Mwenyekiti mwenza wa Cemot, Martina Kabisama
Dar es Salaam. Umoja wa waangalizi wa ndani wa uchaguzi (Cemot) umewataka wasimamizi wa uchaguzi kutoa matokeo haraka katika maeneo ambayo zoezi la kuhesabu kura limeshakamilika ili kuondoa hali ya mashaka na sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Mwenyekiti mwenza wa Cemot, Martina Kabisama aliwaambia wanahabari jana kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imejitahidi kwa kiasi kikubwa kufanya kazi zake kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu lakini maofisa wa uchaguzi wanaiangusha.
Alisema taarifa zilizowafikia kutoka kwa waangalizi 10,050 na vyanzo vingine zinabainisha kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa matokeo katika ngazi za ubunge ambao unaleta wasiwasi kwa wananchi.
Kabisama alibainisha uwepo wa taarifa za baadhi ya wagombea walioshindwa katika majimbo kukataa kusaini matokeo.
“Ni vyema maofisa uchaguzi wa maeneo husika wakatangaza matokeo haraka au kubainisha sababu za kuchelewesha matokeo hayo ili kuondoa wasiwasi miongoni mwa wananchi.
“Hatua hiyo itapunguza vurugu zisizo na lazima kwa kuwa wananchi wanaposubiri kwa muda mrefu, wanaanza kuhisi kuwa haki yao inataka kupokonywa,” alisema.
Hadi jana mchana, Kabisama alisema tayari majimbo 150 sawa na zaidi ya asilimia 50 ya majimbo yote.
Alieleza kuwa katika maeneo mengi watanzania wameendelea kuonesha utulivu wa hali ya juu ingawa kuna maeneo yenye vurugu na kwamba Cemot inaamini kuwa yale maeneo yenye vurugu ni vyema vyombo vya usalama hususan polisi vikaimarisha ulinzi unaozingatia haki za raia.
Wakati huo huo, jeshi la polisi limeonya vyama vya siasa na viongozi wao kuacha kuwakusanya vijana na kuwaandaa kufanya vurugu za kupinga matokeo na kuhatarisha utulivu na amani.
Kamishna wa Polisi, Operesheni na mafunzo, Paul Chagonja jana alisema kuwa wanazo taarifa za kuwepo makundi ya vijana yanayoandaliwa kufanya vurugu na hasa katika miji mikubwa na kwamba baadhi ya vijana hao wametolewa mikoani na hata nje ya nchi na kuletwa jijini Dar es Salaam.
Ili kukabiliana na hali hiyo, alisema jeshi la polisi linafuatilia kwa kina taarifa hizo na kuwataka wanaohusika na harakati hizo kuacha mara moja kutoharibu amani ya nchi yetu.
“Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama limejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa amani na usalama wa nchi hauvurugwi na mtu ama kikundi cha watu wachache wenye nia ovu,” alisema Chagonja katika mkutano wake na wanahabari.
Alisema hali ya nchi inaendelea kuwa salama katika maeneo mbalimbali isipokuwa maeneo machache ambayo baadhi ya vijana ambao ni wafuasi wa vyama vya siasa wamekuwa wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha kucheleweshwa matokeo.
Kuhusu malalamiko ya Chadema juu ya polisi kuvamia vituo vyao vya kukusanya matokeo kutoka kwa mawakala, Chagonja alisema waliwakamata vijana hao zaidi ya 100 kutokana na kuwepo taarifa za kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Alisema vijana hao walikutwa na vifaa mbalimbali vikiwemo kompyuta mpakato na simu na kwamba hadi sasa upelelezi unaendelea wataokutwa na ushahidi wa kutosha watapelekwa mahakamani na wengine wasiohusika wataachiwa huru.
Alipoulizwa kwanini polisi hawajakidhibiti kituo cha CCM cha kukusanyia matokeo, alijibu kuwa huenda kituo hicho kipo lakini hawajapokea taarifa zozote za kiuhalifu kama ilivyokuwa kwa Chadema.
“Kukusanya matokeo kutoka kwa mawala kwa ajili ya matumizi ya ndani siyo kosa ila tatizo ni pale baadhi ya matokeo yasiyo rasmi yanapoanza kuwekwa kwenye mitandao na kuleta mkanganyiko miongoni mwa wananchi.
“Jeshi la polisi halipo hapa kwa ajili ya kumpendelea mtu wala kuonea chama Fulani,” alisema Chagonja.
No comments :
Post a Comment