dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 24, 2015

Dk Magufuli awapa pole Kikwete, Mkapa

Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
By Joyce Mmasi na Tumaini Msowoya, Mwananchi
Dar es Salaam. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amewapa pole Rais Jakaya Kikwete na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwa kuwateua watu wasiofaa.
Dk Magufuli alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani.
“Mheshimiwa rais, nisamehe naomba niseme hili, uliweka watu ambao hawafai, hawakutusaidia na wametuchelewesha kwenda mbele,” alisema Dk Magufuli.
Alidai kuwa watu hao walikuwa wakivaa sare za CCM nyakati za mchana huku usiku wakifanya ufisadi kwa kuwaibia Watanzania.
“Kuna viongozi ambao mchana walikuwa wanavaa sare za CCM na usiku wanafanya ufisadi, watu wa aina hii hawafai na bahati nzuri wameamua kuondoka wenyewe na hata wale waliobaki waondoke,” alisema.
Alisema ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano katika uchaguzi wa kesho, atahakikisha kuwa anapambana na tatizo la rushwa ikiwamo kuwabana watumishi wasioridhika na mishahara wanayolipwa.
“Wapo baadhi ya watumishi wasioridhika ambao hata wakilipwa Sh10 milioni wataendelea kuiba, watu wa aina hii wakiharibu Dar es Salaam sitawahamishia kwingine ila wataishia hapahapa,” alisema na kuongeza:
“Kungekuwa na uwezekano wa mtu kuapishwa kuwa rais kabla ya kupigiwa kura ningeanza kazi hata leo, kwa sababu lengo langu ni kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania wote bila kujali vyama, nitakuwa rais wa wote.”
Alisema anautumia ukali wake katika kutimiza wajibu wake na kwamba ikiwa ataingia madarakani, anatamani kuona wafanyakazi wote wanatimiza wajibu wao.
Aliahidi kushughulikia kero zinazowakabili wafanyakazi ikiwamo kupunguza makato ya kodi ya mshahara ili wamudu gharama za maisha.
Alisema tayari imeshaundwa tume kwa ajili ya kushughulikia kero za wafanyakazi, ambayo ikiwa ataingia madarakani, atahakikisha anafanya nayo kazi.
Bodaboda na Bajaji
Dk Magufuli aliwaahidi madereva wa bodaboda na bajaji kwenye miji ambayo hawaruhusiwi kuingia mjini kuwa atahakikisha anashirikiana na wataalamu kutafuta njia mbadala zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwenye maeneo yote.
Alisema bodaboda na bajaji kama walivyo wananchi wengine, wana haki ya kufanya kazi mahali popote nchini bila kujali mijini na nje ya miji.
“Nitaboresha mawasiliano ya uchukuzi ili miundombinu ya barabara iwawezeshe bodaboda kufanya kazi yao kila mahali bila kujali mijini kwa sababu wana haki,” alisema.
Machinga
Aliwaomba wafanyabiashara ndogondogo kuhakikisha wanawapigia kura wabunge wa CCM ili aweze kusaidiana nao katika kuandaa sheria ndogondogo zitakazowawezesha kufanya biashara zao bila bugudha.
Dk Magufuli alisema anachukizwa na ushuru usio wa lazima ambao umekuwa ukiwapa kero wafanyabiashara ndogondogo kiasi cha kushindwa kufanikiwa kiuchumi.
“Nitafanya kazi na watu wa chini kwa sababu nazijua kero za Watanzania, nimeamua kuomba urais kwa sababu nazijua changamoto,” alisema.
Maji
Kuhusu kero ya maji Dar es Salaam, Dk Magufuli aliahidi kuendeleza Mradi wa Maji wa Ruvu baada ya kesi iliyopo mahakamani kumalizika ili kuondoa kero hiyo.
“Mahitaji ya maji kwa Dar es Salaam peke yake ni lita milioni 500 kwa siku, wakati maji yanayotoka kwa sasa ni lita milioni 350, kiwango ambacho hakikidhi mahitaji,” alisema.
Alisema kama angekuwa waziri wa maji, angebomoa nyumba iliyosababisha mradi huo kukwama kabla kesi haijafikishwa mahakamani ili wananchi waondokane na kero ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa ugonjwa wa kipindupindu.
Kuhusu barabara, Dk Magufuli alisema akiingia madarakani, ataendeleza mradi wa ujenzi wa mradi barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ambao tayari hatua za awali zimeanza.
Alisema mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh6 trilioni, utakuwa na barabara sita za juu na kwamba utasaidia kuondoa msongamano wa magari.
Aliahidi kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza jiji la Dar es Salaam ikiwa atafanikiwa kuingia madarakani ili aweze kuendeleza sekta ya barabara na uboreshaji wa makazi.

Vipaumbele vingine
Licha ya ahadi hizo, Dk Magufuli alitaja kuondoa umaskini kwa kuanzisha viwanda vitakavyosaidia kuongeza ajira kwa vijana kwamba ni kipaumbele kingine.
“Tatizo la ajira litapungua ikiwa tutawekeza kwenye viwanda, naomba niwataarifu watu ambao waliwekeza kwenye viwanda na hawavifanyi kazi kuwa nikiingia madarakani viwanda hivyo nitawanyang’anya na kuwapa wenye uwezo wa kuviendeleza,” alisema.
Alisema mbali na mapambano yake dhidi ya rushwa, kipaumbele kingine ambacho atahakikisha anakifanyia kazi ni kudumisha ulinzi na amani miongoni mwa Watanzania.

Kikwete: Hakuna mwingine
Akimnadi Dk Magufuli, Rais Kikwete akisema CCM haikukosea kumteua waziri huyo kuwa mgombea urais kwa sababu kati ya wagombea wote wanane, hakuna mwenye sifa za kulingana naye.
Alisema mbali na uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii, pia Dk Magufuli ni mwadilifu na asiyeipenda rushwa.
Alisema kati ya wagombea wote wa nafasi ya urais hakuna mwenye ujasiri na aliyethubutu kukemea rushwa na ufisadi isipokuwa Dk Magufuli ambaye alisema amekuwa mstari wa mbele kueleza wazi anavyoichukia rushwa na atakavyowashughulikia mafisadi.
“Magufuli anatosha sana kuwa Rais. Sifa yake kubwa ni kiongozi mchapakazi anayesimama kuhakikisha anatekeleza alilolipanga… akiwa na jambo lake atahakikisha linakwenda vizuri,” alisema.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema hana wasiwasi wa Magufuli kukosa urais kwa kuwa anaamini Watanzania wamemkubali na watampa kura nyingi.
“Anapenda maendeleo ya Tanzania, anaumizwa na unyonge wa Watanzania, anakerwa na matatizo yao na ameeleza wazi namna atakavyokabiliana nayo na kuwatoa katika kero hiyo… hakika huyu ndiye rais anayewafaa,” alisema.
Aliwataka Watanzania kuliombea Taifa na kumuombea mgombea huyo wa CCM ili amalize kampeni zake salama na apate kura za kutosha kuapishwa kuwa rais wao.
Kikwete alisema sifa nyingine ya Magufuli ni kuzunguka nchi nzima na kuyatambua matatizo ya wananchi, kazi aliyosema ameifanya kwa ufanisi mkubwa ukilinganisha na wagombea wengine.
Aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuwachagua wabunge wa CCM ili kumwezesha Dk Magufuli kupata wasaidizi wanaomwelewa na watakaoendana na kasi yake.
“Tuchagulieni na wabunge na madiwani wa CCM, tunataka tupunguze wabunge wanaoandamana na kutoka nje ya Bunge na badala yake tupate wabunge wanaofanya kazi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana aliwataka Watanzania kumchagua Dk Magufuli ili aweze kutatua changamoto zote zinazowakabili.

No comments :

Post a Comment