
Wanatumia mapaja yao kuandika, badala ya meza au madawati tuliyoyazoea. Baadhi hawatamani kuchafua sare zao za shule na kuamua kutandika kanga na makasha ya maboksi chini ili kujisitiri. Miandiko yao kwenye madaftari haifanani kabisa na sifa za mtu aliyejifunza somo la kuumba herufi.
Mazingira haya yanawasukuma kuwa watoro maana si rafiki kwao. Kwa upande wa wanafunzi wa kike ni rahisi kupata vishawishi hasa vya madereva na wahuni wengineo ambao mwisho wa siku ni kukatiza masomo kwa sababu ya kupachikwa ujauzito.
Wanaokabiliwa na hali hiyo ni wanafunzi 148 wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Mangoto iliyopo Kahe, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Inaumiza na haipendezi ukiwashuhudia katika mazingira hayo. Na inasikitisha zaidi wakikueleza tatizo lao la kukaa chini kwa kukosa madawati hata kusikia habari za mwitikio hafifu wa wazazi na walezi wanaojiweka kando kuchangia elimu kwa ajili ya maendeleo ya watoto wao na taifa kwa ujumla.
Hawataki tena kuhusishwa na uchangiaji, wanadhani serikali imebeba jukumu zima la elimu, na kazi iliyobaki kwao ni kuzaa tu.
Hawataki tena kuhusishwa na uchangiaji, wanadhani serikali imebeba jukumu zima la elimu, na kazi iliyobaki kwao ni kuzaa tu.
Ni changamoto inayopaswa kutatuliwa kwa haraka na siyo kuendelea kuifuga, ingawa kuna ukweli usiopingika kwamba, tatizo moja linapotatuliwa jingine hujitokeza katika sura nyingine. Lakini linapoibuka tatizo jipya, sharti ulikabili sawia na kwa wakati.
Tatizo la wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2016, wa Shule ya Sekondari ya Mangoto kukaa chini kwa kukosa madawati, linaibuka wakati Rais, Dk. John Magufuli ametimiza siku 100, tangu aingie Ikulu na kutangaza utoaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari nchini.
Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha nne, ina jumla ya wanafunzi 344 ni miongoni mwa shule za serikali katika jimbo la Vunjo, iliyoanzishwa tangu mwaka 2005.
Mkuu wa shule hiyo, Titho Kithojo anakiri kuwa, hali hiyo imekuwa ikiwaathiri wanafunzi hao kisaikolojia kwa kuwaona wenzao wa madarasa mengine ya kidato cha pili hadi cha nne, wanakaa na kutumia madawati hivyo kuwafanya wawe wasikivu na nadhifu tofauti na wao.
“Ni kweli tuna uhaba wa madawati kwa ajili ya kidato cha kwanza. Lakini uongozi wa Kata kwa maana ya Diwani Rodrick Mmanyi, ametusaidia kukodi viti vya plastiki kwa muda, ili kuwasaidia wanafunzi hawa waelekeze umakini wao na akili kwenye masomo yao…
Tumekwisha iarifu Halmashauri kuhusiana na hali hii na hakuna shaka kwamba wanalishughulikia haraka iwezekanavyo kupata madawati,”anasema Titho.
Zaidi, Diwani wa Kata hiyo, anasema lengo zuri la serikali ya awamu ya nne la kuanzisha shule za Sekondari za Kata, lilikuwa ni pamoja na kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi wa kuhudumia watoto wao kwenda shule za mbali, baada ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Anasema hiyo ni moja ya sababu ya uanzishwaji wa shule hizo, pamoja na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba, ambao wengi walishindwa kupata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari, baada ya kumaliza elimu ya msingi kutokana na uchache wa shule uliokuwapo wakati huo.
Halikadhalika, anasema tangu shule hizo za Kata zianzishwe miaka tisa iliyopita, kumeibuka changamoto lukuki, ikiwamo tatizo la wanafunzi kukaa chini kwa kukosa madawati, miundombinu ya vyoo vya shule kuwa katika hali mbaya na uhaba wa walimu, kutamalaki karibu katika kila kona ya nchi.
Kana kwamba haitoshi, anasema kwa kutambua hali hiyo ni kikwazo katika utoaji wa elimu bora, ndio maana ameamua kujitwisha jukumu zito la kukodi viti 150 vya plastiki kwa ajili ya kuwapunguzia machungu wanafunzi hao, hadi hapo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi itakapofanikiwa kutatua tatizo hilo.
“Baada ya kukaa na kutafakari kwa kina, juu ya adha wanayoipata wanafunzi wa Mangoto Sekondari, nilitambua kwamba kuna gharama za uongozi na zenyewe ndiyo hizo…Kwa hiyo ikanibidi niingine mfukoni na kukodisha kila kiti kimoja kwa Sh. 300. Sasa ukifanya mahesabu ya viti 150 kwa siku utaona ninavyoungua kwa kutoa Sh. 45,000 ambayo kwa mwezi ni sawa na Sh.1, 350, 000,” anasema Diwani.
Anasema kama Halmashauri ya Wilaya hiyo haitapeleka madawati hayo katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja, atalazimika kuendelea kutumia fedha zake kukodi viti hivyo, kutoka kwa wafanyabiashara ili kusubiri kukamilika kwa matengenezo ya meza au madawati.
Lakini je, wanafunzi wanazungumziaje adha hiyo? Mwanafunzi Jacquiline Paul, Dada Mkuu wa Shule hiyo, anasema upungufu wa madawati katika shule hiyo umekuwa ukiwapa adha kubwa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliojiunga mwaka huu na kwamba baadhi ya wasichana wanalazimika kutandika khanga na baadhi ya wavulana kukalia makasha magumu ya maboksi.
Juhudi zilizofanywa na Diwani wa Kata hiyo, zilimkuna mwanafunzi Goodlucky Okale ambaye anasema: “Alichokifanya Diwani kwa kutuletea viti vya kukodi tutakavyovitumia kwa muda ni jambo la kiungwana na la kiuzalendo. Sasa tutasoma na kuelewa, kwa sababu tuna sehemu ya kukaa na hatutawaza kufua wala kushindwa kwenda na kasi ya mwalimu darasani.”
Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), anasema hali hiyo haikubaliki kwa vile tatizo hilo limekuwa likimuumiza kichwa na kumpa msongo wa mawazo, ni kwa namna gani atairejesha sifa ya jimbo hilo kuwa kitovu cha utoaji wa elimu bora.
“Nimefanya ziara katika vijiji vyote 78, na nimekuta kuna shule 16, miundombinu yake ya vyoo iko taabani, achilia mbali uhaba wa madawati, madarasa, maabara, walimu na maeneo ya michezo. Tayari nimeshauriana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi, tutafute ufumbuzi wa haraka kuhusu aibu ya wanafunzi wa kidato cha kwanza Mangoto Sekondari kukaa chini kwa kukosa madawati,”anasema Mbatia.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Fulgence Mponji anasema:
“Kimsingi kama umepokea idadi kubwa ya wanafunzi baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango wa elimu pasipo malipo, uliotangazwa na serikali kupitia waraka namba 5 wa mwaka 2015, na ufafanuzi wa utekelezaji wake kutolewa kwenye waraka namba 6, wa mwaka 2015, ni lazima kutajitokeza suala hilo la upungufu wa madawati. Hivi sasa tunapambana kuhakikisha tunamaliza upungufu huo katika muda mfupi ujao.”
Lakini wakati Mangoto ikiguswa kwa tatizo la kwa kukosa madawati, Shule jirani ya Msingi ya Maendeleo iliyopo katika Kata hiyo hiyo ya Kahe, hali ni tofauti ambako wanafunzi 250 wanalazimika kusomea chini ya mti kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Wanafunzi wanaosomea nje kwa kukosa madarasa, ni wa darasa la kwanza, la pili na darasa la awali, pia shule hiyo ina walimu watano pekee na jumla ya wanafunzi 700.
Je, Mamlaka za serikali zinasemaje kuhusiana na wanafunzi hao kukosa madarasa?
Saimon Mlacha ni Ofisa Elimu-Msingi anasema: “Shule hiyo ni mpya na iligawanywa kutoka Shule ya Msingi Oria, kwa hiyo kutokana na mpango wa elimu bure kuanza kutekelezwa, wanafunzi waliongezeka kwa wingi hivyo kusababisha upungufu wa vyumba hivyo.
Anasemama na kuongeza: “Kwa sasa, tunapambana kuhakikisha watoto waliofurika katika shule hiyo wanapata vyumba vya kusomea na kuondokana na adha hiyo, ingawa suala la shule hiyo kuwa na walimu wachache linatokana na walimu wengine wawili akiwamo Mwalimu Mkuu kwenda masomoni.”
Ofisa Elimu huyo anakiri kwamba, katika awamu ya kwanza ya upokeaji wa fedha za ruzuku ya elimu bure, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, imepokea mgawo wa kiasi cha Sh. milioni 53.5, ingawa hata hivyo wanasubiri mgawo wa awamu ya pili ili kuzielekeza zaidi katika uendeshaji wa shule (capitation grants) na shule za elimu maalum za Msufini na Njia Panda ambazo zitakuwa ndio shule pekee zitakazonufaika na mpango wa elimu bure kwa kupelekewa fedha za chakula.
Kuhusu tatizo la uhaba wa walimu na madawati, Saimon anasema, Idara ya Elimu ya Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, ukiitazama kiuhalisia na kwa kuzingatia mahitaji ya shule tulizonazo, tunakabiliwa na upungufu wa walimu zaidi ya 200 na madawati 1,000.
Ofisa Elimu huyo anaeleza zaidi kwamba, walimu wengi walionao kwa sasa, wana umri mkubwa, na takwimu zinaonyesha zaidi ya 200 watastaafu katika kipindi cha mwaka mmoja, hadi kufikia mwaka 2017.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, ina jumla ya wanafunzi 75,545 wanaosoma katika shule za msingi na walimu 2,407.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment