Baada ya kutokuwa nanyi wapenzi wasomaji wa safu hii kwa takriban mwezi sasa, leo ninarudi tena uwanjani nikiwa na matumaini kwamba tunaanzia pale tuliposhia wakati ule.
Ni dhahiri kwamba mambo mengi yamejitokeza katika jamii yetu kwa kipindi hiki chote ambacho hatukuwa pamoja.
Kikubwa ni matukio mengi, yakiwamo ya maafa ambayo yameyakumba maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kusababisha maafa ambayo kwa kiasi kikubwa yameathiri na wakati mwingine kupoteza maisha ya watu, mali.
Ninachukua nafasi hii kuwapa pole wale ambao wamekumbwa na maafa hayo ambayo yanaelezwa na wataalamu wa hali ya hewa kuwa yanaweza kuendelea, hasa ikiwa mvua kubwa za msimu zitanyesha.
Ni wazi kuwa sisi kama wanajamii hatuna budi kuendelea kutoa tahadhari, hasa kwa wenzetu ambao wamejenga na kuishi katika maeneo hatarishi mijini na vijijini kuwa makini, hasa wakati huu wa mvua ambazo zinanyesha na kusababisha maafa.Pia, kwa upande mwingine, watu wa vitengo vya maafa ambavyo naamini wapo kwenye ngazi zote, kuanzia vijiji, mitaa, kata, tarafa, wilaya, mikoa hadi taifa, lazima wajitambue wao na wajibu walio nao katika kuwahudumia watu wote wanaokumbwa na maafa, yakiwamo ya mafuriko.
Tumeona mara nyingi, waathirika wa maafa hayo wakilalamika kutofikishiwa misaada, ikiwamo ya mahema, vyakula, blanketi na mashuka na hata vyakula, jambo ambalo halikubaliki.
Mbali ya maafa, bado tumeona unyama mwingi ambao unatokana na uhasama baina ya wakulima na wafugaji katika baadhi ya mikoa ambao umesababisha maafa, vifo kwa watu na mifugo, jambo ambalo binafsi linaniumiza kichwa kwa kiasi kikubwa.
Ikumbukwe, miaka michache iliyopita niliandika kwenye safu hii nikieleza kwamba sielewi uhasama huu unatokana na nini, zaidi ya ujinga mwingi tulio nao sisi, Watanzania.
Nilieleza wakati ule kwamba haiingii akilini kuona kwa mfano mkulima akidai kuwa hamhitaji mfugaji, ambaye naye angeweza kujidai kuwa ataishi bila kuhitaji chakula kinachozalishwa na mkulima.
Kwa kuendelea kutegemeana, sioni haja au sababu za jamii hizi mbili kuendelea kuishi kama chui na paka wakati zinaweza kuishi kwa amani, utulivu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma na nchi yetu kuwa yenye amani tena kwa kwa kiasi cha kujivunia.
Ninatambua kuwa ardhi haiongezeki, tofauti na idadi ya watu au mifugo na hivyo mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo, malisho na hata ujenzi yanazidi kuongezeka kila mwaka.
Kwa sababu hiyo, ni rai yangu kwa watawala, wasaidizi wa Rais John Magufuli watambue kuwa wanao wajibu mkubwa wa kumsaidia katika kuiweka nchi katika hali ya amani ikiwa kisiwa cha amani, utulivu.
Hapa, lazima mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wote waamke, watambue kuwa wakati wa fungate umekwisha, lazima wachape kazi kwa weledi, umakini wa hali ya juu.
Niseme wazi kuwa wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umepitwa na wakati na ndiyo maana mawaziri wa JPM, kama ambavyo anaitwa kwa sasa Rais Magufuli nawahimiza wajitambue.
Hakuna shaka, kazi anayoifanya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi haitakuwa na maana kama mwenzake wa Kilimo, Mwigulu Nchemba, Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, kutaja wachache hawakai chini na kufanya kazi kama timu.
Lukuvi ataongoza juhudi za kupima na kugawa hati, lakini haitakuwa na maana kama wakulima na wafugaji wanaendelea kugombea ardhi, iwe kule Kilosa, Kilombero na kwingineko.
Sioni sababu ya wakulima au wafugaji wa Serengeti na maeneo mengine nchini waendelee kuishi kama wakimbizi, eti kwa sababu wanaishi jirani na mbuga au hifadhi, hawatakiwi kufanya lolote katika maeneo yao.
Hili, lazima Profesa Maghembe alivalie njuga kwelikweli, kama tunataka kumaliza tatizo la ujangili ambalo limefikia hatua mbaya ya kuuawa kwa kutunguliwa kwa rubani wa helikopta ya doria kule Maswa mkoani Simiyu.
Hakuna shaka, haya ni matokeo ya uhasama ambao unaendelea baina ya hifadhi na wananchi wanaozunguka maeneo hayo, ambao ukisoma magazeti, kusikiliza redio au kuangalia runinga unakutana na malalamiko, vilio na kero.
Hilo, linafanyika pia kwenye maeneo zilizokuwa ranchi za Taifa wakati zikimilikwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) katika maeneo mbalimbali nchini.
Kule kuna vilio vya wakulima na hata wafugaji kama wa Kata za Kihanga, Mulamba, Igurwa, Kanoni na nyinginezo kule Karagwe, ambao kwa miaka mingi watu wanaishi kama wakimbizi kutokana na manyanyaso ya Ranchi za Kitengule na Mabale.
Hilo linatokea Kagoma, Missenyi na ranchi nyingine kule mkoani Kagera. Hakuna shaka linawasumbua watu wanaozunguka ranchi kama Ruvu, Mzeri, Kongwa na nyinginezo, ambazo zimeuzwa au kumilikishwa kwa wageni, wazawa, lakini bila kuangalia idadi ya mifugo iliyopo kwa sasa kwenye mashamba hayo pamoja na wananchi wanaozunguka maeneo hayo.
Hilo ni jukumu ambalo Nchemba, kama hakujua, lazima ashtuke kwa sasa kwani kuna vilio, kero Karagwe, eneo ambalo nina masilahi nalo, ambazo zimekuwa za muda mrefu, lakini hakuna anayejali, wala kusikiliza.
Ninaomba nimweleze mchana kweupe Waziri Nchemba, kilio cha wafugaji hao, hasa faini za ovyo wanazotozwa na watumishi walioko Kitengule au kule wilayani Karagwe kwa jumla, zinatosha kuwafanya waichukie Serikali yao ya JPM au ‘Mtoto wa Jeba’.
Hilo, linafanyika kule Rukwa, Katavi, Kilimanjaro na kwingineko nchini ambako kulikuwa na ranchi za umma, lakini ambako hakuna tena amani, utulivu ni uhasama mtu.
Kuna mizozo kwenye maeneo karibu yote ya mbuga na hifadhi za wanyama, maliasili zile tulizopewa bure na Mwenyezi Mungu, ambazo badala ya kuwa mkombozi, zimegeuka kuwa laana, kwani zinasababisha vifo, maumivu kwa wananchi, kiasi kwamba wanaiona Serikali kama imewatupa mkono.
Sioni sababu za mawaziri kufikiria kuwa kero ni zile zinazopatikana kwenye miji mikuu ya mikoa au wilaya, wakati kule vijijini ndiko watu wanaishi kwa shida, wanaumia kwa miaka mingi.
Nimweleze wazi Profesa Sospeter Muhongo, anayefanya kazi nzuri kwenye sekta yake, jinsi ambavyo utekelezaji wa miradi kama ule wa umeme vijijini kupitia REA, kama alivyoambiwa kule Karagwe umeacha maumivu kwa wengi, kiasi kwamba unachukiwa. Upo mfano wa wakazi wa Kijiji cha Rwambaizi, vitongoji au maeneo ya Omukigemu, Kanyamwanja, Kanamila, ambao mradi huo umewavuka licha ya wengi wao kuridhia mashamba yao yafyekwe ili kupisha mradi huo, bila wao kudai fidia, lakini sasa umeme upo Rwakilo, umewaacha waliojitolea mashamba wakilia.
Hilo lipo pia Kibona, Kata ya Igurwa, ambako watu walioridhia kufyekwa kwa mashamba yao, wanaona nguzo zinakwenda Kanoni, wao wanaishi kwenye giza kama mende, jambo ambalo linaweza kuchochea uharibifu wa miundombinu hiyo ambayo imegharimu kiasi kikubwa cha fedha zikiwamo za wahisani.
/Mwananchi.

No comments :
Post a Comment