Wafanyabiashara wakiendelea na biashara zao katika soko la Mwanakwerekwe, Zanzibar jana.
Hatimaye aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, ameshinda kama ilivyotarajiwa katika uchaguzi mkuu wa marudio uliofanyika Jumapili iliyopita na kuapishwa juzi, huku amani ikitawala muda wote.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Dk. Shein alitetea nafasi yake hiyo kwa ushindi wa zaidi ya asilimia 91 ya kura za watu waliojitokeza kwenye uchaguzi huo wa marudio, ambao CCM walitarajiwa kushinda kirahisi baada ya mahasimu wao wakubwa, Chama cha Wananchi (CUF) kugomea kwa kile walichoeleza kuwa ni kukosekana kwa sababu za msingi za kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25 na mgombea wao, Maalim Seif Shariff Hamad kuelekea kushinda kwa zaidi ya asilimia 50.Licha ya CUF kugomea na pia waangalizi mbalimbali wa kimataifa wakiwamo kutoka Jumuiya ya Madola na Umoja wa Ulaya (EU), kususia kwa maelezo kuwa uchaguzi wa awali haukuwa na kasoro kubwa kiasi cha matokeo yake kufutwa na ZEC, bado uchaguzi wa marudio ulifanyika kwa amani Jumapili iliyopita na Shein kutangazwa mshindi.
Baadaye, Shein aliapishwa rasmi Jumapili na hivyo kushika tena madaraka ya kuviongoza vsiwa vya Zanzibar kwa miaka mingine mitano, yaani hadi mwaka 2020.
Wakati wa mchakato wote wa kuelekea uchaguzi huo wa marudio, kufanyika kwake na hata baada ya kuapishwa kwa Dk. Shein, kuna mambo mawili makubwa ambayo pengine baadhi ya watu hawakuyatarajia hapo kabla. Nayo ni kushamiri kwa amani na utulivu katika kipindi chote na pili, ambalo ni jambo hasi, ni kuendelea kusuasua kwa shughuli za kibiashara katika baadhi ya maeneo huku pia bei za bidhaa za vyakula zikiendelea kuwa za juu kuliko ilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu wa awali uliofanyika Oktoba 25.
AMANI, UTULIVU
Tofauti na wengi walivyotarajia hapo kabla, hali ya amani na utulivu iliendelea kutamalaki visiwani Zanzibar katika kipindi chote cha kuelekea uchaguzi wa marudio na hata baada ya kufanyika na mwishowe Dk. Shein kuapishwa.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, badhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa za Zanzibar walisema kuwa hali hiyo imechangiwa pia na mambo mawili, kwanza ikiwa ni kauli za viongozi wengi wa kisiasa wakiwamo wa CCM na CUF ambao kwa kiasi kikubwa waliepuka kauli za kuchochea ghasia miongoni mwa wanachama wao na pili ni doria madhubuti iliyoimarishwa visiwani humo na vikosi mbalimbali vya askari katika kipindi chote cha kuelekea uchaguzi huo na hadi kufikia sasa.
“Licha ya kupingana karibu kwa kila jambo, bado watu wenye nguvu ndani ya CCM na CUF walijiepusha na kauli za uchochezi kwa wanachama wao. CCM walihimiza watu kujitokeza kupiga kura kwa amani huku wale wa CUF wakiwahimiza watu wao kutojitokeza na badala yake kutulia majumbani mwao ikiwa ni ishara ya kupinga uchaguzi huo wa marudio… jambo hilo lilisaidia sana kutunza amani inayoonekana sasa visiwani hapa,” mmoja wa wachambuzi wa siasa visiwani Zanzibar aliiambia Nipashe.
Aidha, mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Omar, mkazi wa Kiembe Samaki mjini Unguja, alisema wale waliotaka kupiga kura walifanya hivyo bila bughudha huku walioamua kutopiga kura wakifanya hivyo pia pasi na kulazimishwa.
“Waliotaka kupiga kura waliweza kuitumia haki yao hiyo na wale ambao hawakutaka kupiga kura walikaa majumbani mwao na kuendelea na shughuli zao bila ya kuwabughudhi wengine. Hili ni jambo lililosaidia kutunza amani,” alisema Khadija.
Aidha, mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa alivipongeza vikosi mbalimbali vya majeshi kwa kutekeleza vyema wajibu wao wa kuhakikisha kuwa hakuna jambo kubwa la uvunjifu wa amani.
“Ulinzi ulikuwa wa kutosha karibu katika maeneo yote muhimu. Jambo hili nalo limechangia kuwapo kwa uhakika wa amani na utulivu na halipaswi kusahaulika,” mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa za Zanzibar aliongeza, huku akikumbushia namna vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama vilivyoshirikiana na polisi kutanda katika maeneo mbalimbali visiwani na hivyo kuzima uwezekano wa kuwapo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumzia hali hiyo ya amani na utulivu, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi, alisema kuwa wameridhishwa kwa kiasi kikubwa na utulivu ulipo na kwamba, pamoja na hali hiyo, Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi wakati wote ili amani iliyopo sasa ibaki kuwa ya kudumu.
Aliongeza kuwa hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuwa nzuri kabla, wakati na baada ya uchaguzi awa awali, wa marudio na hata sasa kwa sababu hakuna matukio makubwa ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa.
Msangi aliwataka Wazanzibari kuendelea kudumisha amani ya nchi iliyopo kwa sababu bila ya kuwapo kwa amani, shughuli za kijamii, kiuchumi na maendeleo kwa ujumla hazipata fursa ya kufanyika na hivyo kurudisha nyuma kasi ya maendeleo.
“Tumeshuhudia siku ya uchaguzi wa marudio Machi 20 (Jumapili) kila mtu alikuwa akiendelea kufanya shughuli zake bila ya kubughudhiwa… basi tunataka hali hiyo iendelee kuwapo muda wote na tumejipanga kuhakikisha kuwa hilo linawezekana,” alisema Msangi.
Siku chache kabla ya uchaguzi wa marudio na hata wakati wa uchaguzi huo, maeneo mengi ya Zanzibar yalikuwa na askari wenye silaha wa vikosi mbalimbali wakiwamo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), huku wengi wao wakionekana kwenye maeneo nyeti kama ya Bandari, makao makuu ya ZEC na Uwanja wa Ndege.
Aidha, upekuzi mkali kwa kila abiria aliyekuwa akiingia Unguja kupitia bandarini ulikuwa ukifanyika kabla ya siku ya uchaguzi.
BIASHARA NGUMU, MAISHA MAGUMU
Wakati hali ikiwa ya kutia moyo kuhusiana na hali ya amani na utulivu, hali ya maisha na biashara visiwani hapa imeendelea kuwa ngumu.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa bado bei za bidhaa nyingi, hasa za vyakula, zimeendelea kuwa za juu kulinganisha na vile ilivyokuwa kabla ya uchaguzi wa awali wa Oktoba 25 na kwamba, hata baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio na Shein kurejea madarakani, hali imeendelea kuwa ngumu na kuwakwaza wananchi wengi wa kipato cha chini.
Aidha, shughuli za biashara katika baadhi ya maeneo zimeendelea kurudia katika hali yake ya kawaida kwa kasi ndogo, mfano mzuri ukiwa ni katika eneo la Forodhani.
Mfanyabiashara mmojawapo wa Soko la Darajani mjini Zanzibar, Ali Khamis, alisema hali ya utulivu na amani ilimuewezesha yeye na wenzake kadhaa kuendelea kufanya biashara zao sokoni bila ya kubughudhiwa katika siku ya uchaguzi wa marudio, tofauti na hofu ya baadhi ya watu waliodhani kwamba pengine hali ingekuwa ngumu kwao kisalama.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa, Khamis alisema hadhani kama bei zimebadilika sana bali ni za wastani.
Hata hivyo, alikiri kwamba baadhi ya bidhaa kama viazi mbatata, bei yake iko juu zaidi sasa na hadhani kwamba hali hiyo inatokana na uchaguzi bali kiwango cha viazi vinavyowafikia kimepungua na sasa wanatengemea zaidi bidhaa hiyo kutoka mkoani Mbeya.
Alisema hivi sasa, kilo moja ya viazi mbatata ni Sh. 2,500 wakati bei ya kawaida ya viazi hivyo ilikuwa kilo moja ni kati ya Sh 800 na Sh.1,000.
Mfanyabiashara mwingine aitwaye Ame Salum, ambaye yeye huendesha shughuli zake katika Soko Kuu la Mwanakwerekwe, alisema kuwa shughuli za kibiashara sokoni hapo kabla na baada ya uchaguzi wa marudio zinaendelea katika hali ya utulivu na amani.
Hata hivyo, alikiri kuwa idadi ya wateja ilipungua zaidi sokoni hapo katika siku za kukaribia uchaguzi wa marudio na siku yenyewe ya uchaguzi tifauti na ilivyokuwa hapo kabla.
“Inawezekana idadi ya wateja ikawa imepungua siku ya uchaguzi wa marudio kwa sababu watu walikuwa na hofu… lakini baada ya kuona hali ipo shwari, wakawa wanafika sokoni hapa kupata huduma mbalimbali,” alisema.
Mkazi mmoja wa mjini Magharibi alisema ni kweli hakukuwa na tatizo lolote la kupata huduma katika maeneo ya sokoni wala madukani katika siku ya uchaguzi, lakini tatizo kubwa kwa baadhi yao lilikuwa ni hofu ya kuwapo kwa vurugu na kingine kinachowasumbua hadi sasa ni kuendelea kupaa kwa bei za bidhaa tangu siku chache kabla ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Aidha, eneo la Forodhani ambalo huwavutia zaidi wageni, limeendelea kuwa miongoni mwa yale yaliyokumbwa na athari za kupungua mno kwa wateja katika kipindi cha uchaguzi na hata hivi sasa baada ya kurejea madarakani kwa Dk. Shein.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa eneo hilo, la Forodhani, ambalo ni maarufu kwa kuvutia wageni na watalii mbalimbali wanaofika visiwani Zanzibar, hivi sasa limekuwa likipokea watu wachache tu wanaofika kwa ajili ya kupumzika, na hasa kuanzia Jumapili ya Machi 20 iliyokuwa ya siku ya uchaguzi wa marudio.
Mfanyabiashara mmojawapo wa eneo hilo, Juma Masoud, alisema idadi ya wateja wanaofika hapo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya hofu ambayo bado imejaa miongoni mwa watu kuhusiana na vuguvugu la uchaguzi uliofanyika bila kuridhiwa na CUF na pia kuwapo kwa kipindi hiki kisichokuwa cha msimu wa ujio wa watalii.
“Hali kama unavyoiona hapa (Forodhani). Watu siyo wengi kipindi hiki na biashara zimedorora sana. Kwa kawaida hapa huwa tunafanya biashara mpaka saa sita usiku, lakini hivi sasa ikifika saa nne usiku tunafunga kazi kwa sababu huwa hakuna wateja kabisa,”alisema Masoud.
Masoud aliongeza kuwa hivi sasa, licha ya kuendelea kuwapo kwa amani na utulivu baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa marudio, bado kuna watu wanahofia kutembea, hasa nyakati za usiku na hilo huchangia kudorora kwa biashara zao ambazo huanza saa 12:00 jioni.
CHANGAMOTO KWA DK. SHEIN
Baada ya Dk. Shein kutangazwa mshindi, kazi mojawapo kubwa iliyo mbele yake ni kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kukidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar.
Tangu mwaka 1995, CUF imekuwa ikichuana vikali na CCM huku vyama vingine vikiambulia jumla ya kura za idadi ya chini ya asilimia moja.
Katika kuleta maelewano visiwani Zanzibar, katiba ya mwaka 1984 ilifanyiwa mabadiliko na kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), lengo likiwa ni kuunganisha nguvu ili kuimarisha umoja miongoni mwa Wanzanzibar ambao kwa kiasi kikubwa wamegawanyika kiitikadi kupitia kambi za CCM na CUF.
Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Zanzibar, ili chama cha siasa kipate sifa ya kuwamo katika kuunda SUK, ni lazima kipate walau asilimia 10 ya kura zote halali zilizopigwa katika Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, katika uchaguzi wa marudio ambao CUF walisusia, hakuna chama hata kimoja miongoni mwa vile vilivyoungana na CCM kushiriki uchaguzi huo vilivyoambulia kura kwa idadi hiyo inayopendekezwa katika katiba na pia hakuna chama hata kimoja miongoni mwa vile vya upinzani vilivyopata kiti katika Baraza la Wawakilishi.
Tangu mwaka 1995, CUF imekuwa mpinzani mkubwa wa CCM na karibu kila uchaguzi, imekuwa ikitangazwa na ZEC kupata zaidi ya asilimia 40 ya kura zilizopigwa.
Mwaka 1995, mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, alitangazwa kushinda kwa kupata kura 165,271 sawa na asilimia 50.2 huku Maalim Seif wa CUF akiwa na kura 163,706 sawa na asilimia 49.8 ya kura 328,977 zilizopigwa.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Amani Abeid Karume wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura 239,832 sawa na asilimia 53.2, huku Maalim Seif akifuatia kwa kura 207,733 sawa na asilimia 46.1 huku kura halali zikiwa 450,968.
Mwaka 2010, Dk. Shein alitangazwa mshindi kwa kupata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1, Maalim Seif kura 176,338 sawa na asilimia 49.1 huku kura halali zikiwa 358,815.
Kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010, hali ya kisiasa ya Zanzibar ilikuwa tete, hasa kutokana na viongozi wa CUF na wanachama wake kuamini kwamba kwa miaka yote walikuwa wakishinda isipokuwa ZEC ilishirikiana na CCM kuiba kura.
Hali hiyo ilijitokeza dhairi Januari, 2001, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, kwa kuibuka vurugu na watu kadhaa kupoteza maisha huku wengine wakikimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya walikokaa kama wakimbizi.
Baada ya uhasama wa muda mrefu, mwaka 2010 ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), hali ya kisiasa ya visiwa hivyo ilitulia.
Miaka mitano baadaye sasa, CUF imesusia uchaguzi wa marudio ikitaka mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 2015 atangazwe, jambo linaloibua maswali mengi juu ya mustakabali wa visiwa hivyo.
Hata hivyo, katika hotuba yake baada ya kuapishwa juzi Alhamisi, Rais Shein aliwaomba viongozi wa dini kuhubiri amani na kwamba serikali yake itahakikisha inawaunganisha Wazanzibari wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment