Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema anashangazwa na uonevu unaofanywa na Polisi kwa kuwakamata vijana 191 waliokuwa wakikusanya matokeo kadri yanavyotangazwa kwa nia ya kujua mwenendo wa uchaguzi wa chama chao huku wakidai kuwaweka ndani kwa kosa la ‘human trafficking’ (usafrishaji binadamu) lisilohusiana kabisa na kile walichokuwa wakikifanya, yaani kujumlisha matokeo ili hatimaye kuyalinganisha na yale yatakayotangazwa mwishoni.
Lowassa anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, alisema hatua ya polisi kuwakamata vijana hao wa Chadema ni uonevu wa wazi.
Alisema vijana hao walikamatwa katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam wakiwa na kompyuta zao.
Mgombea huyo alisema vijana hao wanashikiliwa katika kituo cha polisi Ostebay na juhudi zinafanywa kuhakikisha wanaachiwa mara moja ili waendelee na shughuli zao.Aidha, Lowassa alisema wameshawasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuhusu tukio hilo, lakini katika hali ya kushangaza alisema hafahamu lolote kuhusu kukamatwa kwa vijana hao.
Meneja Kampeni wa Ukawa, John Mrema, alisema wamemwandikia barua IGP kutaka vijana wao waachiwe kwa sababu kazi waliyokuwa wakiifanya ni halali na hata Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaendesha kazi kama hiyo maeneo ya Mlimani City.
Mrema alisema polisi hao wakiwa na baadhi ya maafisa wa usalama wa taifa, walichukua kompyuta na vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na vijana hao, zikiwamo taarifa muhimu za mgombea wao, Lowassa.
“Lengo la kuweka vituo vya kujumlishia kura ni kupata taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini kutoka kwa mawakala wetu na kuyajumlisha… wenzetu CCM nao wanafanya zoezi kama letu na hawajakamatwa wala kubughudhiwa na vyombo vya ulinzi na usalama,” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa IGP.
Barua hiyo ilisema hatua hiyo ya vyombo vya ulinzi inaweza kuingiza dosari na uchaguzi huo kutokuwa wa huru na haki iwapo vijana woa hawataachiwa.
“Tunakunaomba IGP uwaachie vijana wetu na vifaa vyao haraka iwezekanavyo na bila masharti yoyote vinginevyo mtawajibika kwa madhara yatakayotokana na kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari.
Mrema alisema endapo Jeshi la Polisi litashindwa kuwaachia vijana hao, watatangaza baadaye kuhusu hatua nyingine watakazochukua.
Aliongeza kuwa bado wanaendelea na kazi ya kukusanya matokeo hayo, kazi inayofanywa na vijana wengine waliobaki na kwamba, kama ambavyo walitangaza awali, watalinganisha matokeo hayo na yale yanayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mrema alisema hivi sasa wanaendelea kupokea fomu za matokeo hayo kutoka katika vituo mbalimbali nchini.
Akielezea suala hilo wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni , Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Suleiman Kova, amesema zaidi ya watu 160 wamekamatwa kutoka sehemu mbalimbali jijini katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za kuingilia kazi ya Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).
Katika mahojiano aliyoyafanya na Kituo cha Televisheni cha ITV, Kamishna Kova alisema, Jeshi la polisi lilikamata watuhumiwa wakiwa na kompyuta katika maeneo ya Kinondoni na Kijitonyama, wakifanya kazi ya kujumlisha na kulinganisha idadi ya matokeo ya kura za uchaguzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
“Tunaendelea kuwahoji watuhumiwa hao kwa sababu kazi ya kujumlisha na kulinganisha matokeo ni ya NEC kwa mujibu wa sheria, na mtu yeyote anayefanya kazi hiyo nje ya NEC, anakuwa anatenda kosa la jinai,” alisema Kova.
Kamishna Kova alisema, mtu yeyote anayefanya kazi hiyo kama waliokuwa wakifanya watuhumiwa hao, anakuwa anatenda kosa la uvunjifu wa amani kwa sababu anaweza akatoa takwimu za kuwaaminisha wafuasi wa chama chake kuwa wameshinda kumbe sivyo.
“Tatizo linakuja pale NEC inapotoa takwimu rasmi za matokeo ya kura na zikawa kinyume na zile walizoaminishwa kabla, hapo ndipo uvunjifu wa amani unaweza ukaanza kutokea,” alisema
Alisema wanawahoji watuhumiwa wote kabla ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
UTANGAZAJI MATOKEO URAIS
Katika hatua nyingine, Lowassa ameitaka NEC kutangaza matokeo kwa haki na kuacha kumpendelea mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.
Alisema mwenendo wa utangazaji matokeo hayo hadi sasa unaonyesha kuwa NEC imeamua kwa makusudi kutangaza maeneo ambayo mgombea wa CCM amefanya vizuri na kuyaacha majimbo ambayo upinzani unaongoza.
Lowassa alisema kwa mwendo wa utangazaji matokeo, NEC inaonekana kuwa imeamua kuwaandaa kisaikolojia Watanzania kwamba mgombea wa CCM atashinda, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema wanatangaza matokeo kadri wanavyoyapokea kutoka katika maeneo mbalimbali nchini.
*Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Joseph Mwendapole, Raphael
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment