Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Arusha. Zaidi ya wakazi 3,000 wa Kata ya Kiranyi Wilaya ya Arumeru mkoani hapa, wameamriwa na Mamlaka ya Bonde la Pangani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo wa Ngaramtoni kubomoa nyumba zao kwa kujenga kwenye chanzo cha maji.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Ngaramtoni (Ngauwsa), Clayson Kimaro alisema nyumba ambazo zimewekwa alama ya X zinazotakiwa kubomolewa kwa kuwa ziko ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo hicho ambacho kwa mujibu wa sheria hazipaswi kuwapo.
Alisema wakazi hao wamekiuka Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali Maji namba 11 ya mwaka 2009 inayozuia maendelezo ya ujenzi na kilimo kwenye eneo la mita 60 kutoka kingo za maji.
Ofisa wa Bonde la Pangani mkoani Arusha, Joel Lao alisema kulinda vyanzo vya maji ni wajibu wa kila mwananchi kama inavyotamkwa kwenye Sera ya Maji ya mwaka 2002 na kazi ya mamlaka ya bonde hilo ni usimamizi wa sheria.
Alisema athari za kuwapo kwa shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji zinaweza kuvikaviusha na kusababisha magonjwa ya milipuko yanayosababishwa na maji machafu kutiririkia kwenye vyanzo vya maji.
Baadhi ya wakazi hao, Hashim Kassimu na Mwanamkuu Shabani walisema unalenga kuwarejesha katika umaskini kutokana na kudunduliza fedha na kujenga makazi yao sehemu hiyo.
“Umaskini unatunyemelea upya. Tunaanza upya maisha,” alisema Kassimu.
Diwani wa Kata ya Kiranyi, John Seneu alisema wakazi hao wanaodaiwa kuvamia eneo hilo walinunua na kupata vibali kutoka Serikali za vijiji na wengine walizaliwa maeneo hayo, hivyo Serikali itumie busara kufanya uamuzi.
No comments :
Post a Comment