MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) chini ya mwamvuli wa Ukawa, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wamejipanga kushinda uchaguzi wa mwaka huu na CCM hakitakuwa na sehemu ya kutokea.
Maalim Seif aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar ikiwa ni mara yake ya tano tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Akiwa amesindikizwa na mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya mwamvuli huo Edward Lowassa, Maalim Seif alisema safari hii wamejipanga vya kutosha.
“Safari hii tumejipanga CCM hawana pakutokea na ikiwa uchaguzi wa huru na wa haki akishinda yoyote nitakuwa wa kwanza kumpongeza na kutambuwa ushindi wake,” alisema.
Alisema Ukawa ni imara na yeye kama mgombea yupo tayari kupambana na mgombea yoyote kati ya waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar akiwemo Hamad Rashid Mohamed ambaye ni mmoja wa waasisi wa CUF anayewania urais wa visiwa hivyo kwa tiketi ya ADC.
Alisema CUF inashangazwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kushindwa kufanya mabadiliko makubwa kwa watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kama alivyokuwa ameahidi baada ya matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwaka 2010.
“Nimeandika barua mara tatu kukumbusha ahadi yake hakuna chochote kilichofanyika, Secreteriet ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ipo vile vile watendaji walioharibu chaguzi zote ndio wale wale waliokuwepo sasa”, alisema Maalim Seif akiwa ameshika mikono kichwani.
Alisema anaamini ni vigumu kwa Dk. Shein kutekeleza ahadi yake kwa sababu inamnufaisha yeye na chama chake ndo maana hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwa watendaji wa tume hiyo.
Alisema kwamba iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kuingia Ikulu vipaombele vyake vikubwa ni kupambana na umasikini, kuweka msingi wa elimu bora, kufunguwa milango ya Uwekezaji na kutumia rasilimali za nchi kuwanufaisha wananchi kwa kuimarisha uchumi kupitia sekta ya mbali mbali ikiwemo uvuvi wa bahari kuu, anga, pamoja na nishati.
Kuhusu vigogo wa CCM wanaoendelea kujiunga na timu ya UKAWA alisema Chama Cha Mapinduzi kimepoteza mwelekeo na sio kile chama cha CCM cha zamani kwa vile kimeshindwa hata kuheshimu taratibu, kanuni na katiba ya chama chake.
“Lowassa na Sumaye wameamua kukiacha chama hicho kwa sababu wamefika pahali wameshindwa na uvumilivu na mwisho wake na sio chama tunachokijuwa kimeshindwa kupata katiba na kanuni zake”, alisema Maalim Seif na kuongeza hata mwalimu Nyerere alisema CCM sio mama yake au baba yake na wananchi wakikosa mabadiliko ndani ya chama watatafuta njia.
Katika mapokezi hayo mgombea wa urais wa muungano Edward Lowassa amewafunika viongozi wenzake kila alipokuwa akionekana na kushangiliwa kwa kishindo.
Wagombea wengine waliochukuwa fomu katika kituo cha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni mgombea wa Chama cha DP Abdalla Kombo Khamis, ambae alisistiza umuhimu wa kuwa na uchaguzi huru na wa haki, pamoja na kuahidi wananchi kushuhudia mabadiliko makubwa ya kiutawala na kiuchumi iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuingia Ikulu.
Kwa upande wake mgombea wa Jahazi Asilia Kassim Bakari Ali amesema kwamba Zanzibar inahitaji mabadiliko ndio maana amemuwa kuchukuwa fomu kugombea nafasi hiyo ili kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi na kujenga Zanzibar yenye uchumi imara.
Wagombea hao walikabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha ambae aliwataka wagombea wote kuzingatia masharti yaliyowekwa katika fomu hiyo ikiwemo kurejesha fomu kwa wakati pamoja na kuwasilisha fedha taslimu Sh milioni mbili.
/Mtanzania.
No comments :
Post a Comment