Aandika Jenerali Ulimwengu: Watawala wezi wakivumiliwa, nchi itatawaliwa na jeshi la waporaji
Na Jenerali UlimwenguNIMEANDIKA kwamba sifa mojawapo ya nchi ambayo in taifa ni kwamba wakuu wa nchi hiyo, wakiwa wezi, watakwenda kuziibia nchi nyingine, lakini ni marufuku kuziibia nchi zao. Wanaoshindwa kutambua hili, wakaliibia taifa, wakikamatwa wanapatwa na adhabu kubwa sana, ambayo inaambatana na fedheha kwa mhusika na familia yake na ukoo wake. Ishara moja kwamba hatujengi utaifa hapa kwetu ni kwamba wezi wanaoiibia nchi, hawaoni haya wala hawana woga. Hawaonekani kama waovu, na badala yake ndio hao hao tunaowachagua kuwa eti viongozi wetu! Wanatamba huku na kule wakidhihirisha dharau ya ajabu dhidi ya wananchi, na wananchi hawaoni uchungu kutokana na kuibiwa na kudharauliwa. Nimeonyesha pia kwamba pale wananchi wanapokuwa na hisia kwamba mali yao imeibwa, uchungu wao na ghadhabu yao wanaionyesha kwa kibaka aliyewaibia kwa kumpiga na kumchoma moto. Sasa, unaweza kujiuliza, iwapo kibaka aliyekwapua shilingi 100 anachomwa moto, inakuwaje mkuu aliyechota mabilioni ambayo ni mali ya nchi asichukuliwe hatua zo zote, na badala yake anakubalika kuwa “kiongozi”? Hali hiyo isiyoonyesha mantiki inasababishwa na hisia kwamba mali ya pamoja haina mwenyewe, ambayo ni dalili ya nakisi ya utaifa katika hisia zetu na katika utamaduni uliozoeleka kwa muda mrefu.Ni dhahiri kwamba tukiendelea hivi na tabia hizi za kipuuzi za kutoona kwamba mali ya pamoja ni yetu sote, na badala yake tukaendelea kuwavumilia wezi na waporaji wa mali za nchi, tunaelekea katika machafuko makubwa. Tusije tukajidanganya kwamba sisi ni tofauti na nchi nyingine za Kiafrika na za dunia ya tatu ambazo zimo katika machafuko. Hatuna tofauti yo yote, na kama vile waliofanya mambo ya kipuuuzi wameishia kubeba gharama kubwa kwa pamoja, hatuna sababu ya kujidanganya kwa kuamini kwamba sisi tutaweza kuiepuka sudi hiyo. Hatutaweza. Kwa kweli dalili za machafuko hayo naziona wazi wazi. Jambo la kwanza ni kwamba tumekwama, na tutaendelea kukwama, kimaendeleo. Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana iwapo kile kidogo tunachoweza kukipata kwa jasho jingi hatukidhibiti na wala hatukioni kama ni chetu. Hatuwezi kuendelea kwa njia yo yote ile iwapo mavuno ya nafaka yaliyotokana na sisi kuhenya katika mazingira magumu ya uzalishaji tunayakabidhi kwa mapanya-buku wanene ili wayagugune wanavyopenda huku watoto wetu wakiwa wanaendelea kwenda kitandani wakiwa wanalia njaa. Jambo la pili ni kwamba iwapo utamaduni huu utaendelea na ukisimika mizizi mirefu katika jamii yetu, itafikia wakati kila mwizi ataona ni haki yake kuiba na atakuwa hana tena pingamizi la kumfanya asite kuiba cho chote anachokiona kama hakina mwenyewe. Mantiki hapa ni kwamba anayeiba waziwazi, mchana kweupe na akabainika, asipopigiwa kelele na kuchukuliwa hatua, huo unakuwa ni mwaliko kwa kila aliye na ujasiri wa kiwizi kujaribu bahati yake. Baada ya muda (na sasa inajidhihirisha) watu wengi zaidi watazuka na kutumia madaraka yao na nafasi walizo nazo kujaribu na wao kujitajirisha kwa kutumia mali za umma ambao wanaostahili kuzilinda wameamua kuziacha ziporwe na wachache. Hivi hili hatulioni? Kila linapozuka sakata la kashfa yo yote ambayo inawahusu wau waliomo katika aina Fulani ya madaraka, mabo machache hujitokeza. Mojawapo ni kwamba ukubwa wa kitita cha fedha kinachodaiwa kuporwa kinakuwa kiukubwa zaidi kuliko cha ile kashfa iliyopita, na ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi maridhawa. Hii inaweza kuwa maana mbili tofauti. Moja ni kwamba kiasi cha fedha zinazoporwa kinazidi kuwa kikubwa zaidi kwa sababu mikondo ya kukusanya fedha za umma, kama kodi, imekuwa ikiboreshwa na sasa serikali inakusanya viwango vikubwa kuliko hapo zamani, na kwa hiyo wezi wanajikuta na vitita vikubwa zaidi ambavyo wanaweza kuvipunguza kwa viwango vikubwa kuliko zamani lakini asilimia ya kilichoibwa ukibakia ni ule ule. Inawezekana pia kwamba fedha zinazokusanywa bado hazijaongezeka kiasi hicho, lakini usimamizi wa hata hicho kidogo kidogo kinachopatikana ni dhaifu mno kwa sababu kila mmoja, ikiwa ni pamoja na walio na dhamana ya kukichunga, hawajali au hata wanashiriki wenyewe katika kukipora. Hii ina maana viwango vinabaki kuwa vidogo katika ukusanyaji lakini vinazidi kuwa vikubwa katika uporaji. Hii inakuwa na maana kwamba asilimia inayoporwa inakuwa kubwa zaidi ya ilivyokuwa zamani, na hii ina athari katika uwezo wa serikali kuendesha shughuli za maendeleo na kutoa huduma za jamii. Hapa ndipo tunapopata maelezo ya kitendawili cha nchi yenye rasilimali kubwa kukosa maendeleo wakati ile isiyokuwa na hizo rasilimali kuwa na maendeleo makubwa.Wala hiki si kitendawili kigumu kukitegua. Mkuu wa kaya anayepata kipato cha shilingi milioni 10 kwa mwezi, na akatumia milioni tisa kulewea na kuoa kila Jumamosi, hawezi kumfikia kiuwekezaji katika maendeleo ya familia jirani yake anayepata shilingi milioni mbili na zote zinaingia katika maendeleo ya familia. Hivyo ndivyo tulivyo, na wala tusione matatizo yetu kimaendeleo kama jambo la kushangaza, kwani linaelezeka.Ukweli ni kwamba watawala wetu wameshindwa kuzilinda mali zetu, na mara nyingi kwa kweli ndio wa kwanza kuzihujumu mali hizo. Sasa, iwapo tutaendelea kuwachagua watu wa aina tunayochagua, na iwapo tutaendelea kuwavulimia wezi hao kwa sababu mali wanazopora hazituuumizi kiasi cha kutaka kuwachoma moto kama tunavyowachoma vibaka, basi kila mmoja wetu aliye katika nafasi ya kuiba akiwa madarakani, ataiba. Kwani nini kitamzuia. Tukumbushane: Watu wengi wanaojizuia kufanya maovu hawajizuii kwa sababu tu ni watu wema; wanajizuia kwa sababu wanajua kuna adhabu inayoendana na maovu. Adhabu hiyo inaweza kutokana na maandiko ya misahafau, ambayo yamejaa vitisho vya kila aina, na kuwafanya watu wasite. Aidha maandiko hayo yamebeba ahadi nyingi za raha zinazomsubiri mtu aliyekuwa mwema hapa duniani. Katika haya, watu wengi wakipima baina ya adhabu zile na mbadala wa mvuto wa ahadi, wanaona ni heri kutenda mema wakisubiri raha za peponi. Kwa watu waliolelewa kuwa na moyo wa huruma, inakuwa ni rahisi kwao kukumbatia mema na kuwatendea haki wenzao. Lakini wapo watu wengi tu ambao wanaziona ahadi za paponi kama hekaya tupu na wala hawaogopi hivyo vitisho, na wala hajavutiwa na ahadi za pepo. Hawa watakachoogopa ni nguvu ya umma iliyowekwa mikononi mwa serikali. Umma ukiipa serikali mamlaka ya kukamata wezi, wabakaji na wauaji na kuwafunga, kuwachapa bakora au kuwafilisi na kuwaaibisha kadamnasi, waovu hao wataogopa kutenda maovu yao. Kwa vyo vyote vile, hata wasipoogopa, adhabu yao itawapata haraka, hapoa hapa duniani. Hakuna kusubiri mpaka huyo afe, azikwe, akae ardhini hasi siku ya Kiama ndip ahukumiwe. Kwa mtu kama huyo, Segereya inatisha zaidi kwa sababu anaijua ilipo, na inawezekana alikwisha kwenda kutembea huko akajionea hali ilivyo, au ndugu yake aliyewahi kuwa huko kama mfungwa ama mfanyakazi alikwisha kumhadithia mambo yalivyo huko. Hakuna aliyewahi kwenda kuzimu na akarudi kutueleza yaliyoko huko, lakini Segerea au Ukonga ni mahali watu wengi wamepaona. Wakuu wetu waliokabidhiwa madaraka wangekuwa mara kwa mara wanakamatwa kwa wizi, wenzao wangejifunza kuheshimu sheria. Lakini sasa, wanatangaza nia kutaka kututawala katika ngazi ya juu kabisa. Itaendelea
- See more at:
http://raiamwema.co.tz/watawala-wezi-wakivumiliwa-nchi-itatawaliwa-na-jeshi-la-waporaji#sthash.CFdC9cGD.dpuf
No comments :
Post a Comment