa sasa idadi kubwa ya watu nchini wanaishi kwenye umaskini uliokithiri ambapo asilimia 60 wanaishi vijijini. Wananchi hawa hawana huduma bora za afya, maji, elimu na usafi wa mazingira.
Aidha, asilimia 15 tu ya Watanzania wanatumia umeme na asilimia 70 ya Watanzania wanaishi kwenye maeneo holela yasiyo na huduma. Na Watanzania wengi wanaishi kwa mlo mmoja kwa siku.
Kuna familia nyingi za Watanzania ambazo huishi kwa kubanana chumba kimoja. Watanzania wengi hawana makazi, wanalala mitaani, wakipita mitaani wakiombaomba au kuwa walinzi wa magari yaliyoegeshwa.
Kuna Watanzania wengi wasio na ardhi wanaishi kwa kuwafanyia kazi watu wanaomiliki ardhi ili wapate kisehemu kidogo cha kulima, kuna Watanzania wengi ambao wamepokonywa ardhi yao na kupatiwa wawekezaji.
Kuna watoto wa Watanzania wengi ambao watoto wao wanasoma wakiwa wamekalia mawe. Kuna watoto wa Watanzania wengi wanaopoteza maisha kutokana na wazazi wao kushindwa kumudu gharama za matibabu, yoye haya yanaeleza uamskini unaowakabili Watanzania.
Jambo linaumiza zaidi ni kwamba hakuna sababu dhahiri kwa nini Watanzania ni maskini baada ya miaka zaidi ya mika 53 ya kujitawala wakati nchi ina rasilimali nyingi. Jibu sahihi ni kwamba, umaskini wa Watanzania unatokana na uongozi mbovu wa chama tawala cha CCM.
Je uhuru uliopiganiwa na waasisi wetu upo au umepotea? Maana bila maendeleo uhuru hupotea kama vile bila mayai kuku wote watakwisha. Ukitaka mtu uendelee kumtawala mfanye awe maskini asijitegemee. Utamtawala milele. Nadhani hili ndilo lengo na CCM.
Uongozi wa awamu ya kwanza ulitilia mkazo suala la elimu ili kupambana na adui ujinga. Elimu ni nyenzo nzuri ya kuwaendeleza watu na kuwawezesha kujiamulia mambo yao wenyewe.
Elimu pia huchochea udadisi na kuhoji mambo na matendo yaliyopitwa na wakati. Kwa mfano, watu wa kijiji kimojawapo walioelimika vizuri hawatakubali wala kuvumilia udanganyifu wa wahasibu ama ubabe wa viongozi wao.
Watu walioelimika watahoji matendo ya viongozi wanaowawakilisha-hata kama kiongozi huyo ni rais. Elimu ni muhimu kwa mustakabali wa taifa. Kwa bahati mbaya, nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa katika sekta ya elimu.
Katika kikao kimoja cha Baraza la Madiwani kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, watendaji waliwasilisha ombi la kupewa idhini ya matumizi ya fedha kwa ajili ya programu ya dharura ya kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wanajiandaa kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba, lakini walikuwa hawajui kusoma wala kuandika.
Jambo hili lilinishangaza sana. Lakini ndivyo ilivyokuwa. Watoto wamefikaje darasa la saba lakini bado hawajui kusoma na kuandika? Hali hii haipo Kishapu tu. Elimu ni janga la kitaifa.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2010 ni kielelezo tosha cha ukubwa wa janga hili. Takribani asilimia 88 ya watahiniwa wa mtihani huo walipata kati ya daraja 0 na IV, yaani, walifeli.
Mwaka wa masomo ya sekondari wa 2012 matokeo ya mtihani yalikuwa mabaya zaidi kiasi cha Waziri Mkuu wa serikali ya CCM kuteua Tume kuchunguza kulikoni kutokea ufaulu wa chini kiasi hicho iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome ambaye baadaye aliteuliwa Katibu Mkuu wa Wiazra ya Elimu na Ufundi.
Bahati mbaya matokeo ya uchunguzi wa Tume hiyo ya Waziri Mkuu yalichakachuliwa na serikali kuamuru eti matokeo yabadilishwe ili ufaulu uonekane nafuu kidogo. Lakini tatizo kubwa zaidi katika elimu ni kuwa wanafunzi wanaandaliwa kushinda mitihani tu.
Mwanafalsafa Socrates alisema kuwa mtu msomi ni mwenye sifa zifuatazo: kwanza, ni mtu anayeweza kuyatawala mazingira yake, badala ya mazingira kumtawala yeye; pili, anakabiliana na hali zote kwa ujasiri na hufanya hivyo kwa kutumia akili ya kisomi; tatu, anashughulikia mambo yote kwa uadilifu na, nne, hudhibiti starehe zake na hawehushwi na wala haharibiwi na mafanikio yake.
Mwalimu Nyerere alituasa kwamba lengo kuu la elimu ni kumkomboa Mtanzania kuondokana na fikra za kinyonge za kutawaliwa, kwa kumfanya ajitambue kwamba yeye naye ni sawa na binadamu wengine.
Aidha, elimu inatakiwa kumkomboa mwananchi kutokana na tabia mbaya inayomfanya ayakubali mazingira yanayodhalilisha utu wake kwa kudhani kwamba mazingira hayo ndiyo stahili yake. Akifafanua zaidi, Nyerere alisema, mafundisho yanayompa mtu mawazo ya utumwa au unyonge si elimu hata kidogo.
Elimu ni lazima iweze kumsaidia mtu kuchambua njia kadhaa tofauti za kufanya maamuzi na kumfanya aweze kuchagua moja kati ya njia hizo tofauti katika kuhangaikia maisha yake, na lazima impe mtu uwezo wa kufasiri maamuzi yake katika vitendo.
Elimu duni ni janga la kitaifa katika nchi yetu. Ukitaka mtu umtawale mnyime elimu bora. Mfumo wa elimu uliowekwa na serikali ya CCM ni dhahiri unawafanya Watanzania wawe wamepoteza uhuru wao kwani kwa mfumo huu wa elimu maendeleo hayawezi kupatikana, na bila maendeleo uhuru hupotea kama bila mayai kuku wote watakwisha.
Uhuru mwingine ambao umepotea ni uhuru wa mtu kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayoyogusa maisha yake. Moja ya mambo yanayogusa Watanzania kwa ujumla wake ni kukubaliana namna ya kujitawala, kukubaliana kuhusu Katiba.
Watanzania walitakiwa wawe huru kuandika katiba wanayoitaka. Serikali iliyopo madarakani, pamoja na chama tawala, si wadau pekee wa Katiba mpya. Mdau mkuu ni mwananchi. Bunge la Katiba liliyaacha maoni mengi ya wanachi.
Hivyo, CCM na serikali yake imewanyima kwa makusudi Watanzania uhuru wao katika kuandika katiba wanayoitaka. Msemo wa kichina unatilia mkazo ushirikishwaji wa wanachi wakati wa kuandika katiba yao, “Ukinieleza nitasahau, Ukinionyesha nitasahau, bali ukinishirikisha nitakumbuka”.
Upo ushahidi wa kutosha kwamba Watanzania wengi hawaijui Katiba ya sasa na hawakumbuki inasema nini. Sababu kubwa ya hali hii ni ukweli kwamba hawakushirikishwa katika kuiandika. Ni dhahiri sasa uhuru wa Watanzania kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayoyogusa maisha yake umepotea chini ya utawala wa CCM na serikali yake.
Kuna uhuru wa mtu binafsi yaani haki yake ya kuishi na uhuru wa mtu kutokamatwa na kuwekwa ndani kwa kuwa tu kamuudhi mkubwa, japo hakuvunja sheria yoyote. Mauaji wa ndugu zetu maalbino na mauaji ya mwandishi wa habari kule Iringa ni moja ya uthibitisho wa kupotea kwa uhuru wa mtu binafsi, haki ya kuishi.
Watanzania kwa sasa wanaishi kwa hofu kubwa. Hali ilivyo sasa, Serikali ya CCM inatumia nguvu kubwa kuwanyamazisha wananchi kutoa maoni yao kuhusu mambo yanayogusa maisha yao. Inazuia wananchi kuandamana wakati ni haki yao kikatiba.
Wananchi wanakamatwa na kuwekwa ndani kwa visingizio vya taarifa za kiintelijensia lakini lengo ni kuwanyamazisha wananchi. Ikumbukwe penye uhuru ni pale wananchi wanaweza kutoa maoni yao bila hofu, na penye demokrasia ni pale serikali inaposikiliza maoni ya wananchi wake.
Hali ya umaskini uliokithiri wa Watanzania, elimu duni au janga la elimu linaloikabili Taifa letu na kufifia kwa demokrasia, inadhihirisha kwamba uhuru uliopiganiwa na waasisi wetu wakati wa TANU na ASP, haupo tena. Bila maendeleo uhuru unapotea, kama ilivyo kwa mayai ambapo bila mayai kuku wote watakwisha.
Hayo machache niliyojaribu kuyaeleza yanayohusu uhuru na kama alivyotuaasa Mwalimu Nyerere hatuwezi kusema wananchi wa Tanzania ni huru mpaka tuwe tuna hakika kwamba Watanzania wanao uhuru wa mambo yote hayo.
Baada ya takribani miaka 50 ya matumaini, upendo, na mshikamano wa kweli uliojengwa katika misingi imara ya haki nchi yetu, Tanzania sasa inaporomoka kwa kasi ya ajabu.
Nchi yetu ilijengwa katika misingi imara ya udugu, uadilifu, umoja, mshikamano, upendo, usawa na haki kwa watu wote. Tunu hizi zilijengwa kwa gharama kubwa na waasisi wa taifa letu. Waasisi hawa walihangaika kupigania uhuru wa Watanzania na wao wenyewe walijitoa nafsi zao sadaka bila woga.
Tangu kuondoka kwa Baba wa Taifa, na kwa kiasi fulani baada ya enzi za mzee wetu, Ali Hasan Mwinyi, awamu mbili zilizofuata, yaani Serikli ya CCM ya Rais Benjamini Mkapa na serikali ya CCM sasa ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, nchi yetu imekosa uongozi imara na imeyumba.
Tanzania yetu ipo njia panda na imekwama. Na hatua tuliyopiga kama taifa haifanani na umri mkubwa wa kujitawala kwetu wala utajiri wa rasilimali uliotamalaki kwenye ardhi yetu. Watanzania tuungane pamoja kuutafuta uhuru mpya wa Taifa letu.
Napenda kuhitimisha makala hii kwa kusema: Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa. Mabadiliko yanawezekana, tukiamini. Pasipo imani, hakuna kinachowezekana.
Ukiwa na imani, hakuna lisilowezekana. Pasipo mashauri, taifa huanguka, bali kwa wingi wa washuri huja wokovu; Mema hushinda mabaya; Ukweli hushinda uongo na Upendo hushinda uovu; Harakati zetu zitafanikiwa.

TUTASHINDA. 


No comments :

Post a Comment