
Alitoa agizo hilo wakati akizindua baraza la madiwani wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki.
Gallawa alisema Rais John Magufuli anabana matumizi na kupunguza vitu visivyo na ulazima ili kukuza uchumi na maendeleo ya taifa hivyo jamii nzima ikiwamo madiwani wanatakiwa kumuunga mkono.
“Mlipanga kuwe na vikao viwili vya baraza ambavyo vingegharimu mamilioni ya fedha, lakini mimi nasema hivi, kikao kifanyike kimoja tu na fedha mliyokuwa mkitaka kulipana posho kwa vikao viwili sasa mtalipana kikao kimoja na fedha nyingine ziende kusaidia shule za msingi,” alisema.
Gallawa alisema jukumu la baraza hilo ni kuongeza pato la mwananchi ili iwe rahisi kuongeza mapato ya ndani ya manispaa pamoja na serikali kwa ujumla.
Alisema kumekuwa na matumizi mabaya ya mapato kwa baadhi ya watendaji kufuja fedha za wananchi kwa maslahi yao binafsi, hali inayopelekea manispaa hiyo kukosa maendeleo.“Nitang’ang’ana na halmashauri ya manispaa hii na wote waliohusika kwenye wizi wa mapato yanayotokana na ukusanyaji wa kodi za wananchi watawajibishwa,” alisema.
Agizo hilo la mkuu wa mkoa linafanana na maagizo kadhaa yaliyotolewa na Rais Magufuli ya kubana matumizi katika mambo yasiyo na umuhimu mkubwa na kuagiza fedha zilizookolewa kwenda kusaidia shughuli za kijamii.
Naye Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffari Mwanyemba, alitaka kuwekwa mfumo wa usimamizi wa mapato kuanzia ngazi ya kata, ili fedha zinazopatikana ziweze kuboresha huduma za jamaii hasa afya na elimu ambazo ni changamoto kubwa kwa manispaa hiyo.
“Tushirikiane bila kujali itikadi za vyama ili manispaa yetu ifikie hadhi ya jiji haraka, naamini hili linawezekana, tuhakikishe tunaenda sawa na kasi ya Rais wetu na kauli mbiu yake ya “Hapa kazi tu,” aliongeza kusema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment