By James Magai, Mwananchi
Dar es Salaam. Hospitali ya Rufaa ya Amana iliyopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ina idadi kubwa ya asilimia 70 ya wagonjwa wanaotibiwa kwa msamaha na kulazimika kutumia zaidi ya Sh8 milioni kwa siku.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Meshack Shimwela aliyasema hayo jana wakati akipokea msaada wa vifaatiba vilivyotolewa na Benki ya Diamond (DTB) kwa ajili ya hospitali yake.
Dk Shimwela alisema asilimia 30 ya wagonjwa ndiyo wanaochangia huduma za matibabu hospitalini hapo.
Alisema pia hospitali hiyo inalazimika kulipia Sh25 milioni kwa huduma ya umeme kwa mwezi.
Dk Shimwela alisema hali hiyo imesababisha hospitali kuwa na upungufu wa Sh5 bilioni kila mwaka.
“Kwa siku tunapokea na kuhudumia wagonjwa kati ya 1,000 na 1,500. Tuna vitanda 350 vya kulaza wagonjwa, lakini vitanda 250 ni vya bure na 100 tu ndivyo wagonjwa huchangia fedha kidogo za uendeshaji,” alisema na kuongeza:
“Tunazalisha wajawazito 80 hadi 100 kila siku bure na gharama ya kumzalisha mmoja ni Sh40,000 na tunafanya upasuaji kwa kina mama 15 hadi 20 kwa siku bure.”
Alisema hospitali ina mahitaji na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa mashine za uchunguzi wa magonjwa hususani CT Scan na MRI.
Pia alisema kuna wa mashine za Ultra Sound ambazo zipo tatu kati ya saba zinazohitajika.
Mkuu wa Idara ya Masoko wa benki hiyo, Sylvester Bahati alisema vifaa hivyo vina thamani ya Sh10 milioni.
Alisema benki hiyo imekuwa ikitoa msaada kama huo mara kwa mara katika hospitali hiyo na nyingine nchini kutokana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya.

No comments :
Post a Comment