Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, March 25, 2016

Ni wakati wa Zanzibar kusonga mbele, na CUF kujitafakari

Image result for dr shein

UCHAGUZI wa marudio Zanzibar umeshafanyika. Kwa kilichotokea, na kwa hakika kabisa, kulikuwa hakuna namna yoyote ya kufanya isipokuwa kurudi kwenye uchaguzi. Ni bahati mbaya sana chama kikuu cha upinzani Zanzibar, CUF kilisusia zoezi hilo la uchaguzi lenye tafsiri ya njia ya kidemokrasia katika kuitafuta ridhaa ya umma kwenye kuongoza.

Kwa CUF ulikuwa ni uamuzi wa kimakosa kususia uchaguzi. Ni uamuzi wenye gharama kubwa zaidi kisiasa. Siasa haipaswi kuwa uadui. Kilichobaki ni kwa CUF kuisogelea meza ya mazungumzo na wenzao CCM ili kuona ni namna gani wataweza kushiriki siasa za ndani ya Zanzibar na zaidi watakavyoshiriki chaguzi zijazo kwa namna ambavyo wanaamini zitakuwa huru na haki.

Na michakato ya namna hii ingelikuwa na maana na nguvu zaidi kama CUF kupitia wawakilishi wake nao wangeingia kwenye Baraza la Wawakilishi kupitia masanduku ya kura. 

Hivyo, wakati Wazanzibar wanahitaji kuyafukia yaliyopita kwenye kaburi la sahau na kusonga mbele kwa pamoja kuijega Zanzibar yao, ni wakati pia wa CUF kujitafakari upya na kujipanga kwa kushiriki siasa ikiwamo kujiandaa na chaguzi zijazo.
Maana, hakuna faida yeyote kwa CUF kujiweka kando na kuwaachia CCM peke yao waendeshe siasa za Zanzibar. Si jambo la tija pia kwa watu wa visiwani na bara.

CUF itambue pia nguvu na nafasi yake ya kihistoria katika kuijenga Zanzibar. Ikumbukwe, Chama cha CUF kiliundwa Mei 28, 1992. Ni chimbuko la kuunganishwa kwa Chama cha kutetea haki za Wananchi (Civic Movement) kwa upande wa bara na chama cha KAMAHURU cha Zanzibar.

CUF imetokana na vuguvugu la mageuzi nchini. Ingawa NCCR-mageuzi kilikuwa ni chama cha kwanza cha upinzani, CUF kilikuwa chama cha pili kusajiliwa katika mfumo wa vyama vingi baada ya CCM. Hii ilitokana na sura yake ya muungano kuonekana dhahiri. Hii ni moja ya nguvu kubwa za CUF. 

Hakuna anayejisumbua kuweka hadharani, ukweli kuwa, kwa sasa, CUF ni chama pekee cha upinzani, chenye uhakika wa kuwa na wawakilishi bungeni kutoka Unguja, Pemba na Bara.

Tofauti za kifikra na kimitazamo ni mambo ya kawaida katika siasa. Kunahitajika majadiliano endelevu katika kupata ufumbuzi wa migogoro. Si lazima papatikane mshindi katika kila mgogoro, wakati mwingine hutengenezwa mazingira ya pande zote mbili kushinda, kila mmoja kujisikia ameshinda. Wazungu wanaita; win- win situation.

Mazungumzo baina ya CUF na CCM yaendelee na hata ikibidi, kwa kushirikishwa mpatanishi kutoka nje. Katika mazingira ya sasa ya CUF na CCM kutoaminiana busara lingefanyika hilo. Dunia inatuangalia.

Ndio. CCM na CUF lazima wakutane, wazungumze, wapatinishwe, utafutwe muafaka wa nne, kwa maslahi ya taifa. Kamanda makini anaelewa , kuwa kwa hali ilivyo sasa kwenye uwanja wa mapambano, kujichimbia handakini ni mkakati wa makosa. Hakuna aliyeshinda kwenye vita ya jana, hakuna atakayeshinda kwenye vita ya leo wala kesho. Bila muafaka, sote tutashindwa.

Ni dhahiri, Wazanzibar wanyonge walio wengi hii leo ni walio wagonjwa kiuchumi na wenye kuhitaji tiba ya haraka ili warejeshe matumaini yao. Vijana walo wengi hawana ajira na hawana hakika yao ya leo na kesho.

Inafahamika, ajira kwa walio wengi visiwani inatokana na sekta ya utalii ambayo sasa iko kwenye umahututi kutokana na hofu ya kutokea machafuko ya kisiasa yenye kuwatisha wawekezaji na watalii wenye mazoea ya kutembelea visiwa hivyo.

Wanachotaka walio wengi Zanzibar ni uwepo wa amani na utulivu wa kisiasa ili maisha na shughuli zao zao za kiuchumi ziendelee. Zanzibar imekuwa na bahati pia ya kuwa na Katiba inayoruhusu uwepo wa Serikali ya Mseto. Kuna tatizo gani kutawala pamoja? Kimoja kikitoa Rais, kingine kinatoa Makamu wa Kwanza.

Kwa hali halisi ilivyo sasa, Wazanzibar hawa hawapaswi kuachwa kuogelea kwenye bahari ya sintofahamu. Naam, Uchaguzi wa Marudio umeshafanyika. Ni wakati sasa kwa wanasiasa kuachana na maslahi binafsi na kuangalia mustakabali wa walio wengi.

Kila la heri Wazanzibar.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/ni-wakati-wa-z%E2%80%99bar-kusonga-mbele-na-cuf-kujitafakari#sthash.8uYXn0uy.dpuf

Wasiliana na mwandishi
Maggid Mjengwa
mjengwamaggid@gmail.com
+255-754678252, +255-712956131
http://mjengwa.blogspot.com
Maggid Mjengwa pia ni Mwandishi wa Kitabu; "Maisha Ya Barack Obama, alikotoka, aliko na anakokwenda". Kinapatikana mitaani.

No comments :

Post a Comment