Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, February 17, 2016

Wanasiasa, jumuiya za kimataifa watupie jicho la huruma Zanzibar

By Masoud Sanani, Mwananchi
Suala la Zanzibar bado ni ‘pasua kichwa’ na jitihada za ziada zinapaswa kuchukuliwa na viongozi na wanasiasa ili kuhakikisha hali ya utulivu na amani katika visiwa hivyo inaendelea kuwapo.
Kadri inapokaribia Machi 20, mwaka huu siku ambayo ilitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, hali ya hatari inayotishia amani visiwani inazidi kujitokeza.
Tangu Jecha alipofuta Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka jana, Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na mvutano unaoendelea kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Jecha alifuta uchaguzi huo wakati waangalizi wa ndani na wa kimataifa na yeye mwenyewe walishaeleza ulikuwa huru na haki na uliendeshwa kwa amani.
Pamoja na Jecha kutoa sababu tisa za kuufuta uchaguzi huo, Jumuiya ya Kimataifa haijakubaliana na sababu zake na kupinga kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao pia, unapingwa na CUF na kuungwa mkono na CCM kwa upande mwingine.
Kwa hiyo, kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati wa sherehe za kutimiza miaka 39 ya kuzaliwa CCM mjini Singida kuwa chama hicho kilikuwa kinajiandaa kushangilia ushindi zinashangaza.
Kikwete katika hotuba yake alisema CCM imepokea kwa unyonge kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa vile wao walikuwa wanajiandaa kushangilia ushindi.
Kauli za aina hiyo katika kipindi hiki cha mgogoro wa kisiasa Zanzibar hazisaidii kuleta hali ya amani, kwani zinazidi kuwaudhi wananchi walio wengi wa Zanzibar ambao walionyesha uamuzi wao katika sanduku la kupigia kura kuwa wanataka mabadiliko.
Hivi sasa kisiwani Pemba kuna baadhi ya nyumba zinachorwa alama ya X ambayo kwa kawaida alama hiyo huchorwa katika nyumba ambazo zinatakiwa kubomolewa jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya wananchi.
Inasemekana kuwa nyumba hizo zilizochorwa X zinadaiwa kuwa ni za wafuasi wa CCM na inadaiwa huenda waliochora ni wafuasi wa CUF, lakini kwa historia ya Zanzibar inawezekana waliofanya kitendo hicho cha kutishia amani ni watu wengine kabisa.
Historia
Ilitokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa Zanzibar mwaka 1995 kulikuwa na vitendo kadhaa vya hujuma kama vile kutia kinyesi katika visima, kuchoma shule na vitendo vyengine, lakini ilikuja kubainika baadaye kuwa vitendo hivyo havikufanywa na wafuasi wa CCM wala CUF.
Hali hiyo ilidhihirika baada ya wakazi wa eneo la Shengejuu kisiwani Pemba kuamua kuweka kikundi cha ulinzi wa siri katika shule yao na usiku wakakikamata kikundi cha watu wakiwa na galoni lenye mafuta ya petroli na bunduki wakitaka kuichoma shule hiyo.
Baada ya tukio hilo vitendo hivyo vya hujuma mbalimbali katika Kisiwa cha Pemba vilikoma kwani ilijulikana dhahiri kuwa havifanywi na wananchi wa kawaida, bali watu wengine.
Viongozi kadhaa wametoa kauli kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, lakini mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahim Kaduma amekuwa mkweli na hakutaka kutafuna maneno kuhusu suala la Zanzibar.
Kaduma aliungana na wadau wengine ambao wanapinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa maelezo kuwa maridhiano baina ya pande zinazosigana yana nafasi nzuri ya kutatua mgogoro uliopo.
“Katika suala la Zanzibar nadhani CCM tungekubali kushindwa. Mimi ni MwanaCCM, lakini nasema tungekubali kushindwa ningekuwa Dk Ali Mohammed Shein ningelinda heshima yangu maana hii ni hatari,” alisema Kaduma.
Mzee kaduma alisema kwakuwa suala la Zanzibar ni baina ya vyama vya CCM na CUF, mtu pekee wa kutafuta ukweli ni mwenyekiti wa CCM.
“Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiye mwenye uwezo mkubwa wa kuweka mambo ya Zanzibar sawa maana yeye ndiye mwenyekiti wa CCM na suala lenyewe linakihusu CCM na CUF ingawa kwa mbali sana Magufuli anaweza kufanya lolote kuondoa tatizo lililopo,” alisema.
Alisema anaamini CCM ingetenda haki kama ingepokea matokeo kama yalivyokuwa ambayo hata waangalizi wa ndani na nje wamesema hayakuwa na dosari.
Ni vyema Rais Shein angekubali matokeo. Chama pia, kingefanya hivyo. Huko ndiko kujisahihisha.Kufanya hivyo Rais Shein angeondoka na heshima yake.
Wakati kiongozi muadilifu Kaduma akitamka maneno hayo ya busara, Kikwete analifanyia mzaha suala la Zanzibar kwa kutoa kauli ambayo ukiipima haifai kutolewa na kiongozi mwenye hadhi kama yake.
Hakuna Mtanzania ambaye hana uhakika kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alionyesha upinzani mkali katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba mwaka jana. Sasa Kikwete anaposema walijiandaa kushangilia anajaribu kumdanganya nani?
Ikumbukwe kuwa Zanzibar hasa Kisiwa cha Pemba wananchi kadhaa walipoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ghasia zilizozuka Januari 2001 baada ya polisi kutumia nguvu kuzima maandamano ya wafuasi wa CUF kutokana na masuala hayo ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilizalisha wakimbizi baada ya vurugu hizo kwa baadhi ya wananchi kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya na baadaye Somalia katika harakati za kuhofia mkono wa Serikali.
Kwa hiyo mwanasiasa wa Tanzania washirikiane na Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya kweli Zanzibar ili kutohatarisha maisha ya wananchi na kuwapa fursa nzuri ya kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kuwa na hofu waliyonayo hivi sasa.
Ni vigumu kuamini kwamba uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20 katika mazingira ya sasa unaweza kufanyika kwa amani, utulivu na kwa uhuru na haki na kila mmoja akapata haki yake.
Haihitaji kuwa mtabiri kugundua hali ya hatari iliyopo iwapo uchaguzi Zanzibar hautashirikisha vyama vyote viwili vikubwa vya CCM na CUF, kwani vyama hivyo ndivyo venye wafuasi wengi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa na Jecha, CCM na CUF kila kimoja kilipata viti 27 vya Wajumbe katika Baraza la Wawakilishi (BLW) na hakuna chama kingine chochote cha siasa kilichoshinda hata jimbo moja.
Wajumbe wa BLW wa CUF na madiwani wa chama hicho ambao matokeo yao yalifutwa na Jecha licha ya wasimamizi wa majimbo na wadi kuwatangaza washindi na kuwakabidhi vyeti vya ushindi wanajiandaa kufikisha suala hilo mahakamani kutetea nafasi zao na kupinga uchaguzi wa marudio.
Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuingilia kwa dhati mgogoro wa Zanzibar na kuacha mtindo unaoendelea wa kutoa matamko.
maoni@mwananchi.co.tz     

No comments :

Post a Comment