
Katika tukio lisilo la kawaida, Naibu aziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, jana aliwafungia nje ya geti watumishi wa wizara hiyo ambao walichelewa kazini na kuahidi kitendo hicho kitakuwa endelevu.
Dk. Kigwangallah ambaye ilielezwa kwamba aliwasili wizarani hapo saa 1:05 asubuhi, alianza kukagua daftari ambalo wafanyakazi wa wizara hujiandikisha wanapofika kazini na ndipo alipobaini kwamba wengi hawajafika.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya zoezi hilo, Dk. Kigwangalla alisema ameamua kufanya hivyo ili kuona kama watumishi wa wizara hiyo wanaweza kufanyakazi kwa kasi ambayo Rais Magufuli anaitaka.
“Hili zoezi litakuwa endelevu, tangu niingie hapa nimeona kuna mambo hayajakaa sawa sasa lazima niwasimamie ili nijue nani wanafanyakazi kwa mazoea na nani wanafanyakazi kwa kuzingatia maslahi ya taifa,” alisema.Awali ilielezwa kuwa Naibu Waziri huyo alipowasili wizarani hapo mapema akitembea kwa miguu, alikwenda moja kwa moja kusimama kwenye geti kuu la kuingilia kama mtu wa kawaida huku akiangalia saa yake ya mkononi mara kwa mara, mmoja wa mashuhuda alieleza.
Ilipofika saa 1:32, Kingwangala alimwagiza askari aliyekuwa akilinda geti hilo kufunga kufuli na asiruhusu mtumishi yeyote kuingia. Magari kadhaa ya Wizara hiyo yalionekana yakitaka kuingia ndani lakini mlinzi huyo aliwakatalia madereva hao akiwaeleza kuwa ameambiwa na waziri asiruhusu mtu yeyote kuingia.
Mmoja wa watumishi walioonja joto la kadhia hiyo ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara hiyo, Michael John, ambaye alitakiwa kueleza ni kwanini watumishi wa wizara hiyo hawasaini vitabu getini.
Naibu Waziri alimwagiza Mkurugenzi huyo kupeleka ofisini kwake mara moja vitabu vya mahudhurio vya vitengo vyote ili vifanyiwe ukaguzi kuwabaini watumishi wenye kawaida ya kuchelewa kazini, habari zaidi zilieleza.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment