Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, February 6, 2016

Siri ya CCM kukaa madarakani miaka 39

Ezekiel Kamwaga
Toleo la 443
3 Feb 2016

SEPTEMBA 22, mwaka 1975, Mwalimu Julius Nyerere, alipitishwa na Mkutano Mkuu wa vyama vya TANU na ASP kuwa mgombea urais wa Tanzania. Wakati huo, ingawa kikatiba nchi ilikuwa inajitambulisha kama ya chama kimoja –ukweli ulikuwa kwamba ilikuwa na vyama hivyo viwili.

Katika hotuba yake ya kukubali kuwa mgombea urais, Nyerere, kwa mara ya kwanza, alizungumza hadharani kuhusu tamaa yake ya kutaka kuona vyama hivyo viwili vikiungana na kuunda chama kimoja cha kisiasa kitakachokuwa na na mamlaka katika pande zote mbili za Muungano.

Kimsingi, Mwalimu alikuwa na wazo la kuunganisha vyama hivyo viwili kwa muda mrefu. Tatizo lilikuwa kwamba aliyekuwa Rais wa ASP, Abeid Amani Karume, alikuwa hataki kusikia hilo jambo.

Maandishi mbalimbali kupitia kwa watu waliokuwa karibu na Karume, akiwamo Salim Rashid, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, yanaeleza kuwa kufikia mwaka 1971, Nyerere na baba huyo wa aliyekuja kuwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume, hawakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara.

Hata hivyo, kifo cha Karume mnamo Aprili 6, mwaka 1972, kilimpa nafasi Aboud Jumbe Mwinyi kuchukua nafasi ya urais wa Zanzibar na wa ASP. Katika siku zake za awali, Jumbe hakuwa na tatizo na Nyerere.

Ndiyo maana, haikuwa ajabu kwamba siku moja baada ya Mwalimu kutoa pendekezo hilo, Jumbe alisema anaunga mkono hoja na mara moja ikaamriwa kwamba vyama husika vianze mchakato wa kutafuta maoni ya wanachama wake kuhusu endapo wanataka suala hilo au la. Wanachama waliunga mkono hoja na ndipo baadaye ikaundwa kamati ya kutengeneza Katiba ya chama kipya kitakachoundwa baada ya kuvunja ASP na TANU.

Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 20, 10 kutoka Tanzania Bara (TANU) na 10 kutoka Zanzibar (ASP). Wajumbe 10 kutoka Bara walikuwa ni Lawi Sijaona, Peter Kisumo, Kingunge Ngombale Mwiru, Peter Siyovelwa, Pius Msekwa, Jackson Kaaya, Basheikh Mikidadi, Beatrice Muhango, Nicodemus Banduka na Daudi Mwakawago.

Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe hao kumi walikuwa ni Thabit Kombo Jecha, Hassan Nassor Moyo, Abdallah Natepe, Seif Bakari, Hamis Hemed, Rajab Heri, Ali Mzee, Asia Amour, Juma Salum na Hamdani Muhidin.

Kamati hiyo ilifanya kazi yake katika kipindi cha takribani mwezi mmoja. Ilipofika Novemba mwaka 1975 kazi hiyo ilikuwa imekamilika. Ndipo, Januari 21, 1977, Mkutano Mkuu wa pamoja wa TANU na ASP ulikutana na kufanya uamuzi wa kuvunja vyama vyao na kuunda kimoja.

Azimio hilo la wajumbe wa Mkutano huo ambalo sasa ni sehemu ya utangulizi katika Katiba ya CCM lilisema hivi; “ Sisi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa pamoja kwa kauli moja tunaamua na kutamka rasmi kuvunjwa kwa TANU na ASP na kuundwa kwa chama kipya cha kipekee na chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba.

Na kwa vile wajumbe hao walikubaliana kwamba chama hicho kipya kitakuwa na kazi ya kuendeleza mapinduzi ya kijamaa na mapambano ya Ukombozi wa Afrika juu ya misingi iliyojengwa na TANU na ASP, chama hicho kikapewa jina la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwanini Jumbe alifurahia CCM?

Katika kitabu chake, Pan Africanism or Pragmatism?, Profesa Issa Shivji, anaeleza kuwa kuundwa kwa CCM kulikuwa na faida kubwa mbili kwa Rais Jumbe.

Mosi, kulipunguza nguvu ya Baraza la Mapinduzi lililokuwa limeundwa na wanasiasa wahafidhina walioshiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Wahafidhina hawa sasa nguvu yao ilipunguzwa na ukweli kwamba sasa CCM ndiyo ilikuwa chombo cha juu naye Jumbe akiwa Makamu Mwenyekiti wake.

Pili, kufuatia kuundwa kwa CCM,ilibidi Nyerere aunde upya Baraza la Mawaziri. Katika baraza hilo jipya la mawaziri, baadhi ya wajumbe walikuwa ni wanasiasa wahafidhina kutoka Zanzibar.

Kwa mfano, Seif Bakari aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi, Brigedia Yusuf Himid (baba mzazi wa huyu Mansour Yusuf Himid) alipelekwa Tabora kuwa Mkuu wa Brigedi ya Nyuki na wengine kama Natepe na Moyo walipewa uwaziri katika wizara nyingine.

Kwa tukio moja la kuvunjwa kwa ASP na kuundwa kwa CCM, Jumbe akawa ameua ndege wawili kwa jiwe moja; ameongezewa madaraka kwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama tawala chenye nguvu na pia wahafidhina wameondolewa Zanzibar.

Jumbe akawa sasa amepumua. Lakini, ni mabadiliko hayahaya ndiyo yalikuja kuwa mwiba kwa Jumbe baadaye. Lakini hii ni mada ambayo nitakuja kuijadili wakati mwingine.

CCM madarakani miaka 40
CCM iliundwa rasmi Februari 5 mwaka 1977. Keshokutwa Ijumaa, chama hicho kitakuwa kinatimiza miaka 39. Tangu kianzishwe hadi leo, hakijawahi kuwa nje ya madaraka.

Kimsingi, sasa kinaweza kuwa chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu kuliko kingine chochote barani Afrika (kama utajumlisha na miaka ya TANU na ASP).

Nini siri ya CCM kubaki madarakani kwa muda mrefu? Swali hili nimemuuliza Katibu Mtendaji wa Kwanza wa CCM, Pius Msekwa, katika mahojiano naye mwishoni mwa wiki iliyopita.

“ Nadhani siri kubwa ya CCM kubaki madarakani kwa muda mrefu ni ule utaratibu wa kupokezana madaraka. Kila baada ya miaka kumi, CCM inatoa mgombea mpya wa urais kabla watu hawajamchoka aliyepita.

“ Kama ukifanya utafiti, utaona kwamba kila Rais anayepita, watu wanakuwa hawamkubali sana wakati wa siku zake za mwisho. Anaweza kupendwa sana mwanzoni lakini mwisho inakuwa shida.

“ Mwinyi alipendwa sana mwanzoni. Lakini, katika siku za mwisho za utawala wake, hakuwa anapendwa sana. Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Benjamin Mkapa. Watu wana kawaida ya kuchoka kuona sura moja kila siku. Hata kama hakuna tatizo kubwa, watu wanapenda kuona sura tofauti.

“ Jakaya Kikwete alipoingia madarakani alipata kura nyingi sana. Ushindi wake ulikuwa wa kihistoria kwenye historia ya siasa za vyama vingi. Lakini, kama Kikwete ndiye angekuwa mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, sidhani kama tungepata ushindi kama tulioupata kwa Magufuli.

“ Ndiyo maana, naamini CCM inaweza kubaki madarakani hata kwa miaka mingine 50 ijayo ili mradi tu ihakikishe kuwa Rais aliye madarakani na viongozi wengine kwa ujumla wanapendwa na wananchi.

“ Kenneth Kaunda alikuwa anapendwa sana na Wazambia lakini hakupiga hesabu vizuri kuhusu muda wake wa kukaa madarakani. Matokeo yake wananchi wakamkataa na chama chake cha UNIP.
“ Watanzania hawana sababu ya kuichukia CCM.
 
Wanaipenda. Lakini pia, CCM ni lidude limoja likubwa hivi na huwezi kulishika. Hivyo, hakuna jambo ambalo linaweza kumpata mtu na akasema tatizo ni CCM.

“Chanzo kitakuwa ni mtu tu na ndiyo maana nasema dawa ni kuhakikisha tunaendelea na utaratibu wetu huu wa kubadilishana nafasi. Mfano ni Rais John Magufuli, leo Watanzania wameanza kurejesha imani yao kwa CCM, utafika wakati watamzoea na itakuwa fursa kwa mtu mwingine,” alisema Msekwa kwa kujiamini.

Kwenye mazungumzo yangu na Msekwa, niligusia kuhusu kile kilichoandikwa kwenye utangulizi wa Katiba ya CCM –kwamba kitaundwa chama “ chenye uwezo wa mwisho katika mambo yote kwa mujibu wa Katiba”.

Kwa maoni yangu, hii ilikuwa sehemu ya kile kilichokuja kuitwa “Chama kushika hatamu”. Ni kwamba kwa kauli ile, chama kilikuja kuwa juu ya serikali. Kikawa sehemu ya dola na leo kuna dhana ya chama-dola.

Msekwa anaamini kuwa duniani kote, ni lazima chama kiwe na nguvu juu ya serikali. Alitoa mfano wa namna chama cha Conservative kilivyoamua kumzuia Margareth Thatcher kwenye baadhi ya mambo ya kiserikali.

Ikanikumbusha matukio katika kitabu ninachosoma sasa cha Eight Days in September kilichoandikwa na Frank Chikane wa Afrika Kusini kuhusu namna Thabo Mbeki alivyoondolewa katika urais wa nchi hiyo kwa chama chake cha ANC kuamua hivyo.

Kuna sababu hiyo ya Msekwa lakini pia kuna watu wengine mashuhuri ambao pia wana sababu zao za kueleza kwanini CCM imekaa madarakani muda mrefu kuliko vyama vyote vilivyopo barani Afrika.

Museveni na Mpungwe wanasemaje?
Mwezi uliopita, nilipata bahati ya kuzungumza na mmoja wa wanadiplomasia na watumishi wa muda mrefu wa serikali, balozi Ami Mpungwe, kuhusu sababu iliyosababisha Mwalimu Nyerere asilazimishe kipenzi chake, Dk. Salim Ahmed Salim, awe Rais wa Tanzania baada yake na si Ali Hassan Mwinyi.

“ Siku moja niliwahi kukaa na Mwalimu na kumuuliza ilikuaje alishindwa kumfanya Dk. Salim awe mrithi wake. Alinijibu kwamba yeye alifanya hivyo kwa maslahi ya taifa. Alisema nilitaka kulazimisha lakini nikawakumbuka nyinyi vijana.

“Sikutaka kutengeneza Taifa ambalo Rais anayemaliza muda wake, anawalazimisha watu wamchague mtu anayemtaka yeye. Kama ningelazimisha kwa Salim, maana yake Mwinyi naye angechagua anayemtaka yeye. Ingekuwa tumetengeneza tabia mbaya kabisa,” Mpungwe alimnukuu Mwalimu.

Inaonekana, kanuni hii inafanya kazi hadi sasa. Inaaminika kuwa Mwinyi alipendelea John Malecela awe mrithi wake, ikashindikana. Benjamin Mkapa alipendelea hayati Abdallah Kigoda awe mrithi wake, ikashindikana. Jakaya Kikwete naye anafahamika kutaka Bernard Membe amrithi kwenye urais, lakini napo imeshindikana.

Kilichokuwa chama tawala nchini Kenya, KANU, kilikaa madarakani kwa zaidi ya miaka 30. Lakini, aliyekuwa Rais wa Kenya, Daniel arap Moi, aliamua kwamba mrithi wake awe kijana asiyefahamika kwenye siasa, Uhuru Kenyatta. Huo ndiyo ukawa mwisho wa KANU kuongoza Kenya.

Mwai Kibaki akapata fursa ya kuongoza Kenya. Kama Moi asingelazimisha Wakenya kumchagua Uhuru na angeacha KANU ichague mgombea ambaye anatakiwa, huenda chama hicho kingekuwa madarakani hadi leo. Pengine, Mwalimu aliepusha CCM na tatizo kama hili kwa uamuzi wake wa kutolazimisha mrithi.

Kwa namna hii, ni wazi kuwa ili vibaki madarakani kwa muda mrefu zaidi, ni lazima MPLA ya Angola ijiandae na mrithi wa Eduardo dos Santos anayekubalika na wananchi wa nchi hiyo badala ya yeye kulazimisha anayemtaka. Waangola wamemchoka tayari na chaguo lake halitakuwa na maana endapo mgombea hatakuwa wa chama hicho.

Dhana nyingine ambayo inaweza kueleza sababu za CCM kubaki madarakani hadi leo inatoka kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda. Kwenye miaka ya nyuma, aliwahi kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza mahali ambako Nyerere aliwazidi viongozi wengi wa Afrika. Kwa lugha ya Kiingereza, Museveni alisema “ Nyerere tamed the army”.

Sababu ya Museveni ni kwamba Nyerere alifanikiwa kuwa na udhibiti kwenye Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF). Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa chama tawala cha Uganda cha NRM, kama Kwame Nkrumah angekuwa na uwezo wa kudhibiti jeshi kama Mwalimu, angedumu madarakani yeye na chama chake. 

Kwenye kitabu cha Cheche, mmoja wa waandishi wa kitabu hicho, Karim Hirji, aliandika kwamba miongoni mwa watu waliopata nafasi ya kujiunga na JWTZ wakati ilipoanzishwa walikuwa ni waliokuwa wanachama wa Umoja wa Vijana wa chama cha TANU (TYL).

“ Pale ambapo Mwalimu aliwazidi akili viongozi wenzake wengi barani Afrika ni namna alivyodhibiti jeshi. Baada ya Mapinduzi ya Jeshi ya mwaka 1964, Nyerere alilivunja jeshi na kuunda JWTZ. Jeshi lile liliundwa na wazalendo na lilijengwa katika itikadi ya kijamaa na kichama. Haikuwa rahisi kumpindua Mwalimu kuanzia hapo,” alipata kusema Museveni.

Patrice Lumumba na chama chake cha MNC angeweza kubaki madarakani kwa muda mrefu kama si kupinduliwa na wenzake na kuzidiwa ujanja na Jeshi lililokuwa chini ya Joseph Desire Mobutu (Mobutu Sesseseko).

Chama cha CPP cha Kwame Nkrumah kingedumu madarakani kwa muda mrefu kama kiongozi huyo asingepinduliwa. Unaweza kusema hivyo pia kwa swahiba wa kisiasa wa Mwalimu, Milton Obote, na chama chake cha UPC.

Yeye alipinduliwa na Jeshi lililokuwa likimtii Jenerali Iddi Amini. Labda kwa sababu hii, Museveni ameamua kuwa na udhibiti wa kweli wa jeshi, ikiwemo wakati fulani kuhakikisha Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Rais (Presidential Guard Brigade-PGB) ni Brigedia Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wake wa kuzaa.

Hivyo, kwa kutumia sababu za muundo wake, kama alivyosema Msekwa, ulioifanya CCM kuwa na muundo uliogusa hadi katika ngazi za chini na kutokuwa na ubaguzi wa kidini, kikabila wala kikanda, mtindo wa kupokezana vijiti, kutolazimisha warithi na udhibiti wa jeshi na vyombo vingine vya dola, chama hicho kimebaki madarakani kwa muda mrefu kuliko kingine chochote barani Afrika.

Na hii, kwa mujibu wa Msekwa, ndiyo fahari kubwa ya waasisi wa chama hicho walio hai hadi sasa. Kwamba walifanikiwa kujenga “lidude” kubwa lililodumu madarakani kwa muda mrefu wakati wengine wakiishia njiani kama mabua kwenye moto.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/siri-ya-ccm-kukaa-madarakani-miaka-39#sthash.iqFMEYJK.dpuf

No comments :

Post a Comment