Rais John Magufuli
Oktoba 25, 2015 ilikuwa siku muhimu kwa Watanzania kwa sababu walipata fursa ya kuchagua viongozi wa kuongoza nchi kwa njia ya kidemokrasia kwa kutumia masanduku ya kura.
Kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi huo ulisimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Zanzibar ulisimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambao hata hivyo, uliingia dosari na kumfanya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kuufuta kabla ya kutangaza matokeo yote.
Hali hiyo ilizua sintofahamu baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kudai mgombea wake wa urais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliibuka mshindi na hata sasa chama hicho kimeendelea kulalamika kuwa kilidhulumiwa ushindi wake.
Kutokana na sintofahamu hiyo, kumekuwapo malalamiko na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya kumaliza tishio la kuibuka mgogoro wa kisiasa visiwani humo kutokana na ZEC kutoa tangazo la kufanyika uchaguzi wa marudio Machi 20 ambao umegomewa na CUF, huku wenzao wa CCM wakiridhia kufanyika kwa uchaguzi huo.
Wapo watu wakiwamo wanasheria ambao wamekuwa wakishinikiza Rais John Magufuli aingilie kati mgogoro huo wa uchaguzi Zanzibar wakidai anaweza kuumaliza kwa kutumia madaraka yake, lakini wanasahau kuwa nchi inaendeshwa kwa misingi ya Katiba na sheria.
Uchaguzi wa Zanzibar unaendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 na sheria zake ambazo hakuna sehemu yoyote inayompa ridhaa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania kuingilia uamuzi wa ZEC.
Ukitazama Katiba ya Tanzania ya 1977 katika sura ya nne inayozungumzia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar imefafanua vyema namna ya kuwapata viongozi na majukumu ya kila chombo miongoni mwa hivyo vilivyotajwa.
Ibara ya 104 (1) cha Katiba hiyo inasema “Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atachaguliwa na wananchi katika Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Zanzibar, na kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar inayohusu uchaguzi kwa ujumla au uchaguzi wa kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.”
Hii inadhihirisha wazi kuwa Rais wa Zanzibar yupo kisheria na mchakato wa kumpata upo kikatiba. Ni wazi kwa mujibu wa Katiba iwe ya Muungano au Zanzibar hazitoi fursa kwa kiongozi au taasisi yoyote kuingilia uamuzi wa vyombo vilivyowekwa kisheria kama tume za Taifa za uchaguzi.
Kama kuna kasoro katika utoaji wa uamuzi ni vyema ikatafsiriwa na Mahakama ambayo ni muhimili wa Dola wenye dhamana ya kuhakikisha haki inatendeka katika kufikia uamuzi.
Kwa kuwa Rais Magufuli hawezi kwa vyovyote vile kuingilia uamuzi wa ZEC kama ambavyo mwenyewe ameshasema, ni vyema kuisoma na kuilewa Katiba na mamlaka anayopewa Rais.
Ni wazi mgogoro wa kisiasa Zanzibar umetoa funzo kubwa kwa wananchi na hususan wanasheria kuzichakata katiba zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na ile ya Zanzibar ya 1984 ili kuhakikisha zinatoa suluhisho unapotokea mkwamo kama ilivyotokea Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Baadhi ya vifungu vinaacha maswali mengi kuliko majibu. Kwa mfano, ukitazama ibara ya 42 (3), mtu aliyechaguliwa kuwa Rais atashika kiti hicho hadi – (a) siku ambayo mtu atakayemfuatia katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais; au (b) siku ambapo atafariki dunia akiwa katika madaraka; au (c) siku atakapojiuzulu; au (d) atakapoacha kushika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.
Sura hiyo ya tatu kifungu (a) kilipaswa kuweka wazi ni katika mazingira gani madaraka ya Rais yatakoma. Kusema kwamba ni lazima Rais ajaye aapishwe kwanza ili kukoma madaraka ya mtangulizi wake ni unyongaji wa demokrasia.
Katika uchaguzi wa kawaida, ni halali kusema madaraka ya Rais yatakoma pale tu anapoapishwa Rais mpya, lakini kwa Uchaguzi wa Zanzibar wa 2015 kuna jambo jipya lililoibuka.
ZEC ndiyo iliyofuta uchaguzi kwa madai ya kutokea dosari katika mchakato wa kupiga kura, kuhesabu, kujumlisha na pia mmoja wa wagombea urais visiwani humo kujitangazia ushindi kinyume cha sheria, kabla ya Tume ya uchaguzi kutoa matokeo halali.
Kama ZEC inafuta uchaguzi ni busara wanasheria wetu wakatazama namna ya kuongeza vifungu vya sheria kwenye Katiba zetu ili kuondoa migongano na migogoro isiyo na lazima kama tunavyoshuhudia Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu uliopita.
Kinachoweza kuinusuru Zanzibar na machafuko ya kisiasa ni maridhiano ya kisiasa pekee.
Anthony Kayanda ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Kigoma, atapatikana kwa namba 0756721311, barua pepe:maoni@mwananchi.co.tz

No comments :
Post a Comment