
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema amesema hajutii kumpigia debe Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Pamoja na kutoswa ubunge, alidai jana kuwa bado anasimamia ukweli kwamba Rais Magufuli ndiye mtu aliyestahili kuliongoza Taifa hili.
Wakati Mrema akisema hayo, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amewataka Watanzania kuacha kummiminia sifa Rais Magufuli kwa kile alichoeleza kuwa ni wajibu wake akiwa kiongozi mkuu wa nchi.
Mrema
Akizungumza na gazeti hili, Mrema alisema kumnadi Magufuli kwa wananchi wa Vunjo kulitafsiriwa vibaya na ndiyo sababu waliamuadhibu kwa kumpiga chini katika kinyang’anyiro cha ubunge.“Nilijua wazi Rais Magufuli ni mtendaji ndiyo maana hata wananchi waliponiadhibu kwa sababu ya kumpigia debe sikuumia, najivunia chaguo langu na kiukweli anafanya miujiza ya hali ya juu.
“Kumpata kiongozi mwenye uthubutu kama alionao Rais Magufuli ni kazi kubwa Watanzania tuache unafiki tumpe nafasi afanye mambo makubwa zaidi,” alisema Mrema.
Hashim Rungwe
Alisema haoni kama kuna kitu kikubwa ambacho Rais Magufuli amekifanya tangu aingie madarakani zaidi ya kuendeleza kazi walizofanya wengine.
Alisema kumwagia sifa kupita kiasi ni ishara kwamba viongozi waliotangulia hawakuleta maendeleo jambo ambalo alidai halina ukweli.
Akitolea mfano sera ya elimu bure alisema utekelezaji wake usingewezekana kama Rais wa awamu iliyopita (Jakaya Kikwete) asingewekeza kwenye ujenzi wa shule za kata. “Unaweka elimu bure wakati watoto bado wanashinda njaa, unategemea wanachofundishwa wataelewa kweli kama siyo kupoteza muda basi atoe na chakula,” alisema Rungwe aliyeshiriki kinyang’anyiro cha urais mwaka jana.
No comments :
Post a Comment