PITIA KWANZA HIZI HABARI ZA KABLA:
HTTP://ZANZIBARNIKWETU.BLOGSPOT.CA/2015/10/MHE-SEIF-SHARIFF-HAMAD-AZUA-MZOZO-KWA.HTML
0000000000000000000000000000000000000000000000000000000000000000000000
NA MWINYI SADALLAH
27th October 2015.
Mabomu hayo ya machozi yalikuwa yakirushwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutawanya watu hao kwa kushirikiana na askari Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU).
Wanachama na wafuasi hao wa Cuf walianza kukusanyika katika eneo hilo mara baada ya Maalim Seif kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari majira ya saa sita mchana na kujitangaza kuwa ameshinda urais.
Wafuasi hao walikuwa wakipiga ngoma na kuimba ‘Seif ndiyo Rais, Seif ndiyo Rais’ na kuingia katika mitaa ya Kiponda, Hurumzi na kuendelea hadi katika maeneo ya Darajani visiwani humo.
“Nimeshinda naomba Tume ya Uchaguzi watangaze matokeo bila ya kuchelewa kwa mujibu wa fomu tulizokusanya za matokeo ya urais katika vituo mbalimbali,” alisema Maalim Seif katika mkutano wake na waandishi wa habari uliochukua takriban dakika 15 kwenye makao makuu ya CUF Mtendeni, Zanzibar.
Alisema amejihakikishia ameshinda urais kutokana na matokeo waliyopata kutoka vituo mbalimbali ambayo alidai yamesainiwa na mawakala na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi Unguja na Pemba.
Alisema amejihakikishia ameshinda urais kutokana na matokeo waliyopata kutoka vituo mbalimbali ambayo alidai yamesainiwa na mawakala na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi Unguja na Pemba.
Maalim Seif akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Kampeni wa Cuf, Ismail Jussa Ladhu, alisema ameshinda kwa aslimia 52.87 dhidi ya mpinzani wake mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita. Alisema wakati mpinzani wake amepata kura 178,363, wakati yeye amepata kura 200,077 na kumzidi kwa tofauti ya kura 21,714 kati ya watu waliojitokeza kupiga kura katika vituo 1,583 Unguja na Pemba.
Hata hivyo, Maalim Seif hakusema kura zilizoharibika katika uchaguzi huo pamoja na matokeo ya wagombea wenzake 12 kupitia vyama vingine vya upinzani visiwani humo.
Aliwataka waangalizi wa kimataifa akiwamo Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia miiko na maadili ili kuhakikisha mshindi halali anatangzwa katika uchaguzi huo.
“Juhudi zozote za kufanya udanganyifu katika matokeo hazitafanikiwa na wala sitakuwa tayari kukubali na kutambua matokeo hayo,” alisema na kuongeza:
“Zec lazima waheshimu maamuzi ya wananchi kwa kunitangaza mshindi kama walivyofanya maamuzi ya kidemokrasia kupitia uchaguzi uliyofanyika Oktoba 25 mwaka huu.”
Maalim Seif alisema lengo la serikali yake ni kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikiwa na mfumo bora katika ngazi ya viongozi wakuu na watendaji wake.
Alisema ataunda serikali ndogo yenye ufanisi mkubwa ili kuijenga upya Zanzibar na kuwapatia huduma bora wananchi wake.
Matokeo hayo yasiyokuwa rasmi ndiyo yalianzisha shangwe na kusababisha watu kukusanyika katika mtaa wa Mtendeni na wengine Mji Mkongwe kabla ya kutawanywa na askari wa FFU na wa JKU.
ASKARI WAMWAGWA
Magari ya umma na yale yaliyotolewa msaada na mashirika ya maendeleo ya kimataifa baadhi yake yalionekana yakiwa yamebeba askari waliomwagwa mitaani kuwatuliza wafuasi hao wa Cuf.
Miongoni mwa magari hayo na namba zake za usajili ni DFP 7651, SLS 168 B pamoja na magari ya polisi PT 2617, STH 2921 na PT 1159 yakiwa yamepakia askari na mengine yakiwa na bendera nyekundu. Askari hao walikuwa wakitumia nguo walizokuwa wamevaa watu waliokuwa wakiwakamata kama pingu kwa kuwafunga watatu watatu na kuwapakiwa katika magari.
WANANCHI WAKIMBIA NYUMBA
Katika eneo la Mtaa wa Mlandege, baadhi ya familia zilionekana zikikimbia nyumba zao zikiwa na mizigo na watoto barabarani.
Njia kuu ya Darajani na Malindi zilifungwa na askari walionekana wakiwa wameimarisha ulinzi katika kila kona ya makutano ya barabara, huku maduka yakiwa yamefungwa pamoja na Soko Kuu la Darajani Zanzibar.
WAJERUHIWA KWA RISASI
Katika hatua nyingine, watu watatu walijeruhiwa kwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) nje kidogo ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis, alithibitisha tukio la watu hao kupigwa risasi na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Moja. Zanzibar.
Alisema askari wa upelelezi wameanza kuwahoji majeruhi hao kuhusu mazingira ya tukio hilo.
“Nimetuma askari wafanye uchunguzi wa kujua chanzo cha tukio hilo kwa sasa sina cha kusema hadi nitakapopokea ripoti ya uchunguzi huo,” alisema Kamanda Mkadam. Watu hao walipigwa risasi katika matukio mawili tofauti, akiwamo Abdulghan Mohamed (17) mkazi wa Jangombe, Juma Kombo Juma (39) Mkazi wa Migombani na Abas Khamis Khamis Issa (63) ambaye hajapata fahamu tangu juzi baada ya kujeruhiwa kichwani na wengine kulifanyiwa operesheni na wanaendelea vizuri.
CCM WAJA JUU
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema, Maalim Seif amevunja katiba na sheria kwa kujitangaza mshindi kabla ya matokeo halali ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec).
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya chama hicho Kisiwandui, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na sheria namba 11 ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutangaza matokeo zaidi ya Zec.
Alisema bila ya hekima na busara za wananchi, kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani na kuitaka Zec kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mgombea huyo wa urais wa Cuf.
“Tumesikitishwa sana na Zec kushindwa kuchukua hatua ikiwamo kukemea kitendo cha mgombea mmoja kujitangaza mshindi kati ya wagombea 14 wanaowania nafasi hiyo. Tunaomba Tume ya Uchaguzi ifanyekazi kwa mujibu wa katiba na sheria bila ya kumuogopa mtu yoyote,” alisema.
Katika mkutano huo, Vuai aliambatana na Spika wa Baraza la Wawakilishi aliyemaliza muda wake. Pandu Ameir Kifichio, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ na wajumbe wa timu ya kampeni ya mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. Aidha, alisema CCM imesikitishwa na tukio la kukamatwa karatasi bandia za kupigia kura katika Jimbo la Chonga, mkoa wa Kusini, Kisiwani Pemba.
Alisema kwamba karatasi hizo zinaonekana zimetegenezwa Afrika Kusini na wakala mmoja wa Cuf katika kituo cha kupiga kura anahusishwa na mpango huo pamoja na msimamizi mmoja wa kituo hicho na kutaka sheria ichukuliwe dhidi ya kitendo hicho.
CHANZO: NIPASHE
OOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOOO
No comments :
Post a Comment