Dk Asha-Rose Migiro
By Kalunde Jamal, Mwananchi
Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuteua watu watatu kuwa mabalozi kabla ya kuwatajia vituo vya kazi, umepokewa kwa hisia tofauti, baadhi wakiukubali na wengine wakihofia kuwapo ukakasi.
Rais Magufuli alimteua waziri wa zamani wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, waziri wa zamani wa mambo ya ndani ya nchi, Mathias Chikawe na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Ramadhani Dau kuwa mabalozi ambao watapangiwa vituo vyao baada ya taratibu za kibalozi kukamilika.
Dk Migiro (60) alikuwa mmoja wa wagombea 38 wa urais wa CCM na alishika nafasi ya tatu, wakati Chikawe alishindwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge ndani ya chama hicho huku Dk Dau akiwa ameshikilia nafasi hiyo NSSF tangu mwaka 2001.
Uteuzi wao umeacha gumzo sehemu mbalimbali, hasa kwenye mitandao, na wadau waliofuatwa na Mwananchi walikuwa na hisia tofauti.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni Waziri kivuli wa Mambo ya Nje wa Kambi ya Upinzani, alisema uteuzi wa rais una ukakasi.
Msigwa alidai Dk Migiro hakufanya kazi vizuri alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), lakini aliporudi nchini alifanya kazi kawaida tofauti na Kofi Annan, ambaye alifanya kazi vizuri baada ya kuondoka katika umoja huo wa kimataifa.
Alisema kitendo cha kukubali uteuzi huo kinaonyesha kuwa anakubali kila anachoambiwa.
“Alitakiwa ajitambue yeye ni nani na anapaswa kufanya nini. Kuteuliwa ni suala moja na kukubali ni jingine. Anaweza kukataa na kufanya vitu vingine vya msingi, vitakavyolinda heshima yake katika utumishi, ”alisema Msigwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alitofautiana na Mchungaji Msigwa akisema uteuzi huo unampa nafasi Dk Migiro kujipanga upya kisiasa, lakini akakubaliana kuwa angeweza kukataa uteuzi na kufanya mambo mengine.
Dk Mbunda alisema kuwa Dk Migiro alikuwa na mambo mawili ambayo angeweza kufanya; kuacha kabisa siasa na kuwa mshauri, au kukubali nafasi yoyote atakayochaguliwa ambayo itampa nafasi ya kujipanga upya kisiasa.
Mhadhiri wa UDSM, Profesa Abdallah Safari alisema Dk Migiro ana uwezo, hivyo alitakiwa afanye shughuli nyingine zinazoweza kumuweka karibu na jamii kama kuwa na taasisi yake.
Renatus Muhabi, ambaye ni katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), alisema nafasi hiyo wangepewa vijana wenye mawazo mapya.
“Kuna vijana wasomi wengi wa masuala ya diplomasia, waliomaliza shule miaka ya hivi karibuni na hawana cha kufanya. Wangepewa nafasi hiyo wangeleta mawazo mapya, mchango mpya, tofauti na kurudia watu wale wale kila siku,” alisema na kuongeza kuwa:
“Tangu ninakua nilikuwa nalisikia jina hilo na bahati mbaya zaidi sijawahi kuona makubwa aliyofanya zaidi.”
Muhabi alisema uteuzi wa kuelekezana unaweza kuhamisha mabaya ya zamani kwenda uongozi mpya.
Naibu Mkurugenzi Mafunzo, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa Chuo cha Diplomasia, Dk Kitojo Wetengere alitetea uteuzi wa Rais akisema anachagua watu kwa kuangalia vigezo mbalimbali ikiwamo uzoefu.
“Inawezekana Dk Migiro amechaguliwa kutokana na uzoefu wake katika mambo ya kimataifa. Anaweza kuipaisha Tanzania kwa sababu anafahamu mambo mengi,” alisema.
Mbali na Dk Migiro, wadau pia walikuwa na maoni tofauti kuhusu uteuzi wa Dk Dau, ambaye ni msomi aliyejikita katika masuala ya masoko.
Akizungumzia hilo, Mchungaji Msigwa alisema kumtoa NSSF na kumteua balozi ni kutumbua jipu kimyakimya.
“Uongozi wake ulikuwa wa kuibeba Serikali iliyopo madarakani na CCM. Kwa hiyo kwa ufanisi ule anapelekwa kwenda kufanya kazi za ushawishi, kuipaisha nchi kimataifa” alisema Msigwa.
No comments :
Post a Comment