Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 27, 2015

Washauri matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani!

Mkuu wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu Tanzania kutoka Umoja wa Afrika (AU), ambaye pia ni Rais wa Zamani wa Msumbiji, Armando Emilio Guebuza .

By Peter Elias
Dar es Salaam. Waangalizi wa uchaguzi wa Kimataifa wameitaka Tanzania kuifanyia mabadiliko ibara ya 41(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuruhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani katika chaguzi zijazo.
Sambamba na mabadiliko ya katiba, waangalizi hao wameitaka Serikali kuangalia upya uteuzi wa watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ili kuifanya Tume hiyo kuwa huru katika utendaji wake.
Wakitoa ripoti zao za awali kuhusu upigaji kura uliofanyika Oktoba 25, Waangalizi kutoka Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Madola (Commonwealth) walisema uchaguzi ulifanyika kwa amani katika mazingira huru na wazi. 
Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Sadc (SEOM), Oldemiro Julio Baloi alisema licha ya kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza siku ya kupiga kura, bado changamoto hizo hazikuweza kuathiri mchakato mzima wa upigaji kura. Alisema watu walijitokeza kupiga kura na kuvumilia muda wote mpaka zoezi hilo lilipokamilika.
“Tumefuatilia uchaguzi kuanzia ufunguaji wa vituo mpaka wanapofunga. Tumebaini kwamba katika vituo mbalimbali tulivyoviangalia hali ilikuwa shwari na watu wameweza kupiga kura zao kwa amani na utulivu,” alisema.
Balozi ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kikamilifu ili kuboresha mazingira ya uchaguzi ujao. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kumaliza changamoto zilizojitokeza wakati wa uandikishaji kwa kutumia mfumo wa BVR.
Kiongozi huyo amesema waangalizi wa Sadc walikutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi na kupokea malalamiko yao tangu wakati wa uandikishaji. Hata hivyo, aliipongeza Tume ya uchaguzi kwa kufanikiwa kuendesha uchaguzi kwa wakati.
“Serikali pia ijitahidi kuongeza ushiriki wa wanawake katika chaguzi kuanzia ngazi ya vyama mpaka wagombea. Pia, makundi ya watu wanaosahalika ni muhimu katika uchaguzi, ni vizuri sauti zao zikasikika,” alisema Baloi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya nje wa Msumbiji.
Waangalizi hao wamependekeza vyama vya siasa kushiriki katika kutoa elimu kwa mpiga kura kipindi cha kampeni ili kusaidia wananchi ambao hawana uelewa juu ya masuala ya uchaguzi na jinsi ya kupiga kura.
SEOM imeridhishwa na uchaguzi mkuu wa Tanzania na kwamba unatosha kueleza matakwa ya Watanzania kupitia kura zao. Baloi alisisitiza kuwa kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza kama vile kutokea kwa vurugu na kuchelewa kufunguliwa kwa baadhi ya vituo, hazijaweza kuathiri sehemu kubwa ya upigaji kura.
Mkuu wa Waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU), Armando Guebuza alisema lengo la uangalizi wao ni kutathmini uchaguzi bila upendeleo kwa kuzingatia sharia na kanuni mbalimbali zinazoongoza uchaguzi hapa Tanzania.
Guebuza aliipongeza NEC kwa kuendesha uchaguzi kwa wakati bila kuathiri masharti yakisheria na kanuni mbalimbali za uchaguzi. Alisisitiza kuwa changamoto zilizojitokeza ni za kawaida zinaweza kutatulika katika uchaguzi ujao.
“Asilimia 95 ya vituo tulivyoviangalia vilikuwa wazi ndani ya wakati unaotakiwa kisheria na vilikuwa na vifaa vyote muhimu. Maandalizi ya NEC yalikuwa mazuri licha ya changamoto za manunuzi walizokumbana nazo,” alisema.
Guebuza ambaye alikuwa Rais wa Msumbiji alisema vyombo vya habari vimeonekana kuwa na upande wakati wa kampeni. Alisema baadhi ya vyombo hivyo sasa vimeanza kutangaza matokeo, jambo linaloweza kusababisha migogoro isiyo ya lazima.
Naye Kiongozi wa Waangalizi wa Jumuiya ya Madola, Goodluck Jonathan alisisitiza kuwa bado wanaendelea kuangalia uchaguzi kwa sababu bado hatua ya utoaji matokeo inaendelea. Alisema ripoti yao ya awali inaonyesha kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wazi.
“Kwa sasa tunasema uchaguzi huu ulikuwa na ushindani mkubwa na ulifanyika katika mazingira ya haki na uwazi. Kama kutatokea kasoro zozote katika hatua ya mwisho ya kutangaza matokeo basi tutaambatanisha mapungufu hayo katika ripoti yetu ya mwisho,” alisema.
Jonathan ambaye pia alikuwa Rais wa Nigeria alisema suala la kukaa umbali wa mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura halikuwa tatizo siku ya uchaguzi. Alisema polisi walikuwepo katika maeneo mengi katika kuangalia usalama.
Kiongozi huyo alibainisha kuwa mazingira ya siku ya uchaguzi yaliandaliwa vizuri na kufanya uchaguzi huo kuwa huru na wa haki. Alisisitiza kwamba matokeo ya uchaguzi yatawakilisha maamuzi ya wananchi wa Tanzania.

No comments :

Post a Comment