Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 27, 2015

Morogoro kigugumizi matokeo ya uchaguzi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).
Wasimamizi wa Uchaguzi katika majimbo mbalimbali ya Uchaguzi mkoani Morogoro, wameendelea kuwa na kigugumizi juu ya kutangaza matokeo ya uchaguzi katika maeneo yao huku wakibainisha kuwa changamoto za kijiografia katika maeneo mengi kukwamisha hali hiyo kufanyika kwa wakati.
Hata hivyo, katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi, Chama Cha Mapinduzi kimeonekana kujizolea viti vingi vya udiwani ingawa maeneo mengine wagombea wake wameshindwa kutetea nafasi zao na viti hivyo kunyakuliwa na wagombea wa vyama vya upinzani vikiwamo vile vinavyoungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na ACT-Wazalendo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mvomero, Wallace Karia, alisema jimbo hilo lina kata 30, lakini moja ya Mvomero haikufanya uchaguzi baada ya mgombea wake mmoja wa udiwani kufariki dunia wakati wa mchakato wa kampeni.
Alisema kati ya kata 30, kata 22 zimenyakuliwa na CCM huku kata mbili za Diongoya na Bunduki, wagombea wake walipita bila kupingwa na saba zikichukuliwa na vyama vya upinzani.
Karia alisema kata zilizonyakuliwa na Chadema ni Chenzema, Nyandira, Mtibwa na Hembeti zilizochukuliwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na Kikeo na Liwale zikienda kwa ACT Maendeleo na kata ya Mangae ikichukuliwa na CUF. Kwa matokeo ya ubunge ambayo katika jimbo hilo, vyama sita ya CCM, Chadema, DP,ACTna UPDP vilisimamisha wagombea.
Hata hivyo, alisema bado wanaendelea kujumlisha kwa njia ya kilektroniki.
Lakini mchuano mkali ulikuwa ni kwa wagombea wa CCM na Chadema.
Akizungumza kwa njia ya simu, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ulanga, zamani Ulanga Mashariki, Isabela Chilumba, alisema wamefanya uchaguzi wa nafasi ya madiwani na Raisi pekee, huku nafasi ya ubunge ikiachwa hadi pale Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakapotangaza upya, baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Celina Kombani.
Alisema jimbo hilo lina jumla ya kata 21, na sita zilichukuliwa na Chadema, huku zilizobaki zikichukuliwa na CCM.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Malinyi zamani likiitwa Ulanga Magharibi, Said Msomoka, alisema Dk. Haji Mponda, aliyekuwa akitetea kiti chake kutoka CCM, alikuwa akiongoza kwa kura nyingi ikilinganishwa na wapinzani wake.
Aidha, alisema kati ya kata 10 zilizopo kwenye jimbo hilo jipya la uchaguzi, kata nne zilichukuliwa na Chadema ikiwamo Kilosa kwa Mpepo, Bilo, Ngoheranga na Itete Minazini, huku sita zilizosalia zikichukuliwa na CCM.
Msomoka alisema changamoto ya jiografia ya maeneo pia iliwachelewesha kufanikisha majumuisho kwa haraka, hasa kwa kata za Itete, Sofi na Kilosa kwa Mpepo kuchelewa kufikisha matokeo.
Kwa upande wa Jimbo la Kilosa Kati lenye jumla ya kata 25, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Iddi Mshihiri, alisema kata tatu zilichukuliwa na Chadema na 22 CCM, huku Jimbo la Mikumi, kati ya kata 15 zilizopo, nne zilichukuliwa na Chadema na nane CCM na kata tatu za Vidunda, Ulaya na Kilangala, walichelewa kufikisha matokeo kutokana na jiografia ya maeneo hayo.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kilombero na Mlimba Azimina Mbilinyi, naye alikiri jiografia ya wilaya hiyo kuchelewesha zoezi zima la kupata matokeo na majumuisho ya kura na kwamba kwa vile njia ya uwekaji matokeo ni ya njia ya kielektroniki, ilihitaji umakini wa hali ya juu ndipo atangaze matokeo, jambo ambalo pia lilibainishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Gairo, Mbwana Magota, aliyedai kata za Nongwe, Magoyeko na Chagongwe zilisababisha zoezi hilo kuchelewa.
Aidha, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Kusini  yenye kata 17 na Morogoro Kusini Mashariki yenye kata 14, Yona Maki, alisema pia tatizo hilo la jiografia ya maeneo na mvua iliyonyesha jana maeneo hayo, zilisababisha matokeo kuchelewa kupatikana kwa wakati hususan jiografia katika kata za Mkuyuni, Tegetero, Singisa na  Bwakila Juu.
Manispaa ya Morogoro hali ilikuwa tofauti zaidi, ambapo Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Morogoro Mjini,Theresia Mahongo, alipohojiwa sababu za kuchelewesha kutangaza matokeo ilihali wapo mjini, alidai wana kata 29 ambazo ni nyingi na baadhi ya maeneo zilizuka vurugu zilizosababisha baadhi ya maeneo wasimamizi wa vituo na mawakala kuahirisha zoezi la kuendelea kuhesabu hadi asubuhi na kwamba kikwazo cha usafiri na jiografia ya maeneo kwa manispaa hakikuwapo kabisa.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment