dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 24, 2015

Lowassa: Mambo manne ya mabadiliko

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akiwahutubia wananchi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Benki, Kata ya Ruaha wilayani Kilosa mkoani Morogoro jana. Picha na Emmanuel Herman
By Peter Elias, Mwananchi
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chadema, anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa ametaja mambo manne atakayoshughulikia endapo wananchi watamchagua kuongoza Taifa akisema mambo hayo ndiyo msingi wa mabadiliko.
Lowassa, ambaye alisema hayo wakati akihutubia Taifa kwa kutumia vyombo vya habari, jana alihitimisha kampeni zake za mikoani kwa kufanya mkutano Ifakara, Ruaha na Mazimbu na leo anatazamiwa kufanya majumuisho ya kampeni za Chadema na vyama vinavyounda Ukawa- Umoja wa Katiba ya wananchi- kwenyeViwanja wa Jangwani kuanzia saa 6:00 mchana.
Katika hotuba yake ya usiku, Lowassa alisema Watanzania wamechoshwa na ahadi hewa ambazo zimekuwa zinazotolewa na CCM kwa miaka mingi sasa.
“CCM imekuwa madarakani kwa miaka mingi mno – zaidi ya nusu karne. Haina jipya,” alisema Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vya NLD, CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema vinavyounda Ukawa.
“Imechoka na haina pumzi ya kuongoza tena Taifa letu. Imebaki kuonyesha jeuri na kubeza tu. Imeishiwa nguvu ya hoja.”
Lowassa, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya awamu ya Nne aliyeihama CCM mwishoni mwa Julai mwaka huu, alitaja jambo la kwanza kuwa ni ukombozi mpya wa Mtanzania. Alisema hakuna maendeleo bila uhuru na haki. Alisema uhuru huo utapatikana endapo mwananchi atakuwa na madaraka kikatiba ya kuamua maisha yake.
Alisema CCM ilikwamisha ukombozi huo baada ya kuikataa Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Alisema anatambua juhudi kubwa zilizofanywa na watu wengi, akiwamo Jaji Joseph Warioba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume hiyo.
“Nikichaguliwa kuwa Rais, suala hili la Katiba mpya yenye maslahi kwa mwananchi litapewa kipaumbele,” alisema Lowassa ambaye ni miongoni mwa wagombea wananane wanaowania urais.
Jambo la pili, Lowassa alisema, ni ukombozi wa maisha ya mwananchi. Alisema wananchi hawawezi kuboresha hali za maisha yao kwa kupitia takwimu nzuri za Pato la Taifa ambazo hazionyeshi maisha halisi ya Mtanzania.
Alisema Watanzania hawali hizo takwimu bali wanataka kula milo mitatu yenye lishe bora; wanataka huduma bora za elimu, afya, maji safi na salama; wanataka umeme vijijini na ajira toshelezi kwa vijana.
“CCM na Serikali yake imeshindwa kuwapa wananchi wake hali bora ya maisha na hivyo kuwanyima furaha kama inavyobainishwa kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015 kuhusu hali ya furaha ya wananchi katika nchi mbalimbali, huku Tanzania ikishika nafasi ya 151 kati ya 156,” alisema.
Alitaja jambo la tatu kuwa ni mabadiliko ya uongozi na mfumo. Alisema wananchi wanataka uongozi wenye fikra mpya, utendaji wa kuaminika, uongozi wa uwajibikaji na uongozi shirikishi.
Alisema wananchi wanataka uongozi makini wenye ubunifu, upeo mpana na unaoongozwa na nidhamu na hasa ile ya matumizi mazuri ya fedha za Serikali kwa manufaa ya wananchi wote.
Aliwahakikishia wananchi kwamba uongozi wake na wa Maalim Seif Sharif Hamad wa Zanzibar si wa kuyumbishwa. Alisema ni uongozi wa kuthubutu katika utatuzi wa matatizo ya wananchi na wa uchapakazi na wa kuchukua maamuzi magumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Lowassa alisema jambo la nne kuwa ni kuheshimu, kulinda na kutetea Katiba ya nchi. Alisema atakuwa mfano wa uadilifu, atapiga vita vitendo vyote vya rushwa na ufisadi na atahakikisha kwamba rushwa inakuwa adui wa haki na maendeleo ya Taifa.
Kutekeleza mambo 16
Lowassa alisema Serikali yake itatekeleza pia mambo 16 ambayo ni pamoja na kupambana na ujinga, umasikini na maradhi. Alisema Serikali hiyo itaboresha elimu kama hatua ya kwanza ya kuwapa Watanzania uwezo wa kujikomboa.
Alisisitiza sera ya chama hicho ya kutoa elimu bora itakayogharamiwa na Serikali kutoka ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu. Alisema atapiga marufuku michango yote shuleni, kujenga maabara na kuboresha maslahi ya walimu.
Pia, alisema ataondoa kodi zote za kero kwa wafanyabiashara wadogo kama mamalishe, madereva wa bodaboda, na machinga. Pia, alisema ataondoa kodi zote za mazao kwa wakulima, wafugaji, na wavuvi ili kuongeze kipato na uwezo wao wa kuwekeza.
“Tutakuza na kulinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa makusudi ili waimarike na waweze kuhimili ushindani,” alibainisha na kuongeza kuwa Watanzania watapewa kipaumbele kwenye zabuni na manunuzi ya Serikali ili kuwajengea mazingira mazuri ya kibiashara.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kuongeza uzalishaji viwandani, kuboresha mfumo wa afya ya msingi na kinga. Vilevile alionyesha dhamira yake ya kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika au makampuni yote ambayo Serikali ina hisa na kuipa ofisi hiyo mamlaka kamili.
“Tutadhibiti matumizi Serikalini na katika mashirika ya umma kama kupiga marufuku matumizi ya magari ya anasa, kupunguza safari za ndani na nje, usafiri wa anga wa daraja la kwanza na semina na makongamano yasiyo ya lazima,” alisema.
Mambo mengine yatakayotekelezwa na Serikali yake ni kudhibiti vitendo vya rushwa iliyokithiri bandarini, kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika sekta ya umma na kuhakikisha kuwa rushwa, urasimu na kero zinazodumaza maendeleo ya wananchi zinakomeshwa, kwa mujibu wa Lowassa.
Lowassa aliongeza kuwa watatengeneza vyanzo vipya vya ajira kwa kukuza sekta za kilimo, viwanda na utalii na kuimarisha miundombinu na kujenga mtandao wa reli na kuunda upya Shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kibiashara.
Amani siku ya uchaguzi
Mgombea huyo wa Chadema aliwataka wananchi kutofanya fujo siku ya kupiga kura, badala yake wawe watulivu na wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili waweze kuiondoa CCM madarakani.
“Ninawaomba wote muwe wastaarabu, mheshimu sheria zilizopo. Hata wakati wote wa kampeni tumedhihirisha kwamba upinzani tunafuata sheria. Tuupige kura kwa amani na utulivu,” alisisitiza Lowassa.
Lowassa alilalamikia dhana inayojengwa na viongozi wa CCM kwamba wafuasi na wanachama wa Ukawa watafanya fujo wakati wa kupiga kura, akisema ni potofu. Dhana nyingine inayoenezwa na viongozi hao, alisema Lowassa, ni kama upinzani utashinda, nchi itaingia kwenye machafuko. Alisema viongozi hao wapuuzwe.
“Wote ni mashahidi kwamba chama cha UNIP cha Zambia kilipoondolewa madarakani kwa kura za ndugu zetu wa Zambia, hapakutokea fujo zozote. Chama cha Kanu cha Kenya pia kiliondolewa madarakani mwaka 2002 bila vurugu zozote. Ghasia za baada ya uchaguzi zilitokea miaka mitano baadaye,” alisema.
“Malawi nako, chama cha MCP kiliondolewa madarakani bila ghasia zozote. Kama ilivyotokea Zambia, Malawi na Kenya. Watanzania wamedhamiria kuleta mabadiliko kidemokrasia na kuiondoa CCM madarakani kwa kura zao.”
Amesikia matatizo ya wananchi
Katika hotuba yake, Lowassa alisema amesikia matatizo mengi ya wananchi katika kipindi chote ambacho ametembea nchini kufanya kampeni kwa kuwa amekutana na watu wa makundi mbalimbali.
“Nimesikia malalamiko ya wakulima na wafugaji kukosa maji na ardhi. Nimesikia kilio cha madaktari, wauguzi, walimu, askari na watumishi wa taasisi za umma kuhusu mazingira magumu ya kazi, kodi za juu na maslahi duni,” alisema.
Alisema jibu lake ni fupi, kwamba amesikia, ameona, ameelewa na atatenda. Aliwaomba wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kutimiza haki na wajibu wao wa kikatiba.
Akiwa Ifakara na Ruaha, Lowassa aliendelea kusisitiza ahadi zake kuwa Serikali atakayounda itatoa elimu bure, kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo, kuondoa kodi kwa wakulima na kuongeza ajira.
Akiwa Ruaha, Lowassa aliwaambia wananchi kuwa hakuna zawadi nzuri ambayo Watanzania watampa kama kura za urais.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Fatemu, Ruaha wilayani Kilombero, Lowassa alisema kuwa amemaliza kazi kubwa ya kuwasikiliza Watanzania na anachosubiri ni wampe urais ili afanye kazi.
“Zawadi kubwa ninayoisubiri ni ninyi kunipa kura za kutosha niwe rais wa Tanzania,” alisema Lowassa aliyetokea Ifakara kufanya mkutano mwingine wa kampeni.
Ukawa wajiandaa kuchukua nchi
Wakati Lowassa akisema hayo mkoani Morogoro, Ukawa imeunda jopo la wataalamu mbalimbali linaloongozwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu kuandaa mchakato wa kuchukua madaraka kutoka Serikali ya CCM.
Profesa Baregu, akiwa pamoja na mkurugenzi wa kampeni za uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa jopo hilo linawahusisha wasomi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, madaktari, wanasheria, watalaamu wa sayansi ya siasa na wanadiplomasia.
“Ni lazima tujipange ili tukichukua nchi tusianzie mwanzo kabisa. Lazima tukae tuitafsiri ilani ya uchaguzi, tujadili tutakuwa na wizara ngapi na zipi ziunganishwe na kutazama vipaumbele tutakavyovitekeleza siku za 100 za uongozi wetu. Tunataka kurudisha matumaini kwa Watanzania,” alisema Profesa Baregu.
Kwa upande wake, Munisi alisema kesho Ukawa itafungua kituo chake cha kuhesabu matokeo nchi nzima katika jengo la Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali ya Mtaa (LAPF) lilipo Kijitonyama, Dar es Salaam, kuwakaribisha watu wote watakaohitaji kujua matokeo ya Ukawa, huku akiitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufuata sheria na kutenda haki.
“Kituo kitakuwa na watendaji 800 na wengine watakuwa mikoani wakituma matokeo ya huko,” alisema Munisi na kuongeza kuwa wameshaapisha mawakala wake wote wa kila kituo.

No comments :

Post a Comment