Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimsimamisha kazi daktari wa upasuaji katika hospitali ya Ligula mkoani Mtwara.
Sababu ya kusimamishwa kwake kunatajwa kuwa ni kuomba rushwa kwa Tatu Abdallah aliyekuwa akimuuguza baba yake.
Tatu akiwa kwenye mahangaiko ya kuokoa maisha ya baba yake, alijikuta akiwa kwenye dimbwi zito la kero ambazo hatimaye aliamua kuzitoa hadharani.
Bila ajizi alimvaa Waziri Mkuu na kumweleza kwa ufasaha yaliyomkuta kwenye hospitali hiyo, hususan kutoka kwa kwa daktari wa upasuaji.
Alidai, ‘‘Februari Mosi nilimleta baba hapa hospitali , nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa nikanunue dawa za Sh85,000 hapo nje kwenye duka la dawa na uzi wa kushonea kwa Sh25,000. Pia daktari akaongeza kwamba anataka Sh100,000 za kwake. Lakini hadi Februari 7, hakufaniwa upasuaji’’
Maneno hayo na mengine mengi yalimfanya Waziri Mkuu ambaye alikuwa kwenye ziara ya siku chache aingiwe na ubaridi na kichefuchefu kuhusu utendaji wa aina hiyo.
Aliamua kuwakusanya watumishi wa hospitali hiyo na kumtaka Tatu kumtambua mtumishi aliyedaiwa kuomba rushwa.
Pamoja na kwamba hakuna daktari aliyejitokeza, lakini Tatu alipoambiwa akamshike mkono mhusika, alikwenda harakaharaka na kumkamata aliyedai ndiye mhusika.
Hata kama daktari huyo atajitetea na kushinda kwa hoja, ukweli ni kwamba vituko na vioja vya aina hiyo ni vingi kwenye ofisi za umma. Vituko vya watumishi wa afya kuomba rushwa, kuwatukana wagonjwa na hata kuwaibia dawa vimejaa katika hospitali nyingi nchini
Mbali ya watumishi wengi kuomba rushwa ya waziwazi, wapo watumishi wanaofanya vituko ambavyo vinawaondolewa hata ubinadamu.
Maagizo ya ‘kanunue dawa’ yanayotolewa na madaktari au wauguzi kwa ndugu wa wagonjwa ni ya kawaida na yanaonekana kukubalika.
Suala la kununua dawa kwa asilimia 90 ni jukumu la ndugu wa wagonjwa, hivyo siyo dhambi, lakini vitendo vya dawa iliyonunuliwa kupotea wodini au vituko vya wahudumu hao kudaiwa rushwa ndivyo vinavyochefua.
Hata mkoani Mbeya ipo hospitali kubwa ya umma ambayo muuguzi wake alimtamkia ndugu wa mgonjwa awe anawahi kumpa dawa mgonjwa wake aliyelazwa.
Kwa bahati nzuri kituko hicho kiliripotiwa kwa viongozi wake na hatimaye alichukuliwa hatua. Lakini ukweli ni kwamba pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano kudhamiria kuondoa kero hizo, wafanyakazi wengi wa umma walishazoea uchafu, hivyo hawaamini kama kweli wanatakiwa kujisahihisha.
Kwa mfano, maagizo yanatolewa kitaifa watumishi wavae vitambulisho, lakini wengi hawajali. Serikali inaagizwa watendaji na hata viongozi msikalie matatizo na kusubiri Serikali kuu, lakini kero zinazidi kwenye ofisi za umma.
Kwa jumla kero kwenye huduma za matibabu ni nyingi, lakini nyingine zinaudhi zaidi.
Ni wazi kwamba mzigo wa ugonjwa unakuwa mkubwa kwa Watanzania wengi kutokana na kutokuwa na bima za matibabu.
Tanzania kwa sasa ino zaidi ya watu 45 milioni, lakini takwimu za hivi karibu zinaonyesha karibu asilimia 19 ya hao ndiyo wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na matawi yake ya CHF na Tiba kwa Kadi. Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na uhalisia wa idadi ya watu, kwani hata magonjwa yanajitokeza mara kwa mara.
Lauden Mwambona ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mbeya. lmwambona@mwananchi.co.tz
No comments :
Post a Comment