Mambo mengi yameandikwa kuhusu uchaguzi huu kwa sababu ya dhana kwamba upinzani safari hii una nafasi nzuri zaidi ya kuondoa madarakani mojawapo ya vyama vikubwa na vyenye mtandao mpana barani Afrika –CCM.
Matukio mbalimbali yaliyotokea kuelekea kwenye uchaguzi huu yameongeza msisimko kwenye tukio hili kubwa. Lakini, kama tutakavyokuja kuona baadaye, ukweli halisi uko mbali kabisa na mihemuko tunayoiona.
Nikiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kampeni ya Taifa ya CCM, na kwa faida ya wale walio tayari kusikiliza hoja makini na kuzipima, nataka kueleza sababu 10 zinazotupa imani ndani ya CCM kwamba chama chetu kitaibuka na ushindi na Dk. John Pombe Magufuli, ndiye atakayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya uchaguzi huo wa Oktoba 25.
1. Kugombea kwa Edward Lowassa
Uchaguzi wa mwaka huu ulitarajiwa kuwa mgumu kwa CCM pasipo kujali ni nani ambaye kambi ya upinzani ingemsimamisha kugombea. Hata hivyo, matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu yaliamuliwa siku ambayo Ukawa walimchagua Edward Lowassa kuwa mgombea wao.Ni jambo ambalo linaweza lisieleweke kirahisi lakini ni ukweli. Kwa CCM, ni rahisi kushindana na Lowassa kuliko kama ingekuwa Dk. Wilbrod Slaa, aliyetajwa kuwa mgombea kabla Lowassa hajajiunga na Ukawa.
Ingekuwa ni vigumu zaidi kushindana na Slaa kwa sababu amejijengea heshima kama mwanasiasa mwenye maadili na asiye na kashfa yoyote ya ufisadi.
Hata kwa Lowassa mwenyewe, anapata shida sana kushindana na mfumo ambao yeye ni mmoja wa walioutengeneza, kuutumikia na aliokuwa akiuamini katika kipindi chote cha maisha yake ya utu uzima hadi Agosti mwaka huu.
Kwa CCM, ilikuwa vigumu kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wake kwa sababu katika miaka ya karibuni watu wamekuwa wakimwona ndiyo alama ya matatizo ambayo chama kinayo kwa sasa.
CCM ingepata shida sana kumuuza Lowassa kwa wananchi na kusema kuwa ndiyo alama ya Tanzania Mpya wanayoitaka. Kama wananchi wanaamini kwamba uchaguzi huu ni mgumu kwa sababu Lowassa amehamia upinzani, tunaamini ungekuwa mgumu mara kumi zaidi endapo ingemsimamisha yeye kuwa mgombea wake !
2. Wapinzani kuacha ajenda ya ufisadi
KATIKA kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010, kumekuwa na matukio mengi ya kuibuliwa kwa ufisadi na kushitakiwa mahakamani kwa watu wenye makosa ya rushwa. Vyombo vya Habari, Asasi za Kiraia na Bunge vimefanya kazi kubwa katika uibuaji wa vitendo hivi.
Rais Jakaya Kikwete ameweka historia ya kwa uamuzi wake wa kutaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iwe wazi na kujadiliwa bungeni – hiki ni kitu ambacho kilikuwa hakijawahi kufanywa huko nyuma.
Lowassa mwenyewe ni mmoja wa waathirika wa vita dhidi ya rushwa kwenye urais wa Kikwete kwani alishinikizwa kujiuzulu Uwaziri Mkuu kutokana na kashfa ya ufisadi ya Richmond.
Pamoja na kujizulu kwa Lowassa, wapo mawaziri waliofukuzwa kwa sababu hizohizo na sasa kuna mawaziri wa zamani wawili wanatumikia kifungo jela kwa sababu ya makosa yanayohusiana na rushwa.
Haya ni mambo ambayo hayakuwahi kutokea kabla Rais Kikwete hajaingia madarakani.
Sasa wananchi wana mwamko kuhusu masuala ya rushwa. Vyama vya upinzani vilijijenga sana miaka michache iliyopita kwa sababu ya kuwa wasemaji wakuu wa suala hilo.
Kimsingi, kukua kwa upinzani nchini kunahusishwa sana na tukio la mwaka 2007 ambapo vyama vya upinzani vilifanya mkutano jijini Dar es Salaam na kutangaza kile kilichokuja kujulikana kama Orodha ya Mafisadi.
Orodha hiyo ilikuwa na majina ya wanasiasa wanaotajwa kama vinara wa ufisadi hapa nchini. Jina la Edward Lowassa lilikuwa la kwanza miongoni mwa majina hayo na kwa miaka nane iliyopita, wapinzani wamekuwa wakilitumia jina la mgombea wao huyo wa sasa kama alama ya rushwa ndani ya CCM.
Uchaguzi huu ungekuwa mgumu kwa CCM kama wapinzani wangeufanya wa kujadili ufisadi hapa nchini. Uchaguzi ungekuwa mgumu zaidi kwa sababu tayari wananchi wanalielewa jambo hili na kufahamu namna linavyowauma.
Lakini, kwa uamuzi wao wa pupa wa kumchagua mwanasiasa ambaye wao wenyewe walitumia muda wao mwingi kumtaja kama fisadi mkuu hapa nchini, maana yake ni kuwa wameamua kuachana na ajenda ya ufisadi.
Kilichofuata baada ya kumchukua Lowassa kinaweza kufananishwa na maigizo. Wale wanasiasa wa upinzani waliojijengea jina na kuonekana mashujaa kama wapinga ufisadi sasa wameamua kula matapishi yao.
Wengi wao ambao walikuwa wakitumia sana mitandao ya kijamii kumchafua na kumtukana Lowassa kwenye siku za nyuma wameamua kufuta maandishi yao –wakisahau kuwa kumbukumbu bado zipo.
Ni wanasiasa wawili tu wa upinzani –Slaa and Profesa Ibrahim Lipumba (ambao wamekuwa vinara wa upinzani tangu miaka ya 1990) ndiyo ambao walijiuzulu nyadhifa zao kupinga Ukawa kumsimamisha Lowassa kama mgombea wake wa urais.
Matokeo yake, sasa mgombea wa CCM, John Magufuli, ndiye pekee anayezungumza habari za kupambana na rushwa mara kwa mara, kwa ujasiri na bila kupepesa macho.
Jioni moja ya mwezi Agosti mwaka huu, nilimwona mbunge kutoka upinzani, Peter Msigwa, akihojiwa na kituo cha televisheni hapa nchini ambako alisema kabla ya kumpitisha Lowassa walifanya utafiti ulioonyesha kuwa “Kwa sasa rushwa si tatizo hapa nchini”.
Aliendelea kwa kuwataka watu wenye ushahidi wa ufisadi wa Lowassa waende mahakamani. Alisema hivyo akisahau kwamba wakati wakitangaza orodha yao ya mafisadi mwaka 2007, upinzani ulidai kuwa una ushahidi wa madai hayo.
Huko nyuma, CCM pia ilikumbwa na matatizo hayahaya ya Ukawa na ikataka wapinzani walete ushahidi wao kuhusu Lowassa. Hata hivyo, kwenye masuala ya ufisadi wa viongozi, tuhuma pekee zinamwondolea mtu uhalali wa kuongoza hata kama ushahidi wa kweli hauonekani.
Ndiyo maana, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipata kusema huko nyuma kwamba mke wa Kaisari hatakiwa hata kutuhumiwa kwa uovu.
Chama cha siasa kilichoacha sera ambayo imekipandisha juu kwenye macho ya watu na kukubalika na wapiga kura kinawezaje kuzitelekeza sera hizo na bado kikataraji kushinda uchaguzi?
Haya ni maajabu !
3. Mabadiliko Yasiyo Mabadiliko
Wakati unapotembea jijini Dar es Saaam, utaona mabango mengi ya kampeni kwa vyama vya upinzani yakiwa na ujumbe “Mabadiliko”. Lakini, kama umehudhuria mikutano yao na kusikiliza hotuba za wazungumzaji wakuu, hutasikia lolote zaidi ya kelele na hasira. Wazungumzaji wawili wakuu wa kampeni za Ukawa ni watu waliowahi kuwa mawaziri wakuu hapa nchini; Lowassa na Frederick Sumaye.
Lowassa anafahamika zaidi kutokana na kashfa mbalimbali za ufisadi zinazohusishwa naye na Sumaye ni Waziri Mkuu mwenye sifa ya kutofanya lolote akiwa madarakani kiasi cha wananchi kumpa lakabu (jina la utani) ya “Mr Zero”.
Watu hawa, kwa namna walivyo, kwa matendo na maneno yao, hawawakilishi Mabadiliko. Hoja kubwa ya wapinzani ni kwamba CCM haijafanya chochote kwenye miaka 50 ya kujitawala kwa Watanzania.
Viongozi wawili wa juu ndani ya chama na serikali waliowahi kupata nafasi ya juu ya uongozi ya Uwaziri Mkuu wanapozungumza hayo majukwaani wanakuwa hawaisemi serikali pekee bali pia wanaonyesha wananchi kuwa wao wenyewe hawafai kupewa nafasi. Hii ni kwa sababu nao ni sehemu ya uongozi wa juu wa nchi ndani ya miaka hiyo 50.
Ni rahisi kuona kwamba wanasiasa wa namna hii wanapozungumzia mabadiliko hawazungumzii mabadiliko ya wananchi bali ya kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine au kubadili mavazi ya chama.
Nimesikiliza kwa makini na kwa muda mrefu hoja za wapinzani kuhusu Mabadiliko na ninachokiona ni kwamba wanachotaka wao ni kuiondoa CCM madarakani. Wapinzani wameshindwa kuwaonyesha Watanzania picha ya matumaini watakayoyaleta endapo watachaguliwa.
Badala yake, kampeni yote ya Ukawa imeelekezwa kwenye kumsaidia Lowassa, ambaye anaonyesha dhahiri kuwa amechoka, kuingia madarakani pekee.
Kadri muda wa kupiga kura unavyokaribia, ndivyo Watanzania wanavyozidi kuufahamu ukweli huu. Na kwa kufananisha historia ya utendaji na muda waliotumika ndani ya chama na serikali, Watanzania sasa wameanza kuona ni nani baina ya Magufuli na Lowassa kweli anawakilisha Mabadiliko.
4. Migogoro ndani ya Ukawa
Kila unapofika wakati wa uchaguzi hapa nchini, vyama vya upinzani hujitahidi kutafuta namna ya kuunganisha nguvu lakini mara zote jitihada hizo huwa hazifanikiwi. Mara hii wamepata jambo la kuwaunganisha ambalo ni mfumo wa Serikali Tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Awali, vyama hivi viliunganishwa na nia yao ya kutaka mapendekezo ya Tume yafuatwe. Baadaye, walipoamua kuufanya muungano wao kuwa wa kutafuta madaraka, walikubaliana kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi zote zinazowaniwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kwenye utekelezaji wa makubaliano yao ndipo sasa matatizo yakaanza kujitokeza. Wakaamua kuvunja taratibu zao zote walizojiwekea kwenye kumpata mgombea mmoja anayefaa wa nafasi ya Urais na badala yake wakamchukua mwana CCM aliyekatwa kutoka kwenye mchakato wa ndani ya chama chake.
Iliaminika kwama kitendo cha Lowassa kuhamia upinzani kingekigawa CCM mapandemapande kwa vile angeondoka na vigogo wengine wa juu wa chama hicho. Hata hivyo, sasa inaonekana kuwa Ukawa ndiyo wameumia kwa vile viongozi wake wa juu zaidi; Dk. Wilbrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CUF, ndiyo hatimaye waliohama vyama vyao.
Kama hilo halitoshi, makubaliano waliyoyafikia kwenye ngazi ya ubunge nayo hayaheshimiwi. Badala ya ushirikiano, sasa kumekuwa na tuhuma, majungu na vurugu.
Mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, alilazimika kuondolewa na askari kutoka jukwaani wakati alipokuwa Masasi mkoani Mtwara akimnadi mgombea aliyepitishwa na ‘wakubwa’ lakini wananchi wakawa hawamtaki na wakisema wako tayari kuipigia CCM.
Katika Jimbo la Nzega mkoani Tabora, viongozi wa kitaifa wa Ukawa walilazimika kuhoji umma juu ya mgombea wanayemtaka miongoni mwa wawili waliokuwa wakishindana. Kwa ujumla, umoja huu umezua mvurugano utakaoisaidia CCM kupata matokeo mazuri hata katika maeneo magumu.
Lakini, kilele cha unafiki wa kisiasa wa Ukawa kwa watu waliokuwa wakiunga mkono kundi hilo wakiwamo wanaharakati ni hatua yake ya kumuunga mkono mwanasiasa aliyekuwa kinara wa kupinga mapendekezo ya Jaji Warioba kuwa mgombea wake wa urais.
Kwamba, inakuaje umoja uliojengwa kwenye misingi ya kutetea mapendekezi ya Tume ya Katiba umchague mtu aliyeyapinga mapendekezo hayo kwa nguvu zote kuwa mgombea wake?
Kwa kundi la watu ambao kwao misingi ni kila kitu na madaraka si kitu, tabia hii ya Ukawa kusahau misingi kwa lengo tu la kupata madaraka linaonekana kama ulafi wa madaraka na si Mabadiliko ambayo wananchi wanayataka.
Wakati viongozi wa Ukawa wakijitahidi kuonyesha sura za tabasamu na matumaini kwenye majukwaa ya kisiasa, wanatumia muda mrefu zaidi kusuluhisha migogoro baina yao kuliko muda wa kupanga namna ya kuleta Mabadiliko.
Kama Ukawa wanashindwa kukubaliana kuhusu namna ya kusimamisha wagombea hata katika ngazi za chini kama majimbo, itakuaje utakapofika wakati wa kuunda serikali.
Bahati nzuri kwa Watanzania ni kwamba uwezekano wa hilo kutokea (la Ukawa kushinda) ni sawa na alama sifuri.
5. Ukawa kushindwa kufika nchi nzima
Kwa sababu zinazojulikana vizuri kwa viongozi wa Ukawa, Lowassa ameshindwa kufanya kampeni ya kuzunguka nchi nzima kama anavyofanya Magufuli.
Anachofanya Lowassa ni kutembelea mji mkuu wa mkoa kwa njia ya anga na kufanya mkutano. Akimaliza mkutano huo mkubwa anachagua maeneo mengine mawili ya kufanyia mkutano ambako pia anakwenda kwa usafiri wa anga. Baada ya hapo anarejea Dar es Salaam.
Kwa mfano, wakati Mkoa wa Tanga una majimbo tisa ya uchaguzi, Lowassa alifanya kampeni kwenye majimbo matatu tu. Mkoani Ruvuma, Lowassa alitembelea majimbo matatu kati ya tisa. Mkoani Kigoma, alitembea majimbo mawili tu kati ya tisa. Hali kama hiyo iko katika mikoa mingi mingine.
Kwa upande wa Magufuli, hali sasa ni tofauti. Tangu kuanza kwa kampeni Agosti 23 mwaka huu, mgombea huyo wa CCM amezunguka katika mikoa yote na majimboni takribani mbalimbali kwa kutumia usafiri wa barabara.
Anatumia barabara kuhutubia na kufanya kazi za kisiasa mtaa kwa mtaa na kijiji kwa kijiji na kwa siku anahutubia wastani wa mikutano nane hadi 12.
Hadi sasa, kwa sababu ya tatizo kubwa la ufikaji kwa wakati wa taarifa muhimu, kampeni za aina hii ya Magufuli zina nguvu na ushawishi sana. Mikutano ya Lowassa inavutia watu wengi kwenye miji miji mikubwa. Kwa upande wa Magufuli, yeye anapata watu wengi mijini na vijijini.
Kama kigezo cha kushinda kwenye uchaguzi huu ni wingi wa watu kwenye mikutano, basi hivi sasa tayari CCM imeshinda uchaguzi. Lakini, tofauti na upinzani, CCM haipumbazwi na umati unaohudhuria mikutano yake.
CCM ina kumbukumbu nzuri ya mikutano mikubwa na iliyoweka rekodi wakati Augustine LyatongaMrema, mgombea wa upinzani mwaka 1995, alipokuwa na ushawishi mkubwa.
Pamoja na kuvuta maelfu ya watu kwenye mikutano yake, bado Mrema alishindwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa. Nguvu ya CCM iko kwenye sehemu nyingine ambayo ndiyo mada inayofuata hapa chini.
6. Mtandao wa CCM
Hadi sasa, hakuna chama hapa nchini, na pengine barani Afrika, kinachoweza kujisifu kuwa na mtandao mpana kuliko CCM. Wakati Ukawa wakiwa wanapumbazwa na umati kwenye mikutano yake, CCM inajivunia mtandao wake wenye kiongozi katika kila nyumba kumi hapa nchini.
Wanachama na wapenzi wa CCM hawahitaji kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya kuonyesha kina wafuasi kila mkoa. Ukweli ni kuwa CCM iko kila mahali hapa nchini.
Wakati Ukawa wakihangaika na siasa za majukwaani pekee, CCM inaendelea na kampeni zake majukwaani na katika ngazi za chini kabisa, mbali na kamera za vyombo vya habari. Kwa wanaojua namna CCM inavyofanya mambo yake, hawashangazwi na ushindi kinaopata kwenye chaguzi.
Kwenye miaka ya 1950 wakati wa mapambano ya kudai uhuru, TANU ambayo ndiyo baba wa CCM, ilitengeneza mtandao huu kwa ajili ya kuwaunganisha wananchi. Mwalimu Nyerere na wenzake walitengeneza mtandao huu kwa ajili ya kuisaidia CCM katika nyakati za uchaguzi kama hizi.
Wakati mijadala hapa nchini ikiwa imetawaliwa na kashfa mbalimbali za ufisadi dhidi ya viongozi wa CCM –na wengine wakisema chama kikiwa katika hali yake ya chini zaidi katika historia yake mwaka jana, CCM iliibuka na ushindi wa asilimia 81 dhidi ya upinzani kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
7. Usafi wa Magufuli
Mwaka jana, baadhi ya rafiki zangu wanahabari waliniambia kwamba ndani ya CCM, hakuna mwanasiasa mgumu kumshambulia na kummaliza kuliko Magufuli. Ana rekodi katika jamii kama msafi, mchapakazi, asiye na mzaha na mwenye kupata anachotaka.
Hajawahi kuwa mtu mwenye tabia za kawaida zinazohusishwa na wanasiasa hapa nchini. Watu walishangazwa hata na ule ukweli kwamba alijitokeza kuwania urais. Na hata alipojitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa, hakuwa na mbwembwe.
Uteuzi wa Magufuli unafanana na ule wa Mkapa mwaka 1995. Chama kikiwa kwenye wakati mgumu wa mpinzani aliyekuwa mwana CCM kabla (Mrema), chama kiliamua kupitisha mgombea mwenye rekodi isiyo na shaka na asiye na doa.
Siku zote, CCM imekuwa hodari katika kupata mgombea ambaye hajatarajiwa na wengi lakini mwenye uwezekano mkubwa wa kushinda uchaguzi.
Ndiyo maana, hata mashambulizi ya Ukawa hivi sasa yanaelekezwa zaidi kwa CCM kuliko Magufuli. Hawana namna nyingine na hoja yao kubwa ni kwamba imekaa madarakani kwa muda mrefu.
Ikrari, kuna watu ambao wanaweza kukubaliana na hoja hii. Lakini, tatizo ni kwamba wanapoambiwa wafanye uchaguzi kati ya Magufuli na Lowassa, wanamchagua Magufuli.
8. Mafanikio ya CCM Vijijini
Mimi ni Mbunge wa Jimbo ambalo mgombea Urais wa CCM alishinda kwa asilimia 85 mwaka 2010 wakati ushindi wake kitaifa ulikuwa asilimia 61. Kwenye uchaguzi huu, nataraji Magufuli atashinda kwa asilimia 88 jimboni kwangu.
Majimbo kama ya kwangu yako mengi nchini Tanzania. Hii ni kwa sababu vyama vya upinzani vinawaona wananchi wa vijijini kama watu wajinga na wasio na ufahamu na ndiyo maana siku zote wanaipigia CCM.
Kudhani kwamba watu hawa ni wajinga kwa sababu tu wanaipigia kura CCM ni makosa. Mahali kote duniani, watu hupiga kura kwa sababu ya maslahi yao. Mwaka 2000, vijiji vinne tu katika jimbo langu vilikuwa na umeme, leo vijiji 44 vina umeme.
Bado hatujafikia kiwango kizuri kinachotakiwa na kila mtu lakini ukweli ni kwamba tumepiga hatua kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Watoto wengi hivi sasa wako shuleni kuliko majumbani, kuna wauguzi wengi kuliko zamani, zahanati nyingi zaidi, shule nyingi zaidi, barabara nyingi zaidi zimetengenezwa na huduma za mawasiliano zimekuwa bora zaidi.
Kimaendeleo, bado hatujafika Makkah lakini hoja inayosemwa sana na wapinzani kwamba CCM haijafanya chochote kwa wananchi haiingii akilini kwa wananchi hao wanaoona tofauti kwenye maisha yao.
Matokeo yake, wanawaamini zaidi wagombea wa CCM wanaosema watafanya mengi zaidi kwa sababu tayari wameona nini kinafanyika kwao hivi sasa.
9. Muda wa Kuzungumza
Uchaguzi hauamuliwi na ahadi pekee bali ni nani anayezitoa na anazitoa kwa namna ipi. Msingi wa hili unaanzia katika siku ya kwanza ambayo mgombea na chama chake alitoa ahadi kwa chama chake.
Kufahamu hili, mtu anatakiwa kufanyia uchambuzi ufunguzi wa kampeni uliofanywa na Lowassa na Magufuli. Mgombea wa Ukawa alizungumza kwa dakika tisa, alizozitumia pia kuahidi kuachia huru wabakaji watoto na watuhumiwa wa ugaidi ambao masuala yao tayari yanashughulikiwa na vyombo vya dola.
Magufuli alizungumza kwa dakika 58, akieleza kwa undani ahadi zake kuhusu elimu, ajira, afya, rushwa, huduma za maji na miundombinu. Tangu hapo, mikutano yote ya Magufuli imebeba ajenda hiyo kwenye maudhui na muda uliotumika.
Watu wanaondoka kwenye mikutano ya Magufuli wakiwa na matumaini na ari lakini wanaokwenda kwenye mikutano ya Lowassa wanaondoka kwenda nyumbani wakiwa wamechanganyikiwa.
Siku ya kupiga kura, wananchi wanakumbuka namna mgombea alivyoonekana na kusikika. Wanakumbuka walijisikia namna gani wakati mgombea alipokuwa akizungumza.
Tukumbuke, kuna mikutano ambayo kwa sababu hii au ile, mgombea wa Ukawa hakuzungumza kabisa ingawa wananchi walikuwa wamemsubiri kwa hamu azungumze.
Kwenye eneo hili, nadhani wapiga kura watamkumbuka zaidi Magufuli wakati watakapokuwa wanakwenda kupiga kura.
10. Namba hazidanganyi
Tanzania na Watanzania kwa ujumla wake, hawana utamaduni wa kutumia kura ya maoni kwenye mambo yao. Hata hivyo, kwenye masuala ya kimsingi ya kisera, nchi yetu ina utaratibu wa kutafuta kwanza maoni ya watu. Mfano ni Kura ya Maoni wakati tulipotaka kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi na pia hata Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwaka 2005, utafiti uliofanywa na taasisi moja ulibashiri kwamba CCM ingepata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi huo na kwa hakika chama kikaja kupata ushindi wa asilimia 80.
Mwaka 2010, taasisi ya Synovate-Ipsos ilibashiri kwamba CCM ingeshinda kwenye Uchaguzi Mkuu lakini ingepata asilimia 61 tu ya kura. CCM wakati huo ilipingana na utafiti huo kwa madai kwamba kiwango hicho kilikuwa kidogo.
Wakati wa uchaguzi ulipofika, CCM ilishinda kwa asilimia 61 !
Hivi karibuni, matokeo ya tafiti mbili yameanikwa hadharani. Matokeo hayo yametolewa na taasisi mbili ambazo ni maarufu na zinazoheshimika kwenye eneo la utafiti na mambo ya kura za maoni; yaani TWAWEZA na IPSOS.
Pamoja na kwamba taasisi hizo ni tofauti, zinazotumia njia tofauti kufanya mambo yao, zikifanya utafiti kwa nyakati tofauti na mbinu tofauti; wote wameibuka na jibu moja kwamba CCM itashinda kwa zaidi ya asilimia 62.
Kwa sababu zozote zile, mtu anaweza kupingana na hoja nyingine tisa nilizozitoa kueleza kuhusu ushindi wa CCM lakini si hii. Hii ni kwa sababu, kwa kawaida, namba huwa hazisemi uongo.
Ni kweli kwamba kwenye utafiti wowote ule unaofanyika, kuna wapiga kura ambao wanakuwa hawajafanya maamuzi. Hata hivyo, kwa sababu tisa nilizozitoa hapo kabla, ni wazi kwamba wapiga kura hawa ambao hawajaamua mpaka sasa, wana uwezekano mkubwa wa kuipigia kura CCM kuliko Ukawa.
Ni kweli, kura za maoni zinaweza kuwa na kasoro za hapa na pale na watu hawatakiwi kuangalia sana matokeo ya kura za maoni.
Ukweli unaoumiza ni kwamba, hoja hiyo hutolewa na wale ambao kura za maoni zinaonyesha kuwa wanashindwa.
Mwandishi wa makala haya January Makamba ni mjumbe katika Kamati ya Ushindi ya Mgombea Urais kupitia CCM John Magufuli.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/magufuli-anashinda-sababu-10-ni-hizi#sthash.uw04q6lv.dpuf
No comments :
Post a Comment