Hali kadhalika, Dk. Magufuli amewataka wana-CCM hao kutoendeleza makundi kwa kuwa yatahatarisha ushindi wa chama hicho.
Aidha, amewaombea msamaha wagombea wa Majimbo ya Sumbawanga Mjini, Kwela, Kalambo mkoani Rukwa na Momba mkoani Sogwe.
"Nawaomba muwasamehe saba mara sabini kwa kuwa hawachagui malaika bali binadamu ambaye siyo mkamilifu," alisema Dk. Magufuli.
Alisema yawezekana yapo ambayo hawakuyatekeleza kama inavyotakiwa na makosa mengine ambayo yamekuwa kinyume na matarajio ya wananchi, lakini anawahitaji afanye nao kazi na ahadi zote watakazoahidi watazitekeleza kwa maendeleo endelevu ya wananchi.
ATAKA MAKUNDI YAVUNJWE
Akiwa Jimbo la Kwela ambalo mgombea wake ni Ignus Malocha, alisema kura za maoni zimeisha na kinachotakiwa ni kuvunja makundi na kufanya kazi ya kuipa ushindi CCM.
"Inawezekana mbunge wenu hakufanya hadi mlipotarajia, namuombea msamaha kweli kweli, nipeni, huyu ni binadamu hatuchagui malaika, mchagueni Malocha msihadaishwe na maneno mengi," alisisitiza.Akiwa Jimbo Kalambo ambalo mgombea wake ni Josephat Kandege, alisema waliobwagwa kura za maoni hawapaswi kulalamika na kuacha kuunga mkono mgombea aliyepita, kwani akiwa rais nafasi za kazi zitakuwa nyingi kila mmoja atapata.
"Nakwenda kuwa rais, nafasi za kazi ni nyingi sana. Mligombea kwa kuwa mnataka kufanya kazi, nitawapa kazi, lakini hakikisheni huyu anashinda," alisema.
Katika Jimbo la Momba ambalo mgombea wake ni Dk. Lucas Siyame, alirejea ombi la msamaha kwa wananchi hao kwa kuwa mgombea huyo alihimiza ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Tunduma, lakini kwa sababu ambazo hazieleweki walimuangusha.
"Tunaambiwa tusamehe saba mara sabini, kama kuna dhambi aliifanya msameheni na ikifika Oktoba 25, mmpe kura za ndiyo," alisema.
Alisema wagombea wengine wasiwe na shaka kwani serikali ya awamu ya tano itakuwa na nafasi nyingi za wachapakazi na waadilifu na kutokana na nia yao ya kutumikia watu, hawatakosa nafasi hizo.
"Licha ya jitihada za wakati huo, lakini mkampiga chini, ila namuombea msahama, mrudisheni wakati huu nifanye naye kazi, tunahitaji maendeleo bora kwa wote na hayo yataletwa na mafiga matatu kwa maana ya diwani, mbunge na rais," alisema.
Dk. Magufuli alisema kufanya kosa siyo kosa bali kosa kurudia kosa.
Akiwa Jimbo la Sumbawanga Mjini ambalo mgombea wake ni Aeshi Hilary, pia aliwaomba wananchi wafute makosa na kuanza upya kwa kumpa kura za ushindi.
Akiwa Jimbo la Mpanda Mjini, alitoa ahadi ya kazi kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kipindi kilichopita kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Said Arfi, na kuangushwa kwenye kura za maoni za CCM, huku akisema alikokuwa alikuwa amekosea njia.
"Kazi zipo nyingi nitakuwa rais wa nchi hii, kazi zipo nyingi wala usiwe na shaka, sitakosa nafasi ya kukupa, najua uwezo wako katika kazi," alisistiza.
Akihutubia wananchi wa eneo la Nzokala, Lusaka na Laela, alisema katika mchakato wa kumsaka mgombea urais wa CCM walikiwa 38, lakini alichaguliwa kupeperusha bendera ya chama hicho lakini wamevunja makundi na kumuunga mkono.
Aliagiza wagombea hao kupeleka orodha ya wagombea wote wa kura za maoni kwenye majimbo yao kwa ajili ya kuwapatia kazi baada ya kuingia Ikulu.
Aidha, alisema ahadi zote anazotoa atatekeleza na kwamba kubwa kwake ni utekelezaji wa huduma za jamii kama ujenzi wa zahanati vijiji vyote, vituo vya afya kwenye kata, hospitali wilayani na hospitali za rufaa mikoani na kuhakikisha dawa zinakuwapo na siyo maduka binafsi kuwa na dawa na maeneo ya umma kukosa dawa.
Alisema atahakikisha huduma ya umeme, majisafi na salama vinapatikana kwas kuwa kama aliweza katika ujenzi wa barabara, hivyo mengine hatashindwa.
ASKARI KUBORESHEWA MISHAHARA
Dk. Magufuli aliahidi kuwa akishinda katika nafasi hiyo, ataboresha maslahi ya askari ili wasiendelee kuomba rushwa kwa kuwa watakuwa na maslahi mazuri.
BARAZA DOGO LA MAWAZIRI
Aidha, alisema Baraza lake la mawaziri litakuwa dogo la kuhudumia Watanzania.
Akihutubia wananchi katika uwanja wa Nelson Mandela, Jimbo la Sumbawanga Mjini, Dk. Magufuli alisema Baraza la Mawaziri atakalounda litakuwa na mawaziri wachache na wenye kuwajibika kwa wanyonge na katika kuwapata atawachambua pole pole.
Alisema katika hilo, hatafanya usanii bali kweli tupu kwa kuwa anajua kuna maisha baada ya dunia na kwamba anataka kutekeleza ahadi zake zote kwa Watanzania ili siku atakapokufa awe rais wa malaika mbinguni.
"Sijagombea urais kwa majaribio, bali kuleta maendeleo, yapo mengi yamekwama kwa sababu ya watendaji kutotekeleza wajibu wao vizuri, wapo viongozi wala rushwa na majizi wanaosababisha huduma za wananchi zinakuwa chini," alisema.
Alisema amekuwa waziri kwa miaka 20 na akiwa Waziri wa Ujenzi, amejenga kilomita 17,762 za barabara kwa kiwango cha lami, madaraja 12,000 kati yake makubwa ni 110, madaraja mapya makubwa yanayojegwa ni 16,000 na madogo 7,200.
Aidha, alisema fedha za mfuko wa barabara miaka 10 iliyopita zilikiwa bilioni Sh. 73 na kwa mwaka huu zimeongezeka hadi kufikia Sh. bilioni 866.63 lakini tatizo kubwa ni viongozi walafi kuzitafuna.
Pia aliahidi kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 231 za barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, kilomita 112 za barabara ya Sumbawanga hadi Kasana na nyingine ni Sumbawanga -Mpanda -Uvinza ili kurahisisha maendeleo ikiwamo kufanya biashara na nchi za Uganda, Kenya na nyinginezo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment