Kandoro aagiza wafanyakazi wa Forodha watiwe mbaroni

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro.
Tunduma. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ameiagiza polisi kuwakamata wafanyakazi wote Idara ya Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka Tanzania na Zambia wa Tunduma ili waisaidie polisi katika uchunguzi wa magogo 1,301 yaliyokamatwa kwa kukwepa kulipa kodi.
Inadaiwa kuwa magogo hayo yalikamatwa yakiwa yamefichwa kwenye nyumba kwa ajili ya kuvushwa kwenda nchini Zambia bila ya kulipiwa kodi.
Kandoro, pia alishuhudia nguzo za umeme 50 mali ya msitu wa Taifa wa Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa (Sao Hill) zikiwa katika harakati za kwenda nchini humo zimefichwa kwenye nyumba iliyopo mpakani hapo.
“Watu wa forodha walijua kuwa magogo haya hayajalipiwa kodi, wao ndiyo waliofungua lakili ya kutoka nje na kufunga ya kwao baada ya kukaguliwa na kuruhusu kupita bila kulipa ushuru hivyo nasema hivi watumishi wote wa waforodha wakamatwe waisaidia polisi mara moja,” alisema.
Awali akitoa taarifa, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Nyigesa Wankyo alisema walikamata magogo hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema na kwamba polisi ilifanya operesheni maalumu juzi na kuyakutayamefichwa kwenye baadhi ya nyumba mjini Tunduma.
Alisema katika operesheni hiyo walilikuta lori likiwa na magogo baada ya kutoa lakili iliyofungwa na maofisa wa forodha mpakani hapo huku kukiwa hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha malipo ya mapato ya mzigo huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema watu saba wamekamtwa akiwamo mmoja wa wamiliki wa nyumba hizo kwa tuhuma hizo.
Msangi alisema wamepokea agizo la mkuu wa mkoa na kwamba utaratibu unafanyika kuhakikisha watumishi hao wa idara hiyo wanakamatwa ili kuisaidia polisi kuhusiana na tukio hilo.
Ofisa Misitu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Ajanson Mloge alisema magogo yaliyokamatwa ni ya mti aina ya mninga bila ya kuwa na nyaraka zozote zinazoenyesha kulipiwa kodi.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Tanzania na Zambia ni marufuku kusafirisha magogo ambayo hayajachakatwa.
No comments :
Post a Comment