Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, January 6, 2016

ZANZIBAR: Damu ikishamwaika nani atainywa?

Image result for elections zanzibar
UAMUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kushikilia kuwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar lazima urejelewe ni wa kushangaza na kushtusha.

Uamuzi huo ni wa kushangaza kwa sababu unaonyesha jinsi chama hicho kinavyoweka mbele maslahi yake badala ya kuweka mbele maslahi ya taifa. Tayari ukaidi wa wababe wa CCM-Zanzibar wa kukataa kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais wa Zanzibar umeikosesha Tanzania msaada wa zaidi ya shilingi trilioni moja ($472.8m) kutoka Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani.


Fedha hizo zinatakiwa zitumike katika usambazaji wa umeme ili wananchi waweze kunufaika na maisha yao yawe mepesi. Inavyoonyesha ni kwamba viongozi wa CCM hawajaujali usumbufu wa wananchi ilimradi chama chao kiendelee kuhodhi madaraka Zanzibar hata kama ni kwa kutumia kila aina ya ghilba.

Moja ya ghilba hizo ni kuutia dosari Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanywa Oktoba 25 mwaka jana. CCM inashikilia kwamba uchaguzi huo urudiwe kwa kisingizo kwamba kwa sababu ya dosari hizo ule wa mwaka jana ulifutwa na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Inashangaza pia kukiona chama cha CCM kikishikilia uzi wake huohuo licha ya shinikizo za Jumuiya ya Kimataifa yenye kuhimiza kwamba mchakato wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wa wawakilishi na madiwani ukamilishwe kwa kutangazwa matokeo yaliyosalia.


Huo ndio msimamo wa serikali ya Marekani, wa Muungano wa Ulaya (EU) na wa jumuiya na taasisi kadhaa za kimataifa na za Tanzania.


Waziri mpya wa mambo ya nje Dk. Augustine Mahiga aliwashangaza na kuwasikitisha wengi kwa maneno aliyoyasema alipokutana kwa mara ya mwanzo na mabalozi wa kigeni wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania. Mahiga alinukuliwa akisema kwamba “mgogoro wa Zanzibar usiwe kigezo cha baadhi ya nchi kudharau hatua kubwa za kidemokrasia zilizofikiwa.”


Labda nimfahamishe ndugu yangu Mahiga kwamba huo anaouita “mgogoro wa Zanzibar” usipopatiwa ufumbuzi wa haki utakaoheshimu misingi ya kidemokrasi utaendelea kutufanya tudharauliwe. Kwa taarifa yake sio nchi tajiri tu zenye kutudharau bali hata zilizo masikini.


Binafsi nimeshawasikia wananchi kutoka nchi kadhaa za Kiafrika wakitucheka kwa sababu ya yaliyojiri Zanzibar baada ya Oktoba 25 mwaka jana. Kwa kutucheka wanatudharau na wanatudharau kwa sababu sisi wenyewe tunajidharaulisha kwa kuwaachia viongozi wetu wajifanye mazuzu kwa kuibomoa misingi ya kidemokrasia huku wakijidai kwamba wanaijenga demokrasia.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na mabalozi wa kigeni Mahiga alisema: “Wengine wanajua kabisa taratibu za kuheshimiana lakini wanaamua kwa makusudi kutumia uwezo wa kutudharau isivyopaswa. Lakini wanatakiwa kuheshimu uhuru wetu kama tunavyoheshimu wao. Uhuru wetu haujadiliki.”


Alikusudia nini aliposema: “Uhuru wetu haujadiliki?” Tuseme alikuwa na maana kwamba viongozi wa CCM-Zanzibar wanaong’ang’ania madaraka wasiingiliwe uhuru wao wa kufanya watakavyo?
Bahati mbaya Zanzibar ina viongozi ambao ama wamebobea kusema uongo au wasiojuwa wakisemacho. Mfano mzuri ni Balozi Seif Ali Iddi. 


Wiki iliyopita alizungumza na waandishi wa habari kuhusu matayarisho ya maadhimisho ya kufikia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika mkutano huo ambapo alisisitiza kwa mara nyingine kuwa uchaguzi wa Zanzibar utarudiwa Balozi Iddi aliyagusia mazumgumzo yanayofanywa Ikulu, Unguja. Alinukuliwa akisema kuwa hajui nini kinaendelea hadi sasa.


Lakini itakuwaje hajui kinachoendelea ilhali yeye ni mmoja wa washiriki wakuu katika mazungumzo hayo? Kwa nini asiseme tu kwamba hawezi kulizungumzia kwa sasa suala hilo kwa sababu ni nyeti au kwa sababu bado wakati wake haujafika? Kwa nini aliona lazima aseme uongo, adanganye na kujifanya hajui kinachoendelea katika mazungumzo ambayo yeye anashiriki?


Mahiga, aliyeanza kuitumikia Tanzania kwa kufanya kazi katika Usalama wa Taifa, anafaa atambue kwamba ni viroja kama hivi vinavyotufanya tudharauliwe. Viongozi wetu wameshazoea kudanganya, kunyang’anya na kuyaparaganya mambo. Wanawanyang’anya wananchi haki yao ya kumchagua wamtakaye, wanaudanganya ulimwengu kwamba kwa kufanya hivyo wanatenda haki na wanaiparaganya misingi ya utawala bora kwa kutumia mabavu.


Matokeo yake ni kuidhuru jamii kama, kwa mfano, kwa kukamatwa na kuteswa mashekhe kwa sababu viongozi wanawaogopa kwa kweli waisemayo. Misingi ya utawala bora inakiukwa na ubabe unatumika.


Hivi sasa Zanzibar imo mikononi mwa wababe, ‘ma-cow boy’ wetu, wenye kuamini kwamba wanaweza kufanya watakavyo na lisiwe lolote. Wanaamini hivyo kwa sababu wanajiona kuwa wao ndio wenye silaha, wao ndio wenye kuvidhibiti vikosi vya usalama. Kwa ufupi, wao ndio wenye kuushika mpini.


Ujeuri na kibri kinawazidi kwa sababu wanajuwa, tena kwa uhakika, kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawalinda na itaendelea kuwalinda kwa chochote watachoamua kukifanya.
Hivyo ndivyo ilivyo hadi sasa. Labda wasichokijuwa ni kwamba wanacheza na moto. Ndiyo maana uamuzi wa kuufanya upya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unatisha.


Balozi Seif Ali Iddi ananukuliwa akisema kwamba ijapokuwa mazungumzo ya Ikulu yanaendelea, serikali imeamua kuwa uchaguzi urejelewe. Tamko lake haliwezi kuwa sahihi kwa sababu serikali anayoizungumzia si Serikali ya Umoja wa Kitaifa, si serikali halali. Labda ni “serikali nusu”.


Chama kikuu cha upinzani Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF), kilichokuwa na ubia katika serikali iliyopita, kinaipinga vikali hatua hiyo ya kurejelewa uchaguzi. Kikiamini kwamba katibu mkuu wake Maalim Seif Sharif Hamad ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais kinaitaka Tume ya ZEC imtangaze kuwa ni mshindi. Hamad pamoja na viongozi wenzake wa CUF wamewasihi wafuasi wao wawe watulivu na wawe na subira.


Mpaka sasa viongozi wa CUF wamesikilizwa na wafuasi wao licha ya wafuasi hao kushambuliwakatika nyakati tofauti baada ya uchaguzi wa Oktoba na makundi ya watu wanaojivisha barkoa nyusoni mwao. Mitaani washambulizi hao wanaitwa “mazombi” na mashambulizi yao ni yenye kukiuka haki za binadamu.


“Mazombi” hao pia, katika nyakati tofauti baada ya uchaguzi uliopita, walizihujumu steshini mbili za redio mjini Unguja na waliwapiga watumishi wa steshini hizo.


Mashambulizi kama hayo yaliwahi kufanywa wakati wa enzi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na sasa tunayashuhudiwa katika enzi ya Rais John Magufuli. Wakati wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa majeshi yaliwaua Wazanzibari waliokuwa wakitetea haki yao baada ya uchaguzi. Kwa hivyo, mashambulizi yote hayo ni aibu yao wote watatu.


Mashambulizi ya makundi kama ya “mazombi”, “janjaweed” au “ubayaubaya” yana lengo mahsusi. Nalo ni kuwatia hofu wananchi, hasa wapinzani, wasiendelee kuwa na msimamo wa kutetea haki zao. Hii ni moja ya mbinu zinazotumiwa katika mikakati ya kuwagandamiza wananchi wasiweze kusimama na kutetea haki zao. Ni mbinu ya kutumia hofu na vitisho kuwa kama silaha dhidi ya wananchi.


Inashangaza kwa pahala padogo kama Unguja mjini kwamba hadi leo hakuna hata mmojawao hao “mazombi” aliyetiwa mbaroni seuze kushitakiwa. Na wale waliowatuma wafanye unyama walioufanya nao pia mpaka sasa hawajatiwa mbaroni ingawa baadhi ya majina yao tunasikia yakitajwatajwa pamoja na wapi zilipo kambi wanakopatiwa mafunzo hao “mazombi”. Ni dhahir kuwa huu ni ugaidi unaofanywa na baadhi ya viongozi wenye madaraka kwa lengo la kung’ang’ania madaraka yasiwaponyoke.


Hawa ndio mzizi wa fitina yote hii na ikiwa mzizi huo hautofyekwa basi tusitaraji kwamba vitendo hivi vya mashambulizi havitochomoza tena. Tabia kama hii ya kupalilia chuki za kisiasa, chuki zisizoingia akilini na zisizoeleweka, haina mwisho mwema, hasa pale silaha nzito na za kijadi zinapotumiwa dhidi ya mahasimu wa kisiasa.


Si taabu kuutabiri mustakbali wa hayo. Burundi tunapakana nayo na tunashuhudia michirizi ya damu inayomwaika huko, maiti zinazozagaa mitaani na mkururo wa wakimbizi wanaovuka mpaka na kuingia Tanzania.


Ingefaa wababe wetu wa Zanzibar wasite kidogo, watafakari, kwa kina, kisha wajiulize: damu ikishamwaika nani atainywa?
 

- See more at: http://raiamwema.co.tz/z%E2%80%99bar-damu-ikishamwaika-nani-atainywa#sthash.FBZEp46X.dpuf

No comments :

Post a Comment