Spika Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Pandu Ameir Kificho.
Spika Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Pandu Ameir Kificho, ameanguka katika uchaguzi wa kuwania wadhifa huo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kushika wadhifa huo kwa miaka 25.
Kuanguka kwa Kificho kunaashiria mwisho wa nguvu za kisiasa ndani ya CCM za waliokuwa viongozi wa Bunge Maalum la Katiba.
Kificho alikuwa mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalum la Katiba kabla ya kuchaguliwa kwa Samuel Sitta ambaye pia alianguka katika mchakato wa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM wakati Rais John Magufuli alipoibuka kidedea. Sitta alianguka tena katika jaribio lake la kutaka kugombea uspika wa Bunge kupitia CCM baada ya kupitishwa kwa jina la Spika Job Ndugai.Uchaguzi huo ulifanyika Makao Mkuu ya CCM Kisiwandui chini ya Mwenyekiti wake aliyekuwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Idd.
Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar Waride Bakar Jabu alisema majina matatu yalipigiwa kura katika uchaguzi huo.
Awali, wagombea waliokuwa wakiwania wadhifa huo walikuwa nane, akiwemo aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pereira Ame Silima na Mrajisi Mkuu wa Serikali, Abdalla Waziri Ramadhan.
Wengine ni Mwaakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahamoud Mohamed Mussa, Hakimu mstaafu Janeth Nora Sekihola, David Mwakajuki, Waziri wa zamani wa Miundo Mbinu na Mawasiliano, Zuberi Ali Maulidi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis ambaye alijitoa kabla ya mchujo wa majina kufanyika.
Waride alisema kuwa baada ya vikao vya Kamati maalum ya Halmashari Kuu ya CCM Zanzibar kujadili majina ya wagombea waliojitokeza, Kamati Kuu ndiyo ilichagua majina matatu baada ya kukutana juzi bila ya Mwenyekiti wake Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete.
Majina hayo yalikuwa Spika Kificho, Maulidi na Janet.
Waride alisema katika uchaguzi huo, Maulidi ambaye ana shahada ya biashara ameibuka mshindi baada ya kupata kura 55 na kumwagusha Kificho aliyepata 11 na Janet kura 4, kati ya kura 72 ambapo kura mbili ziliharibika.
Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Balozi Iddi alisema kuwa nafasi ya Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Kamati utaratibu wake utatangzwa baadaye kwa wajumbe.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Zuberi alisema kuwa anatarajia kufanya mabadiliko makubwa kwa kuhakikisha Baraza linatekeleza majukumu yake kwa viwango vya ubora vya utendaji wake.
Alisema kuwa pamoja na Baraza la Wawakilishi kutokuwa na upinzani baada ya wajumbe wake wote kutoka CCM, lengo lake ni kuisimamia serikali kwa umakini na kutetea kero za wananchi katika majimbo yao.
“Nitatumia uzoefu wangu niliopata nikiwa Mwenyekitiwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulijengea uwezo Baraza katika kutekeloeza majukumu yake ya kikatiba na Sheria,” alisema Maulidi.
Akizungumza na Nipashe, Kificho alisema amepokea matokeo hayo bila ya kinyongo na wajumbe wametumia haki yao ya kidemokrasia.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment