
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Wakala wa Umeme na Ufundi (Temesa) juu ya uendeshaji wa vivuko na ukusanyaji mapato.
Sambamba na hilo, ameitaka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kubadilika kiutendaji ili kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea serikali.
Akizungumza jana na wafanyakazi wa wizara hiyo mjini hapa, Profesa Mbarawa, alisema serikali itachukua uamuzi mgumu ikiwamo kuwachukulia hatua wale wanaoshindwa kuwajibika.
Alisema wizara ilitangaza kutumia Sh. bilioni 60 kufanya matengenezo na ukarabati mkubwa wa uwanja wa ndege wa Musoma ili kuwaondolea adha wananchi wa mkoa na watalii wanaofika kutembelea hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Alisema hatua hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, hivyo serikali imetenga dola milioni 30 (zaidi ya Sh. bilioni 60 kwa ajili ya kazi hiyo.Aliongeza ulegevu katika kazi umesababisha adha kubwa kwa wananchi ambao sasa wanalazimika kusafiri hadi mkoani Mwanza kutafuta huduma hiyo huku uwanja huo ukikosa mapato.
Kuhusu Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Profesa Mbarawa alisema inapaswa kubadilika kiutendaji badala ya kutegemea serikali kufanya biashara ili kuongeza pato la taifa.
Hivi karibuni, Profesa Mbarawa alianza kazi ya kusafisha taasisi Zilizo chini ya wizara yake kwa kuwang’oa vigogo waandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (THA) na kuwahamishia makao makuu ya wizara. Pia alimsimamisha kazi meneja wa Fedha wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa ubadhirifu wa mamilioni ya fedha.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment