
Rais Yoweri Museveni
Mtaalamu mmoja wa siasa nchini Uganda ameelezea mdahalo wa Februari 13, Jumamosi uliokutanisha wagombea wanane (8) wa urais nchini humo kuwa ni mbegu ya demokrasia nchini humo.
Waganda wengi waliusifu na kuusherehekea mdahalo huo ulioanza jioni na kumalizika siku ya pili siyo kwa sababu mgombea huyu au yule aling’ara, bali kwa sababu mdahalo uliwezekana kufanyika kwa kushirikisha wagombea wote.
Wagombea wanane walioshiriki katika mdahalo huo ni pamoja na Profesa Venansius Baryamureeba, Benon Biraaro, Dk Abed Bwanika, John Patrick, Amama Mbabazi, Rais Yoweri Museveni, Dk Kizza Besigye, mgombea pekee mwanamke, Maureen Kyalya na Joseph Elton Mabirizi.
Kufanyika kwa mdahalo huo kuliwapa Waganda nafasi ya kuwasikiliza wagombea wao na kuamua yupi ameweza kujieleza vyema na kushawishi wapigakura kumchagua kesho Alhamisi Feb, 18.
Jambo jingine lililovutia wengi katika mjadala huo uliandaliwa na Baraza la Dini la Uganda (IRCU) ni ukweli kwamba mdahalo huo ulikuwa ni wa kistaarabu, licha ya vijembe vya hapa na pale.
Kwenda vema kwa mdahalo huo kulitokana na kazi nzuri ya waongozaji akiwamo Mtangazaji wa Sauti ya America, Dk Shaka Ssali, Mkurugenzi wa Mawasiliano na uhusiano wa nje wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Joel Kibazo na Mkuu wa Idara ya Saana ya Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Makerere, Dk Suzie Muwanga.
Rais Museveni aliyehofiwa kuwa asingefika alijitahidi kuweka urais pembeni na kushiriki kama mgombea mtetezi wa kiti hicho.
Mwisho wa mdahalo ndipo Museveni alipoteza subira na kuzungumza kama mkuu wa nchi baada ya Besigye kulalamika kuhusu hatari ya amani kuvurugika iwapo uchaguzi hautakuwa huru na wa haki.
Museveni alimwambia wazi Besigye kuwa hana haki ya kuwatishia Waganda na kwamba uchaguzi utafanyika kwa amani na watakaofanya fujo watashughulikiwa.
Mdahalo wa Feb 13, ambao ulioneshwa na karibu vituo vyote vya televisheni nchini humo na kutangazwa na vituo vya redio ulikuwa ni wa pili kwa mwaka huu, lakini Museveni hakushiriki mdahalo wa kwanza kwa sababu mbalimbali.
Wakati mdahalo wa kwanza uliangalia zaidi masuala ya ndani, katika mdahalo huu wa pili mengi yaliyojadiliwa yalihusu zaidi mambo ya nje na mahusiano ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa katika wagombea wanane, wawili, Amama Mbabazi na Besigye walikuwa ni washirika wakuu wa Museveni miaka ya nyuma.
Hata hivyo, Waziri Mkuu mstaafu, Mbabazi aliyefanya kazi na Museveni kwa miaka 30 ndiye adui mpya wa rais huyo.
Kwa Besigye, daktari wa zamani wa Museveni, yeye ana miaka 10 katika upinzani na hii ni mara ya nne kugombea urais chini ya chama chake cha FDC.
Kabla ya mdahalo kuanza, wagombea wote wanane walitakiwa kushikana mikono kwa ajili ya sala ya pamoja, iliyoongozwa na Askofu Mkuu, John Baptist Odama wa Gulu, jambo ambalo lilivutia waganda wengi na kutoa matumaini ya kuvuka uchaguzi utakaofanyika Alhamisi, Februari 14 kwa amani.
Demokrasia ina gharama yake na zoezi hilo la mdahalo nalo lilithibitisha hilo.
Kwa tulioangalia mdahalo huo, tuliona wagombea makini na wengine waliokuja kufanya mzaha na uchekeshaji, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wagombea hapa nyumbani.
Katika mdahalo wa wagombea wanane, hakukuwa na muda wa kutosha kwa kila mgombea kujieleza vema na ndiyo maana wagombea wachekeshaji walionekana kama wanapoteza muda.
Miongoni mwa wagombea ambao Waganda walitaka kuwasikiliza ni Museveni, Mbabazi na Besigye.
Yaliyoigusa Tanzania
Mambo kadhaa ya msingi yalizoungumzwa katika mdahalo huo yaliigusa Tanzania kwa namna moja au nyingine.
Kwanza, kuonyesha jinsi wenzetu wanavyoithamini Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, (EAC), mdahalo huo ulifunguliwa kwa wimbo wao ya taifa na kufuatiwa na wimbo wa Afrika ya Mashariki, ambao kwa kweli binafsi sijawahi kuisikia hapa Tanzania ukiimbwa popote.
Katika mdahalo huo pia, mustakabali wa Afrika Mashariki ulijadiliwa ambapo Tanzania na Burundi zilitajwa kuwa nchi zinazochelewesha shirikisho la kisiasa. Tanzania pia, ilitajwa kuwa inakataa shirikisho ikihofia Waganda na Wakenya kuja kunyakua ardhi zao.
Hata hivyo, Museveni aliitetea Tanzania kwa kusema ilichopinga Tanzania siyo lengo la kufikia shirikisho, bali ni uharakishwaji wa mchakato wa kufikia lengo hilo, huku mgombea mchekeshaji Mabirizi akimpiga kijembe Museveni kuwa shirikisho haliwezekani mpaka Uganda ifuate mfumo wa wengine wa kuwa na ukomo wa utawala.
Wagombea wengine walishauri kuwa pamoja na shirikisho, nchi ziwe na uhuru wa kutunga sheria kuhusu haki maalumu kwa raia ikiwamo kumiliki ardhi.
Nafasi ya Uganda kufaidika kichumi katika Jumuiya ya EAC ilitajwa pia, kuwa inakuwa finyu kwa sababu ya Waganda kutojua Kiswahili, lugha muhimu ya eneo hili. Huu ulikuwa ni mtazamo wa mgombea pekee wa kike katika kinyang’anyiro hicho, Maureen Kyalya.
Alipoulizwa kama EAC ni muhimu, Museveni alitaja sababu mbili za Uganda kutaka kujumuika na nchi nyingine kuwa ni kutafuta ustawi wa watu wake na mkakati wa kiusalama. Akitoa mfano alisema Uganda inazalisha mahindi mengi kuliko mahitaji yake na hivyo inaangalia nchi za Afrika ya Mashariki kama soko muhimu.
Aidha, Tanzania ilitajwa katika mdahalo ule mara kadhaa ikisifiwa kwa hili au lile.
Katika tamko lake la mwisho, mgombea Mbambazi alimtaja Rais John Magufuli kama rafiki ambaye ameingia madarakani na kufanya mabadiliko ya msingi na ya kweli kwa Tanzania, ambayo yeye, Mbabazi angependa kuyapeleka Uganda.
Naye, Rais Museveni alipoulizwa uamuzi bora aliowahi kuufanya katika maisha yake alijibu kuwa ni ule alioufanya mwaka 1966 wa kuchagua kwenda kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Museveni, alisema kuja Tanzania na kujiunga na chuo hicho kulimpatia fursa ya kukutana na Mwalimu Nyerere na wanamapinduzi wengine wakiwamo Samora Machel, rais wa zamani wa Msumbiji.
Changamoto zilezile
Baada ya kusikiliza mdahalo wa wagombea urais wa Uganda nimegundua kuwa nchi zetu zinakabiliana na changamoto za aina moja. Elimu ilikuwa ni suala kubwa katika uchaguzi wa Tanzania na ni hivyo hivyo Uganda.
Mmoja wa wagombea alisema ni asilimia 37 wahitimu wa vyuo vikuu vya nchi hiyo ndiyo wanaoajirika, kwa maaana wanakuwa na ujuzi wa kuwezesha kuajiriwa.
Besigye alisema mahali pa kuanzia katika kutatua matatizo ya Uganda ni elimu. “Lazima tuwe na elimu mwafaka na bora. Na ndiyo maana tunazungumzia kurudisha mfumo wa kuingiza elimu ya ufundi katika mitaala ya elimu ya kawaida (reintroducing vocationalization of education).”
Mbabazi naye akasema: “Kama watoto wetu hawawezi kupata kazi Uganda, vipi unategemea wapate nje ya Uganda? Serikali yangu itajishughulisha zaidi na kuwapa vijana ujuzi ambao utawafanya waweze kushindana kimataifa.
Profesa Venansius Baryamureeba “Nataka kubadili mfumo wa elimu na kugeuza mitaala izalishe wahitimu wenye ujuzi unaoweza kuwafanya waajirike. ” Changamoto nyingine zilizotajwa ni pamoja na hali duni katika sekta ya afya, ukosefu wa ajira na wawekezaji matapeli.
Barua pepe: maoni@mwananchi.co.tz
No comments :
Post a Comment