
Mkwamo wa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar umeibua mjadala mzito kwa kwa zaidi ya takriban miezi mitatu sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao ulifanyika Oktoba 25.
Mjadala huo umetokana na mambo makubwa mawili ikiwemo uhalali wa kikatiba na kisheria kwa Mwenyekiti wa Tume kufuta matokeo na uchaguzi wote na uhalali wa Kikatiba wa Rais wa Zanzibar kuendelea kubakia madarakani baada ya kukamilisha muda wake wa miaka mitano wa kuongoza Zanzibar.
Wanasheria wakongwe Zanzibar wamekuwa wakivutana juu ya uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume huku wengine wakipinga na wengine wakiunga mkono uamuzi wake wa kufuta matokeo ya uchaguzi kwa madai ulitawaliwa na vitendo vya udaganyifu.
Katika maamuzi yake Jecha anasema aliamua kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kutumia Kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar pamoja na kifungu cha 3 (1) na 5(a) vya sheria namba 11 ya Uchaguzi wa Zanzibar.Kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar kinawataja viongozi wa ZEC kuwa ni pamoja na Mwenyekit, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wanne na kila uamuzi wa tume ni lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi.
Wakati sheria ya uchaguzi kifungu cha 3(1) cha sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinasema kanuni, maelezo na matangazo yote ya ZEC yatakuwa na uhalali ikiwa yatakuwa yamesainiwa na Mwenyekiiti wa tume au Mkurugenzi wa uchaguzi.
Wakati Kifungu cha 5 (a) cha sheria hiyo ya uchaguzi ya Zanzibar kinazungumzia “usimamizi mzima wa mienendo ya jumla katika uchaguzi wa rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na viongozi wa serikali za mitaa ni jukumu la ZEC.
Hata hivyo, Mwansheria Mkuu wa Zamani Zanzibar (AG) Othman Masoud Othman anasema hakuna kifungu cha Katiba wala sheria ya Uchaguzi inayompa uwezo wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Othman anasema njia muafaka ya kumaliza mkwamo wa uchaguzi wa Zanzibar ni rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kuachia madaraka kupisha Tume maalum kuchunguza kama Mwenyekiiti wa ZEC alikuwa na mamlaka ya Kikatiba na kisheria kufuta matokeo ya uchaguzi na nafasi ya rais ishikwe na Jaji Mkuu wa Zanzibar kupisha uchunguzi huo.
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) na Wakili Mkongwe wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Awadhi Ali Said anasema Katiba ya Zanzibar vifungu vingi vimeporomoka tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.
Anasema tangu kuvunjwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) Agosti 13 mwaka jana kwa mujibu wa Katiba kifungu cha 90(1) Baraza jipya lilitakiwa liwe limeundwa ndani ya siku tisini hadi ifikapo Novemba 12 mwaka jana.
Anasema kukosekana kwa Baraza hilo hadi sasa Zanzibar ni uvunjaji wa katiba jambo ambalo halikubaliki katika misingi ya utawala wa sheria.
Awadhi ambaye alikuwa Kamishina wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anasema Rais na Mawaziri wake wamefikisha ukomo wa kubakia madarakani tangu Novemba 2 mwaka jana.
Anasema Kifungu cha 28 (2) (a) cha Katiba ya Zanzibar kinazungumza kuwa “Kufuatana na maelezo ya kifungu (1) cha kifungu hiki, Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano ya kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa rais wa Zanzibar.
Awadhi anasema huwezi kuteuliwa kuwa Waziri bila ya kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa msingi huo Mawaziri wote wamefikisha kikomo cha kubakia madarakani pamoja na rais.
Hata hivyo, Mwansheria Mkuu wa zamani wa SMZ, Hamid Mbwezereni na Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar , anasema Rais wa Zanzibar ni halali kuendelea kuwa rais mpaka rais anayefuata ale kiapo cha kuwa rais kwa mujibu wa kifungu cha 28(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Lakini anasema kwa bahati mbaya kuna wanasheria wanatafsiri Katiba na sheria tangu kuibuka mkwamo wa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa utashi wa kisiasa na kwa madhumuni ya kufurahisha makundi maalum yakiwemo ya kisiasa.
Mtazamo wa Mbwezeleni unaungwa mkono na wanasheria wengine Zanzibar akiwemo Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mtoto wa Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar , Abdulaziz Hamid Mahamoud.
Wanasheria hao wanasema mbali na ZEC kuwa na kazi ya kuandaa, kuitisha, kuratibu na kutangaza matokeo lakini pia pia inaweza kufuta matokeo.
Hata hivyo, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu anasema alitegemea mgogoro wa Kikatiba wa Zanzibar ungewasilishwa Mahakamani lakini wanasheria Zanzibar wameshindwa na badala yake wamebakia kulalamika mitaani tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka jana.
Jaji Makungu anasema kwa bahati mbaya mjadala wa katiba wa Zanzibar umeshindwa kupelekwa katika vyombo vya kutafsiri sheria badala yake kazi hiyo imeachwa ikifanywa na wanasheria mitaani na katika Vyombo vya Habari.
“Pale masuala ya kikatiba na kisheria yanapojitokeza basi tuyawasilishe katika chombo cha Mahakama kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu kwani hao ndiyo wenye mamlaka ya kisheria ya kutoa tafsiri,” anasema Jaji Makungu
Anasema wanasheria ni kiungo muhimu sana katika utatuzi wa migogoro ikiwemo ya kikatiba na kisheria katika jamii na kuwataka kuacha tabia ya kuburuzwa na wanasiasa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Pamoja na ushauri huo ambao unaonyesha njia nzuri ya kutafuta ufumbuzi wa mvutano wa Kikatiba, lakini umechelewa na sasa ZEC imeishatangaza Machi 20 mwaka ni siku ya marudio ya uchaguzi.
Ushauri huo kwa nini haukutolewa mapema kwa kuwa ungeweza kumaliza mkwamo wa kisiasa Zanziabra badala ya kutolewa sasa.
Hata hivyo, nadhani ni muhimu kwa wanasheria Zanzibar kujiepusha na kufungamana na makundi ya kisiasa ili waweze kuivusha Zanzibar katika mgogoro wa kikatiba.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment