
Meno ya tembo.
Dar es Salaam. Polisi jijini Dar es Salaam imekamata vipande 156 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 211.66 vikiwa vimetandazwa kwenye nyumba moja wilayani Temeke. Kamishna wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwaambia wanahabari jana kuwa nyara hizo za Serikali zenye thamani ya Sh1 bilioni zilikamatwa juzi Mtaa wa Miburani wilayani humo.
Alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuwa kwenye nyumba ya mkazi mmoja anayeishi mtaa huo kumehifadhiwa meno hayo yaliyofunikwa kwenye chumba kimoja.
“Katika upekuzi wetu pia tumefanikiwa kukamata bunduki mbili aina ya Rifle inayotumika kuwindia wanyama,” alisema Kova.
Alisema wanawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumiliki nyara hizo, huku wakiendelea kuwasaka wengine ili kubaini mtandao huo wa majangili.
“Kutokana na uzito wa shauri hili, polisi inashirikiana na maofisa wa idara ya wanyamapori ili kutusaidia kwenye upelelezi dhidi ya suala hili,” alisema.
“Upelelezi ukikamilika watuhumiwa hawa na wengine tunaowasaka, watafikishwa mahakamani. ”
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Andrew Satta aliwataka wananchi kutoa taarifa za kuzuia uhalifu wa aina yoyote ukiwamo wa nyara za Serikali kwenye maeneo yao.
Wakati huohuo, Kamishna Kova alisema polisi imejipanga ipasavyo ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa saa 24 katika kipindi hiki cha kuelekea katika sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismas na Mwaka Mpya wa 2016.
No comments :
Post a Comment