Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha ACT – Wazalendo, imeazimia kutoshiriki uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliopangwa kufanyika Machi 20.
Akisoma maazimio hayo kwa waandishi wa habari jana, Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama chake kinapinga kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa sababu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilikiuka taratibu.
Vyama vingine ambavyo vimesusia uchaguzi huo ni CUF, UMD, Jahazi Asilia, Chaumma, UPDP, DP, CCK.
Zitto alisema Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha hakuwa na uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria kufuta mchakato uliokuwa ukiendelea wa kuhesabu kura Oktoba 28, mwaka jana na kwamba hali hiyo ilionyesha kuwa alichukua hatua hiyo kwa shinikizo kwa lengo la kuzuia ushindi wa chama kimoja kilichoelekea kuibuka na ushindi.
“Hatutashiriki na tunaitaka ZEC, iwatangaze madiwani na wawakilishi walioshinda katika uchaguzi wa Oktoba 25, ili watambuliwe na waanze kuwatumikia wananchi,” alisema Zitto.
Alisema hakuna sababu ya msingi kwa uchaguzi huo kurudiwa na kwamba waangalizi wa ndani na nje ya nchi, pamoja na jumuiya za kimataifa walishatamka kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika katika mazingira ya haki, huru na demokrasia.
“Nitoe wito wa Rais (John Magufuli) kuchukua hatua stahiki kwa mamlaka aliyopewa kikatiba kuhakikisha kuwa umoja na amani ya Taifa inaendelea kuimarika nchini.
“Kingine Rais Magufuli afanye kazi yake kikatiba katika sakata hili. Kwa sababu yeye siyo Rais wa Tanganyika, hivyo siyo vyema kulikimbia suala hilo kama alivyotamka jana (juzi) katika hotuba yake,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.
Juzi, Rais Magufuli alitoa msimamo wake kuhusu sakata hilo kwa kusema hataingilia mkwamo wa uchaguzi Zanzibar kwa kuwa anaheshimu utawala wa kisheria.
“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni huru kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kifungu kati ya 112 au 155. Lakini kama ilivyo tume huru ya uchaguzi duniani haiwezi kuingiliwa na rais yeyote. Ni kama ilivyo wa ZEC na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndivyo ilivyo,” alisema.
Zitto alisema Kamati Kuu ya ACT – Wazalendo iliyokutana juzi kwa zaidi ya saa tano, inaamini suluhu ya mkwamo huo wa kisiasa Zanzibar ni mazungumzo na siyo vitisho vya vyombo vya dola.
Mbali ya Zanzibar, Zitto alisema chama hicho kinaunga mkono juhudi za Dk Magufuli za kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wenye tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma na kutaka hatua hizo zifanywe kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, utawala bora na utu.

No comments :
Post a Comment