Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, August 5, 2015

Lowassa rasmi urais Ukawa.

  Duni Haji wa Cuf mgombea mwenza, Mbowe, Maalim Seif: Ushindi lazima.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (wa pili kushoto), akinyanyua mikono ya wagombea urais, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (kushoto) na mgombea mwenza Juma Duni Haji (wa pili kulia) kupitia chama hicho jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad. Picha: Seleman Mpochi.
Mkutano Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umempitisha rasmi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
 
Aidha, wajumbe wa mkutano huo wamempitisha Waziri wa Mindombinu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Duni Haji, kuwa mgombea mwenza wa Lowassa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Wagombea hao walipitishwa jana kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ambao ulithibitisha Ilani ya Uchaguzi ya Chadema.
 
Lowassa alijunga Chadema Julai 27, mwaka huu akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile alichoeleza kutoridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea urais ulivyoendeshwa na vikao vya juu vya chama tawala vilivyofanyika mjini Dodoma mwezi uliopita. Duni ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), alijiunga na Chadema ili apate fursa ya kuwa mgombea mwenza wa urais kwa sababu sheria ya vyama vya siasa na sheria ya gharama za uchaguzi hairuhusu vyama vya siasa kuungana.
 
Vyama vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD, vilianzisha ushirikiano wakati wa Bunge Maalum la Katiba na kuunda Ukawa, kutokana na kutoridhishwa na Bunge hilo lilivyokuwa likiendeshwa ili kukusanya nguvu ya pamoja ya kutetea maoni ya wananchi yaliyokuwamo ndani ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
 
WALIVYOPITISHWA
Wagombea hao walipitishwa kwa kupigiwa kura kwa utaratibu uliotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kwa kusema ndiyo au hapana tofauti na utaratibu wa siku zote wa kupiga kura kwenye karatasi. Utaratibu huo ulikubaliwa na wajumbe wa mkutano huo.
 
LOWASSA: HATUTAKUBALI KUIBIWA KURA
Lowassa akizungumza na wajumbe wa mkutano huo baada ya kupitishwa kuwa mgombea, alisema Chadema na Ukawa kwa ujumla watafanya kampeni za kistaarabu zisizokuwa za matusi na kejeli na kuishina CCM mchana kweupe.
 
Alisema wakati wa mikutano ya kampeni ambayo aliahidi kutembea nchi nzima katika majimbo yote, atahakikisha hakutakuwa na fujo zozote zitakazojitokeza na kutahadharisha wasiibiwe kura.
 
“Nitapita kila jimbo la nchi hii ili kuhakikisha tunapata kura nyingi za rais, wabunge na diwani, kama wewe ni mgombea kajiandae kabisa, nasistiza sina msamaria wa kushindwa hapa ila nina msamiati wa kushinda, yale yaliyotokea Kenya hayawezi kutokea hapa nchini kwetu cha msingi haki itendeke,” alisema huku akishangiliwa.
 
Alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara wenye asili ya kiasia wameingiwa na hofu na baadhi yao wameanza kukusanya fedha zao wakidhani kuwa kutatokea fujo na kuwahakikishia kuwa hakuna fujo zozote zitakazotokea wakati wa uchaguzi huu.
 
Lowassa alisema amefurahi kujiunga Ukawa na kuwahakikishia marafiki zake waliopo Zanzibar ambao wamekuwa wakimweleza kuwa mgombea urais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, atavunja Muungano ni uongo kwani hana mpango huo kabisa tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu.
 
“Nikiwa CCM nilisema hii ni safari ya matumaini, sasa ni safari ya mabadiliko nje ya CCM, Muungano huu wa Ukawa ni mzuri sana na Watanzania watuunge mkono ili tuichukue nchi mchana kweupe cha msingi ni mshikamano,” alisema.
 
Alisema aliamua kujiunga Chadema kwa kutambua kuwa kazi yeyote ya chama cha siasa ni kushika dola  na Chadema ni chama ambacho kimejiandaa vizuri kushika dola.
 
“Wanaosema kwamba Chadema haiwezi kuogoza nchi wanajidanganya, Tanu ilipewa nchi ikiwa na miaka saba, Chadema sasa ina miaka 23 tangu kuanzishwa kwake itashindwaje kuongoza nchi?” alihoji.
 
MAALIM SEIF: LOWASSA, DUNI WANASUBIRI KUAPISHWA
Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Lowassa anazo sifa zote za kuwa rais wa Tanzania na kwamba kwa jinsi Ukawa ulivyojipanga katika uchaguzi huu, Lowassa na Duni wasubiri tu kuapishwa.
 
“Lowassa ondoa wasiwasi, wewe ni Rais wa Tanzania anayesubiri kuapishwa, Duni, Makamu wa Rais anayesubiri kuapishwa, Maalim Seif  rais Zanzibar anayesubiri kuapishwa, watake wasitake watatoka wananchi wanataka mabadiliko,” alisema.
 
Hamad  akizungumzia kuhusu Muungano, alisema hana mpango wa kuuvunja kama inavyoelezwa na baadhi ya watu isipokuwa msimamo wake ni kuwa na muundo wa serikali tatu. 
 
Alisema yeye pamoja na viongozi wenzake wakishaingia madarakani kazi ya kwanza watakayoifanya ni kuhakikisha Katiba Mpya iliyokwamishwa na CCM inapitishwa ambayo ilitokana na maoni ya wananchi.
 
Kuhusu taarifa za kujiuzulu Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba, Hamad  alisema habari hizo zilizoripotiwa na gazeti moja (siyo NIPASHE), hazina ukweli kwa sababu hadi juzi saa 4:00 usiku alikuwa naye na hakumweleza jambo lolote kuhusu kujiuzulu.
 
“Wanataka kutuchafua, mimi ndiye Katibu Mkuu, Katiba yetu inaeleza wazi kiongozi wa kitaifa akitaka kujiuzulu ni lazima aandike barua kwa mkutano mkuu, lakini hadi sasa mimi kama Katibu Mkuu hakuna barua yoyote niliyoipata toka kwa Prof. Lipumba,” alisema.
 
DUNI: UMASKINI NI SERA, MTAJI WA CCM
Naye Duni akizungumza katika mkutano huo, alisema CCM haiwezi kuwasaidia Watanzania kuondokana na umaskini kwa sababu umaskini ni sera ya chama hicho.
 
“Sera ya umaskini ni sera ya CCM kwa sababu mwenye pesa huwezi kumtawala, CCM wanahakikisha Watanzania wanakuwa maskini ili waendelee kuwatawala,” alisema.
 
Alisema mwaka 1961 hakukuwa na masuala ya ujambazi, vikundi kama panya road na machangudoa, lakini mambo yote yameibuka kwa sababu CCM imeshindwa kuongoza nchi vizuri.
 
MAKAIDI: CCM WAKAE MKAO WA KUTAWALIWA
Mwenyekiti wa Taifa wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema kumpata Lowassa kugombea urais kupitia Ukawa ni sawa na kupata chombo, hivyo CCM wakae mkao wa kutawaliwa.
 
MBATIA: WATEULIWE WAGOMBEA WENYE SIFA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema ili kujenga heshima  ya Ukawa, lazima kuteua wagombea hususani wabunge wenye sifa, wa kweli, waaminifu, wacha Mungu na wanaochukia maovu.
 
Mbatia alisisitiza kuwa wakati wa uchaguzi huu, vyombo dola na majeshi visimamie misingi ya haki kwa sababu Taifa hili siyo la CCM pekee na kwamba vyama vinavyounda Ukawa vitahakikisha vinamsaidia Lowassa anaibuka na ushindi.
 
MBOWE: HATUTAKUBALI KUIBIWA KURA
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, alisema katika uchaguzi huo Ukawa haitakubali kuona wanaibiwa kura.
Alisema sheria ya vyama vya siasa na sheria ya uchaguzi zimekuwa ni kandamizi kwa vyama kwa sababu haziruhusu vyama kuungana, hivyo Ukawa itakapoingia madarakani itafuta sheria hizo.
 
Mbowe alisema vyama vya siasa ni vyombo vya uchaguzi na madaraja ya kuvusha Watanzania kwenda kwenye mabadiliko ya kweli.
 
“Siasa ni watu, chama cha siasa siyo mahakama, ndani ya Chadema tumejenga utamaduni wa kuishi kama familia, mwanachama anayejiunga leo ana haki sawa na yule wa zamani, ndani ya Chadema hakuna mkubwa,” alisema.
 
Aliongeza kuwa wanachama na viongozi wa Chadema waendelee kwapokea watu wanaotaka kujiunga na Chadema na yale mambo mabaya yaliyokuwapo katika vyama vyao vya awali waachane nayo na waje na mambo mapya ndani ya Chadema.
 
KAKOBE: HAKUNA KIONGOZI MTAKATIFU
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gosper Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, alisema tangu Chadema wametangaza kupata mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kumekuwapo maneno kwamba mbona mgombea huyo siyo msafi na kwamba maneno hayo ni ya uongo.
 
Alisema Watanzania lazima wafahamu kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu hachaguliwi Baba Mtakatifu wa kwenda kuongoza Kanisa Tanzania au Msikiti wa Tanzania, bali ni kuchagua kiongozi atakayesaidia kuinua uchumi na maendeleo ya nchi.
 
Askofu Kakobe alisema kama akitafutwa kiongozi ambaye ni mtakatifu, hatapatikana kwa sababu hakuna kiongozi au viongozi watakatifu.
 
“Tukisubiri mtakatifu tutakesha, kwa viwango vya mtakatifu hatutamuona, tunachagua mtu atakayetusaidia kiuchumi na kimaendeleo,” alisema.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa na mabalozi kutoka nchini mbalimbali, viongozi wa vyama vya siasa kutoka nchi za Msumbiji, Kenya na Denmark.
 
DUNI NI NANI?
Mgombea mwenza huyo alizaliwa Novemba 26, mwaka 1950 Zanzibar. 
 
Alianza masomo katika Shule ya Msingi Mkwajuni iliyoko Zanzibar kati ya mwaka 1959 hadi 1965. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Gamal Abdel Nassor (Beit El Ras) mwaka 1966-1969 na baadaye katika Shule ya Sekondari  Lumumba (Lumumba College), kwa masomo ya juu ya sekondari mwaka 1970 hadi 1971.
 
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikosoma Shahada ya Sayansi katika elimu mwaka 1972 hadi 1975.
 
Baadaye alisoma Stashahada ya Uzamili katika Elimu kati mwaka 1978 hadi 1979 Chuo Kikuu cha Reading, Uingereza.
 
Pia alisoma Stashahada ya Uzamili ya Biashara kati ya mwaka 1993- 1994 Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza.
 
Aidha, alisoma Shahada ya Uzamili kwenye Usimamizi wa Rasilimali mwaka 1994 -1995 Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza.  
 
Mgombea mwenza huyo vile vile alihudhuria kozi fupi fupi za Mipango ya Elimu Nigeria mwaka 1980 na ya  uchumi mwaka 1982 Japan.
 
Duni alikuwa mwalimu wa sekondari mwaka 1975, Ofisa Elimu mwaka 1976 hadi 1979 na kisha Katibu Mkuu Mipango mwaka 1980.
 
Aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda 1980 -1981, Katibu Mtendaji Tume ya Taifa ya Mipango na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Sukita mwaka 1980.
 
Alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Fedha mwaka 1997, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Mkunazini 1998 -2000.
 
Alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Cuf (Zanzibar) mwaka 1999, Mkurugenzi wa Fedha Cuf toka mwaka 2003, mgombea mwenza wa urais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi wa mwaka 1995, 200, 2005 na 2010.
 
Duni aliwahi kuwekwa kizuizini kwa tuhuma za uhaini Zanzibar. Yeye na wanachama pamoja na viongozi wa Cuf walikaa gerezani wakituhumiwa kutaka kuiangusha serikali ya Dk. Salmin Amour, kabla ya mahakama kutoa hukumu iliyokataa uwapo wa uwezekano wa kufanyika uhaini Zanzibar, kwa sababu ni sehemu ya Muungano.
 
Mwaka 2001/2002 Duni alikuwa mmoja wa viongozi wa Cuf waliohusishwa na mauaji ya askari polisi huko Pemba.
 
Amepitia misukosuko mingi akilinganishwa na wanasiasa wengine wengi Zanzibar, hali inayomfanya awe ni jabali la siasa za Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment