
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umesema wanawake waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, walipachikwa majina yaliyolenga unyanyasaji wa kijinsia ili kuwakatisha tamaa.
Kadhalia, TGNP imeweka wazi kuwa, baadhi ya wanawake walishindwa kupiga kura kutokana na vitambulisho vyao kufichwa na wenza wao siku moja kabla ya Oktoba 25 hivyo kusababisha wakose haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.
Madai hayo yalitolewa katika warsha iliyoandaliwa na TGNP na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwamo wanawake wanaounda Mtandao wa Vyama vya Siasa (Uringo), na kufanyika jijini Dar es Salaam.
Hapakutolewa uthibitisho wowote wa madi hayo, hata hivyo.Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Katibu mkuu wa Chama cha ADC, Lydia Bendera alisema licha ya changamoto hiyo, wanawake wengi walimudu kukabiliana nazo na kushinda.
Alisema katika kipindi cha kampeni baadhi ya wagombea wanawake walikatishwa tamaa wakiwa majukwaa ya siasa kwa kuitwa majina ya kibaguzi kama “embe bichi”.
Changamoto nyingine, walizokumbana nazo wanawake kwenye uchaguzi ni kuombwa rushwa ya ngono, alisema Bendera.
Aidha, Bendera alidai wanaume wengi hawakuwa tayari kuwasaidia wanawake kwa lengo la kuwainua bali kwa malipo ya ngono jambo ambalo lilikuwa ni tatizo kufikia malengo ya kuwa wanawake viongozi.
Pamoja na changamoto hizo, TGNP ilijadili nini kifanyike ili ukatili huo usitokee tena katika chaguzi zijazo kwa kuwapa wanawake ujasiri.
TGNP ilisema ni muhimu kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanzisha kitengo maalum cha mwanamke ili pakitokea unyanyasaji kijinsia wajue pa kupeleka malalamiko yao.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment