Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, January 6, 2016

Uchaguzi Zanzibar Februari!

[​IMG]


  • Ni wa marudio baada ya majadilano ya kina
UCHAGUZI Mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kurudiwa wakati wowote kuanzia mwishoni mwa Februari au mwanzoni mwa Machi mwaka huu, Raia Mwema limeambiwa.

Hii ni taarifa rasmi ya kwanza kupatikana tangu kuanza kwa mazungumzo baina ya viongozi wa vyama vya CUF na CCM, yaliyotokana na kufutwa kwa uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Mmoja wa wahusika wa mazungumzo hayo ameliambia gazeti hili kwamba ni wazi uchaguzi huo utarudiwa na tarehe zinaweza kuwa ni mwishoni mwa Februari au mwanzoni mwa mwezi Machi.

“Jambo la hakika ambalo naweza kukwambia ni kwamba Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utarudiwa kama ambavyo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilisema. Tume imetangaza uchaguzi ulikuwa batili na hamna namna ambayo inaweza kuyatangaza upya matokeo hayo kuwa ni halali.

“Huu uchaguzi unarudiwa. Tunaweza kujadiliana kuhusu ni tume ipi itasimamia huo uchaguzi na utafanyika kwa namna gani lakini kurudiwa utarudiwa. Hilo ni jambo pekee la uhakika ambalo naweza kukwambia” kilisema chanzo hicho cha habari cha Raia Mwema.

Gazeti hili halitaweza kutaja chanzo chake cha habari hii kwa kuwa kinashiriki kwenye mazungumzo yanayoendelea sasa.

Kwa sasa, kuna mazungumzo yanaendelea kati ya waliokuwa wagombea urais wa uchaguzi huo; Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM na Seif Shariff Hamad wa CUF ambayo yanawahusisha pia marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.

Hakuna taarifa kamili iliyowahi kutolewa kuhusu nini hasa kinazungumzwa kwenye mazungumzo hayo; ingawa vyama vyote viwili vimekuwa vikitoa kauli binafsi kuhusu msimamo wao kwenye mazungumzo hayo.

Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Chama Cha Mapinduzi wamekuwa wakiwasisitizia wanachama wao kuwa wajiandae na kushiriki kwenye uchaguzi huo wakati tarehe ya kuurejea itakapotangazwa.

Wakati huohuo, viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) nao wamekuwa wakiwaambia wapenzi na wanachama wao kuwa wanasubiri mshindi katika uchaguzi huo atangazwe.

Kufutwa kwa Uchaguzi

Oktoba 28 mwaka huu, siku tatu baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo akitoa sababu nane.

Sababu hizo ni kasoro kisiwani Pemba ambako kura zilizopigwa zilizidi idadi ya wapiga kura, kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha wa masanduku ya kupigiwa kura, kuharibiwa kwa kura na pia tishio la vijana waliokuwa wakitishia kufanya fujo.

Pia Jecha alisema kulikuwa na matukio yasiyo ya kawaida kwenye uchaguzi huo ikiwemo makamishna wa uchaguzi katika tume hiyo kupigana kutokana na tofauti zao, wakawa na upendeleo kwa vyama walivyotoka na kwamba kuna maeneo mawakala wa vyama walifukuzwa na wapinzani wao na hivyo hakukuwa na uhakiki wakati wa kuhesabu kura.


Hatua hiyo ya ZEC ilipingwa na wadau mbalimbali kikiwamo Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kilichosema kwamba Jecha hakuwa na mamlaka ya kufuta uchaguzi.

Katika tamko lililotolewa mara baada ya kauli hiyo ya Jecha, ZLS ilisema; “Chama cha Wanasheria kimepitia kwa umakini Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama mwenyekiti anao uwezo wa kufuta matokeo ya uchaguzi kama alivyoeleza kwenye tamko lake na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufutwa kwa uchaguzi nchi nzima.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, Tume ni Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya tume lazima yaungwe mkono na wajumbe waliowengi lakini wajumbe wawili walitoka hadharani mbele ya waandishi na kusema hawajashirikishwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya ZLS.

Hali ilivyo Zanzibar

Raia Mwema lilikuwa visiwani Zanzibar wiki mbili zilizopita na kuna hali ya sintofahamu miongoni mwa wananchi wa visiwa hivyo hivi sasa.

Mfumuko wa bei umeongezeka na mapato kupitia sekta ya utalii yameshuka kwa vile watalii wengi wameahirisha safari zao wakisubiri kwamba mgogoro huu wa kisiasa umalizike.
Wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema kwamba ingawa kuna utulivu, lakini wangependa suala hilo limalizike kwa namna yoyote; iwe kwa kutangazwa matokeo kama wanavyotaka CUF au kurudiwa uchaguzi kama inavyotaka CCM ili hatimaye maisha yarejee katika hali ya kawaida.

Kuna mgogoro wa kikatiba pia kwamba Rais wa Zanzibar anatakiwa kukaa madarakani kwa muda wa miaka mitano na Ali Mohamed Shein alitakiwa kumaliza muda wake Novemba 3 mwaka jana, ingawa Katiba haiweki fursa ya ombwe la uongozi na inataka Rais aliyepo madarakani aendelee hadi pale atakapopatikana Rais mpya.

CCM na CUF wanasemaje

CCM kupitia kwa Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Ali Iddi, alisema mwishoni mwa wiki kuwa chama chake kinajipanga kwa marudio ya uchaguzi huo na kwamba wanaosema vinginevyo wanapotosha wananchi.

“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndiyo iliyopanga huo uchaguzi na baada ya kuona upungufu mkubwa uliojitokeza, yenyewe ndiyo ikaamua kuufuta na kwa mujibu wa sheria zetu, ZEC ndiyo itapanga uchaguzi huo urudiwe lini.

“Wanaosema vinginevyo wanawapotosha tu wananchi. Sisi tunajipanga kwa marudio ya huu uchaguzi kwa sababu aliyeupanga ndiye aliyesema haukufanyika unavyotakiwa kufanyika. Tunaomba ZEC itangaze tarehe ya uchaguzi mapema ili nasi tuanze maandalizi,” alisema Balozi Iddi.

Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema hivi karibuni kwamba uamuzi wa kurudiwa uchaguzi haujafikiwa na kwamba mazungumzo yanayoendelea ndiyo yatakayomaliza mkwamo huo wa kisiasa Zanzibar.

Alisema CCM inapowaambia wanachama wake wajitayarishe na uchaguzi haisemi ukweli juu ya kinachoendelea na kwamba chama tawala kimekuwa kikitoa kauli zinazokinzana kuhusu suala hilo.

Jussa aliwataka wanachama wa CUF kumpa nafasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuendelea na juhudi za ngazi ya juu za kuhimiza upatikanaji wa ufumbuzi wa haraka juu ya mkwamo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

“CUF haitatetereka, na itasimamia kwa dhati maamuzi yao waliyoyafanya Wazanzibari kwa njia ya kidemokrasia kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani wao,” alisema Ismail Jussa.

Alisema wakati macho na masikio ya wananchi yametega Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Wazanzibari wanastahili kupongezwa kwa kuonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa kwa kuendelea kutunza amani na utulivu wakati viongozi wa kitaifa wakiendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kutanzua mkwamo huo. 


- See more at: http://raiamwema.co.tz/uchaguzi-z%E2%80%99bar-februari#sthash.7XPmv0ml.dpuf

No comments :

Post a Comment