NA EDITOR
27th October 2015.
Taarifa zilizotufikia ni kuwa kazi hiyo ilikwenda kwa amani na utulivu ingawa pia zilikuwapo ripoti za kuwapo matatizo katika sehemu mbalimbali nchini. Matatizo hayo ni pamoja na upungufu wa vifaa kwa baadhi ya vituo na kwingine kutopelekwa kabisa. Hatuna nia ya kumhukumu yeyote, lakini tunaamini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inapaswa kutoa maelezo ya kila kilichosabababisha kutokea kwa dosari katika sehemu mbalimbali nchini. Hali hiyo ilisababisha kurudiwa kwa uchaguzi katika baadhi ya maeneo jana.
Inasikitiska kuona kuwa watu walijitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura, lakini wakakuta hali tofauti kwa kuelezwa kuwa vifaa vilikuwa vimechelewa kufika.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa matatizo haya yalitokea hata katika Jiji la Dar es Salaam ambalo ndiyo makao makuu ya Nec. Ni jambo la kushangaza kwa Nec kushindwa kuwahisha vifaa katika Jiji la Dar es Salaam ambalo ni makao makuu yake. Pia jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa matatizo haya yanadaiwa kutokea katika maeneo ambayo yanaaminika kuwa na wafuasi wengi wa vyama vya upinzani.
Hata hivyo, siyo nia yetu kuihukumu Nec juu ya malalamiko hayo, lakini matukio ya namna hii ndiyo yanasababisha baadhi ya watu kudai haja ya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi. Nec ilitakiwa kufanya maandalizi ya kutosha ili kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu kuepusha matatizo ambayo husababisha malalamiko. Uchaguzi hutoa nafasi kwa watu kuamua na kuchagua wagombea wanaoawania nafasi mbalimbali za uongozi.
Na ndiyo maana Nec hutakiwa kuhakikisha kuwa kunakuwapo uchaguzi ulio huru na haki ili kuwasaidia wananchi kupata viongozi wanaowataka. Kama ilivyohisiwa kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni wa ushindani mkubwa baina ya vyama vinavyopambana.
Jambo hili lilidhihirika wazi kwa jinsi ambavyo wananchi walivyokuwa wanafurika kwenye mikutano mbalimbali ya kampeni. Ndiyo maana tunatoa wito kwa Nec na wasimamizi mbalimbali wa uchaguzi huu kuhakikisha kuwa wanatangaza matokeo mapema. Mathalani, Nec imetangaza kutoa matokeo ya uchaguzi wa rais keshokutwa, ni matumaini yetu kuwa ahadi hiyo itatekekezwa. Ucheleweshaji wa utangazaji wa matokeo umekuwa kati ya mambo kwa kiasi kikubwa yanayosababisha vurugu katika kipindi cha uchaguzi.
Nec na wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa kuwa makini katika suala hilo kwani kuna mifano mingi ya ucheleweshaji wa kutangaza matokeo, ambayo hatima yake husababisha vurugu. Pia tukumbuke kuwa tatizo siyo la kuchelewesha matokeo, bali pia wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa kuhakikisha wanatangaza matokeo halisi ya wapigakura.
Mwaka jana kulikuwa na vurugu kubwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji wakati wa kutangaza matokeo.
Hata hivyo, watu wengi wana kumbukumbu jinsi nchi kama Kenya na Ivory Coast zilivyoingia katika vurugu kubwa kutokana na ucheleweshaji wa utangazaji matokeo, ambayo yalikuwa kinyume cha matakwa ya wapigakura.
Ni kwa msingi huo ndiyo maana tunaishauri Nec ihakikishe kuwa suala la kutangaza matokeo linafanyika mapema na kwa uadilifu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment