
Tukio hilo lilitokea wakati alipofika mahakamani hapo kusikiliza kesi inayomkabili ya kudaiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Katika tukio hilo lilitokea jana saa 4:00 asubuhi baada ya mbunge huyo kuwasili mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi yake iliyopangwa kusikilizwa ushahidi wa utetezi.
Hata hivyo, baada ya askari kanzu kumkamata na kumuweka mbunge huyo chini ya ulinzi, wakili wake, Peter Kibatala, alihoji uhalali wa kumshikilia wakati alitakiwa kusikiliza kesi ya jinai inayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.“Niliwahoji kwa nini wanamshikilia wakati anatakiwa kusikiliza kesi yake ya jinai inayomkabili ambayo inatakiwa kusikilizwa na kumalizika kwa wakati ili kuondoa mlundikano wa kesi… walikubali kumwacha hadi atakapomaliza kusikiliza kesi yake,” alieleza wakili wa utetezi, Kibatala wakati akihojiwa na Nipashe.
Mshtakiwa alipanda kizimbani saa 5:03, ushahidi wa utetezi ulitolewa na Waandishi wa Habari, Shaban Matutu wa New Habari (2006) Limited na Josephat Isango kutoka Mwanahalisi.
Kwa nyakati tofauti, mashahidi hao, walidai Desemba 14, mwaka jana, wakiwa katika kiwanda cha Tooku Garmet Limited, hawakusikia mtu yeyote akielekeza lugha ya matusi dhidi ya Makonda.
Akiongozwa na Kibatala, Matutu alidai siku hiyo aliagizwa kwenda kufanya kazi kama mwandishi katika kiwanda hicho, kuhusu mgogoro wa wafanyakazi na kiwanda.
“Nilifika kiwandani hapo saa nne asubuhi kuchukua habari, niliwakuta wafanyakazi wakiwa kwenye mgomo… nilimuona Kubenea ambaye alifika kwa ajili ya kutatua mgogoro, lakini saa tisa alasiri, alifika Makonda eneo hilo na kufanya mazungumzo na wafanyakazi na viongozi wao,” alidai na kuongeza:
“Makonda alishika kipaza sauti na kuwaeleza wafanyakazi kwamba huo ndio mwisho wa mkutano na akiwa Rais wa Wilaya ya Kinondoni, amefunga mkutano na haruhusiwi mtu mwingine kuzungumza…Kubenea alihoji kwa nini Makonda anafunga mkutano wakati mgogoro huo aliuanza yeye na hajampa nafasi ya kuzungumza wakati yeye mbunge siyo kibaka, amekwenda kwa kuwa amechaguliwa na wananchi,” alidai Matutu.
Akifafanua zaidi shahidi huyo alidai baada ya Kubenea kuhoji uhalali wa kufungwa mkutano huo, Makonda aligeuka nyuma na kumuuliza nani ni kibaka, mbunge huyo alimjibu kwamba hakumwita yeye (makonda) kibaka.
”Mara nilimsikia Makonda akiwaamuru polisi wamkamate Kubenea na walitii amri hiyo wakamuweka chini ya ulinzi…,” alidai Matutu.
Naye shahidi wa nne, Isango alidai hakumsikia mtu akitoa lugha ya matusi ikiwamo kutamka kibaka wala mpumbavu dhidi ya Makonda.
Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, mwaka huu, kwa ajili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja za majumuisho ya kesi hiyo za kama mshtakiwa ana hatia ama la.
Baada ya kuahirishwa kesi hiyo askari kanzu wawili waliondoka na Kubenea mahakamani hapo kwa ajili ya kwenda kumhoji dhidi ya tuhuma za kufanya vurugu katika uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam.
SOURCE: NIPASHE
No comments :
Post a Comment