Oparesheni ya kubomoa majengo yaliyokuwa yamejengwa kwenye maeneo ya wazi, barabara, na kwa wale waliojenga kwa nguvu maeneo a watu wengine imeendelea leo jijini Dar es salaam na kuwaacha watu wengi wakiwa kwenye simanzi.
Takriban nyumba 300 zimekwisha bomolewa katika bonde la Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni tangu kuanza kwa operesheni hiyo ianze wiki iliyopita na kuathiri zaidi ya familia 2,000 kutokana na nyumba zao kubomolewa.
Aidha, kwa siku ya jana kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi kufikia saa 6:00 mchana, tayari nyumba nyingine 18 zilikuwa zimebomolewa.
Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Charles Mkalawa, aliiambia Nipashe jana kuwa kazi ya kukamilisha ubomoaji katika bonde hilo ilitarajiwa kukamilika jana jioni.
“Leo tunamalizia kabisa hapa bonde la Mkwajuni. Nyumba zote zilizo katika maeneo yaliyo kando ya njia za maji tutazibomoa, hivyo ni vyema wananchi wakahama wenyewe,” alisisitiza Mkalawa.
Pia alisema baada ya kumaliza eneo hilo, wataelekea eneo la Selander Bridge ambako watabomoa nyumba zilizoko eneo la Mto Msimbazi kabla ya kwenda kwenye mitaa ya Florida na Suni.
“Leo kazi inakwenda taratibu kwa sababu mashine moja imeharibika na mafundi wanaendelea na kazi ya kurekebisha ili kazi iende haraka, kwa hiyo mashine inayotumika ni moja tu,” alifafanua.
“Leo kazi inakwenda taratibu kwa sababu mashine moja imeharibika na mafundi wanaendelea na kazi ya kurekebisha ili kazi iende haraka, kwa hiyo mashine inayotumika ni moja tu,” alifafanua.
Hata hivyo, waathirika wa eneo hilo, wameiomba serikali kuwapa maeneo ya kuishi badala ya kuwatelekeza.
“Siyo kwamba tunafurahia kuishi maeneo haya, bali hatuna sehemu za kwenda. Serikali itufikirie hata sehemu za kuishi na watoto wetu kwa muda,” alisema mmoja wa waathirika, Amisa Rashid.
Goleda Kashimbe, mkazi wa eneo alidai kuwa serikali imewaonea kwa vile wao ni wanyonge.
“Kwa nini hawakuwaandalia makazi ya kuishi kwanza? Leo tunashuhudia watoto na akina mama wakitapatapa mitaani, tena wakiwa wamepoteza kila kitu,” alisema Kashimbe.
Kazi hiyo ya ubomoaji ilianza katika bonde la Mkwajuni Manispaa Kinondoni na inasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Nemc, Mhandisi Bonaventure Baya, nyumba zote za mabondeni zitabomolewa.
Aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuondoka mara moja ili kupisha kazi hiyo ambayo ni endelevu.
Jana, Nipashe lilishuhudia baadhi ya wakazi wa eneo hilo wakihaha kuokota vitu vyao vilivyokuwa vimesalia kwenye nyumba zilizobomolewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment