dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 3, 2015

Ubabe ubabe.

Naibu Waziri wa Kazi na Ajira na Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Milton Makongoro Mahanga.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira na Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Milton Makongoro Mahanga, ametangaza kuhama chama hicho na kukusudia kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Segerea, jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mahanga alisema ameamua kuchukua uamuzi huo mgumu kutokana na kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM jimboni humo.
 
“Hivyo basi, kuanzia leo tarehe 2 Agosti, mwaka 2015, mimi Dk. Milton Makongoro Mahanga, natamka kwamba si mwanachama tena wa Chama Cha Mapinduzi na ninakusudia kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo kama uongozi wa chama hicho utakubali kunipokea,” alisema Dk. Mahanga.
 
Kwa mujibu wa Dk. Mahanga, hana ugomvi wowote na wanachama wa CCM ndani ya jimbo hilo kwa miaka 15 sasa tangu achaguliwe kuwa mbunge wao mwaka 2000, isipokuwa mfumo mbovu wa chama hicho unaowapa vingozi wachache uhalali na kiburi cha kufinyanga demokrasia na kuendeleza dhuluma na hila katika kupata wagombea bora hivyo kukiangamiza Chama. Alisema iwapo angeshindwa kwa halali katika mbio hizo za kura za maoni ndani ya CCM katika jimbo hilo, asingekuwa na kinyongo chochote dhidi ya Bonnah Kaluwa, aliyedai kuibuka mshindi.
 
“Katika ushindani, kuna kushinda na kushindwa, lakini kwa hila na dhuluma hizi zilizofanywa na uongozi wa CCM ngazi ya wilaya na kata, ni wazi wanachama wa CCM Jimbo la Segerea hawakupewa haki ya kumchagua mgombea waliyemhitaji kubeba bendera ya chama chao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” alisema Dk. Mahanga na kuongeza:
 
“Kwa dhuluma na njama hizi, mimi Dk. Milton Makongoro Mahanga, nitakuwa najidanganya kwenye nafsi yangu na kuwadanganya wanachama na wananchi wa Jimbo la Segerea kwamba nitabaki ndani ya chama hiki na kushiriki kukipigania kwenye uchaguzi mkuu.”
 
Alisema ni imani yake kwamba viongozi na wanachama wa chama hicho ambao wamekasirishwa na vitendo vya kihuni, dhuluma na wizi wa kura  hizo, watamuunga mkono kwa uamuzi mgumu aliofanya ya kujiunga na chama kingine cha siasa na kuendeleza juhudi zake za kuwatumikia wananchi.
 
Kwa mujibu wa Dk. Mahanga, wagombea ubunge wa jimbo hilo akiwamo Bonnah, walianza kampeni tangu mwaka juzi huku uongozi wa wilaya wa chama hicho, ukiwa kimya licha ya yeye kupeleka malalamiko kwa uongozi wa CCM kuanzia ngazi hiyo, mkoa hadi Taifa.
 
“Licha ya malalamiko yote haya, uongozi wa CCM ulikaa kimya na baada ya muda mrefu eti ulichukua hatua ya kuwakanya Bonnah na wenzake kwa mdomo,” alisema Dk. Mahanga.
 
Alisema mchakato wa kura za maoni jimboni humo ulijawa na uchakachuaji katika madaftari ya wanachama kwa madai kwamba yaliingizwa (madaftari) kinyemela majina feki ya wanachama.
 
Aliongeza kuwa zaidi ya kadi mpya 5,000 ziligawiwa kwa wanachama feki kwenye jimbo hilo na kuruhusiwa kupiga kura za maoni.
 
Alidai baadhi watu waliofanikisha kuangushwa katika kura hizo ni makatibu kata, wilaya na kigogo wa chama ngazi ya taifa wa chama hicho. 
 
Tangu CCM itangaze mteule wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, baadhi ya wanachama wamekuwa wakihama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani.
 
Miongoni mwa waliochukua uamuzi huo ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye amejiunga na Chadema.
 
Lowassa tayari amechukua fomu ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba ridhaa ya Chadema agombee nafasi hiyo ya juu ya uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 
Wengine waliohama CCM na kujiunga na Chadema ni James Lembeli na Esther Bulaya.
 
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya  Rorya mkoani Mara, Pendo Odele, amehama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
Odele amedai kuwa amefikia uamuzi huo kutokana na kuchoshwa na manyanyaso anayofanyikwa na baadhi ya viongozi wa CCM.
 
Odele ambaye pia alikuwa Diwani wa Viti Maalum wa chama hicho wilayani humu, alifafanua kuwa amelazimika kuihama CCM na kujiunga na Chadema kutokana kuchoshwa na mmoja wa viongozi wa chama hicho tawala huku  akiongoza vikao vyake kibabe vya kamati ya siasa na halmashauri kuu ya chama hicho wilayani humu.
 
Alidai kiongozi huyo amekuwa akimchafua kwa madai kuwa CCM ilimsimamisha kuhudhuria vikao vyote vya Chama kwa mwaka mzima wakati si kweli.
 
Alisema amehamia Chadema na kukabidhiwa kadi ya chama hicho.
 
“Nawashukuru wanawake wa CCM walinipa ridhaa nikawa Mwenyekiti wa Wanawake na Diwani ni kwa sababu nilikuwa nawafaa, ila nimeamua kuondoka CCM na kuhamia Chadema kwa sababu nimechoka kuzongwazongwa," alidai Odela.
 
Aliongeza: “Kama Edward Lowassa, kigogo wa CCM hakutendewa haki, mimi nangoja nini? CCM hakuna demokrasia bali ni ubabe na rushwa."
 
Katibu wa Chadema Wilaya ya Rorya, Akechi Otuoma, alithibitisha kada huyo kuhamia kwenye chama chao.
 
Aliwataja wengine waliohama CCM kuwa ni Rose Choka, aliyekuwa Diwani wa Viti Maalum na Martin Goroba, aliyekuwa mtangaza nia kuwania udiwani wa kata ya Bukura.
 
Otuoma alisema Odele na Choka, wametangaza nia kuwania udiwani wa Viti Maalum kupitia tiketi ya Chadema na Goroba udiwani katika kata hiyo.
 
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawata) Wilaya ya Rorya, Mary Philipo, alisema amewapokea wanawake wenzake hao na kuwakaribisha zaidi kujiunga na chama hicho akisema hakina ubaguzi kwa wanachama wake.
 
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Samwel Kiboye, alisema kila mtu ana haki ya kujiunga na chama anachokipenda.
 
Kiboye alisema hakushangazwa kuhama kwa wanachama hao kwa kuwa wapo wakongwe wa CCM akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa na wafuasi wake wamehama katika chama hicho kwa maslahi yao binafsi.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment