Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, March 11, 2016

Siku Mwalimu Nyerere alipokataa viatu New York

Pius Msekwa
Toleo la 446
KWA kuwa kitabu hiki kinaelezea shughuli za uongozi na utawala wa Mwalimu Nyerere, maelezo yake binafsi yanastahili kuwekwa mapema katika sura za mwanzo, ili wale ambao hawakupata bahati ya kumfahamu vizuri katika kipindi cha uhai na uongozi wake, wapate fursa ya kufanya hivyo kabla hatujafikia kueleza kazi zake, na sifa zake nyingi za uongozi, pamoja na tabia yake binafsi.

Lakini kabla ya kueleza sifa hizo za Mwalimu Nyerere, ni vizuri kwanza kumkumbusha msomaji wa kitabu hiki kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa ni binadamu kama walivyo binadamu wengine; kwa hiyo bila shaka yeye pia alikuwa na mapungufu fulani fulani ya kibinadamu, kama vile hasira, ambazo wakati mwingine zilimpelekea kufanya makosa katika maamuzi yake, kutokana na hasira iliyompata ghafla.
Ipo mifano kadhaa ya kuthibitisha hilo.

Mfano mmoja ni ile siku alipowavurumisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliofanya maandamano ya kupinga mpango wa Jeshi la kujenga Taifa, na baadhi yao kupayuka maneno ya hovyo kwamba ‘heri wakati wa ukoloni”, wakimaanisha kwamba hali ya nchi ilikuwa bora zaidi wakati wa utawala wa wakoloni.
Maneno hayo yalimkasirisha Rais Nyerere kiasi cha kuamuru chuo hicho kifungwe, na wanafunzi wote warudishwe makwao kwa muda alioutaja wa miaka miwili, ili watumie muda huo kutafakari kosa walilolifanya wakiwa pamoja na wazazi wao.

Mfano mwingine unaofanana na huo ni wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipofanya maandamano ya kupinga Koloni la Southern Rhodesia kujitangazia uhuru wake kinyemela mwezi Novemba 1965; na Serikali ya Uingereza isichukue hatua yoyote dhidi ya viongozi wa Koloni lake hilo.

Maandamano yao hayo yaliwafikisha kwenye jengo la Ubalozi wa Uingereza, ambapo waliharibu baadhi ya mali zilizokuwamo katika jengo hilo. Vijana hao walikamatwa na Polisi na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Kati. Baada ya hapo Mwalimu Nyerere akaagiza vijana hao wapelekwe Ikulu ili aweze kuzungumza nao.

Walipofika huko aliwapokea vizuri na kuwaeleza ubaya wa kosa lao la kufanya maandamano bila ruhusa ya Polisi, na pia kosa la kuharibu mali katika jengo la Ubalozi wa Uingereza. Hatimaye akawataka waombe radhi kwa Balozi wa Uingereza kwa makosa hayo.

Halafu akauliza kama kulikuwa na yeyote miongoni mwao ambaye alikuwa anapinga wazo ilo la kuomba radhi. Mwanafunzi mmoja akajitokeza na kusema kwamba yeye anapinga wazo hilo. Papo hapo Rais Nyerere akamwamuri Kamishna wa Polisi amchukue kijana huyo na kumpeleka akachapwe viboko sita.

Baada ya tukio hilo kuwa limepita, Rais Nyerere alimuita tena kijana huyo aende Ikulu, ambapo alimueleza kwamba alikuwa ametoa amri hiyo kwa hasira iliyompanda ghafla, na kwamba hasira hiyo ilikuwa imempeleka kwenye hulka za ualimu wake wa darasani ambapo adhabu zinazotolewa kwa wanafunzi huwa ni kuchapwa viboko.

Hapo Mwalimu Nyerere alidhihirisha uungwana wake wa kukiri kosa, bila kujali wadhifa mzito aliokuwa nao kama Rais wa nchi.

Aidha maswali ya kipuuzi kutoka kwa waandishi wa habari yalikuwa yakimpandisha hasira. Kuna wakati ambapo mwanasiasa uchwara mmoja, aliropoka kusema kwamba Mwalimu Nyerere eti hakuwa Mtanzania wa kuzaliwa hapa, bali ni mtu aliyetoka Burundi.

Upuuzi huo uliandikwa kwenye baadhi ya magazeti ya hapa nchini. Siku moja baadaye, Mwalimu Nyerere akiwa katika safari zake za kawaida, alipitia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyetta, Nairobi.

Mwandishi mmoja wa habari aliyekuwapo hapo akamuuliza Mwalimu Nyerere swali: ‘tumesikia tuhuma kwamba wewe siyo Mtanzania, bali ni Mrundi. Je tuhuma hizo zina ukweli ? Swali hilo la kipuuzi lilimuudhi sana Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo akamjibu kwa kejeli kwamba; “umesema kuwa umesikia tuhuma hizo. Je ukisikia tuhuma kwamba mimi ndiye baba yako niliyekuzaa na mama yako, utakuja kuniuliza kama tuhuma hizo ni za kweli?”
Waandishi wote waliokuwapo wakacheka kwa kutambua kwamba swali la mwenzao huyo lilikuwa la kijinga, alipouliza swali ambalo jibu lake liko wazi kabisa kwamba siyo kweli.

Ndipo Mwalimu Nyerere alipowapa somo waandishi hao wa habari kwa kuaambia kwamba “swali la kijinga linastahili majibu ya kijinga”
Sasa tuangalie sifa za Mwalimu Nyerere
Ukiondoa mapungufu ya aina hiyo ambayo ni ya kila binadamu, kwa jumla muonekano wa tabia ya mwalimu Nyerere kwa watu wengi mbalimbali ulikuwa ni wa kuheshimika sana, hususani katika maeneo yafuatayo :-
Alijua kutumia vizuri sana kipaji chake cha ualimu.
Sifa yake ya wazi kabisa ilikuwa ni kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa ni mwalimu wa kweli, kwa maana ya mtu anayefanya kazi ya kufundisha, yaani mkufunzi, au mhadhiri.

Mwalimu Nyerere ni mtu aliyetumia usomi wake vizuri sana, kulingana na ahadi ya mwanachama wa CCM inayosema kwamba “nitatumia elimu yangu kwa faida ya wote” .

Yeye kwa hakika alitumia elimu yake kwa faida ya wote, kupitia hotuba alizokuwa akizitoa, ambazo kila moja ilikuwa ni darasa kwa wasikilizaji wake; na pia kupitia Makala nyingi mbali mbali alizokuwa akiziandika, ambazo pia zilitosha kabisa kuwa ni makala za kufundishia.

Bahati njema hotuba zake karibu zote, na pia Makala zake nyingi, zimechapishwa kwenye vitabu vyake vyenye majina ya Uhuru na Umoja; Uhuru na Ujamaa; pamoja na vitabu vingine alivyoviandika yeye mwenyewe kama vile Our Leadership and the Destiny of Tanzania; na vingine vingi.

Aidha, alikuwa na kipaji kingine cha kubuni vidokezo vinavyoeleza jambo kubwa katika maneno machache. Mifano yake ni kama vile Uhuru ni Kazi; It can be done, Play your Part; We must run while others walk; Linalowezekana leo, lisingoje kesho; kupanga ni kuchagua; n.k.

Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuridhisha watu kwa nguvu ya hoja zake.

Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuridhisha watu kwa nguvu ya hoja zake (power of persuasion). Uwezo huo ndio uliomsaidia kupata mafanikio makubwa katika malengo yake ya kisiasa.

 Uwezo huo unajidhihirisha katika matukio yafuatayo:
Kwanza, ni pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa nguvu ya hoja zake, wanachama wa Asasi ya Kijamii ya kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika katika serikali ya Kioloni, iliyokuwa inaitwa “Tanganyika African Association” (TAA); kuvunja chama chao hicho na badala yake kuunda chama kipya cha siasa cha “Tananyika African National Union (TANU), mwezi Julai 1954, ili kiwe ni chombo cha kupigania uhuru wa Tanganyika.

Pili na pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa nguvu ya hoja zake, wanachama wa chama hicho cha TANU, wakakubali kuvunja chama chao hicho na kukiunganisha na Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar na kuunda chama kipya, Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kiwe ni chombo chenye uwezo mkubwa zaidi wa uongozi wa nchi yetu.

Tatu ni pale alipofanikiwa kuwaridhisha kwa nguvu ya hoja zake, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika Tabora mwaka 1958; na kufanikisha mkakati wa Wakoloni wa “Kura Tatu”, pamoja na ubaya wake uliokuwa wazi kabisa, ukakukubaliwa na Mkutano huo. Ulikuwa ni mkakati wa hila uliobuniwa na serikali ya kikoloni kwa lengo la kuchelewesha uhuru wa Tanganyika, endapo ungekataliwa na TANU. 

Mkakati wenyewe ulilikuwa hivi:
Katika uchaguzi wa kwanza kabisa nchini Tanganyika uliopangwa na serikali ya Kikoloni, serikali hiyo iliweka masharti magumu sana. Mojawapo likiwa ni kwamba kila mpiga kura atatakiwa kupiga kura tatu, moja kwa mgombea mzungu, nyingine kwa mgombea muasia, na nyingine ya mgombea muafrika. Awali sharti hilo lilikuwa limekataliwa na wajumbe wengi wa mkutano huo.

Mwalimu Nyerere aliarifiwa mapema kabla ya mkutano kuhusu msimamo huo wa wajumbe, kwa hiyo naye akaandaa hoja zake mapema. Kwanza aliomba mkutano uchague Mwenyekiti mwingine wa muda wa mkutano huo, ili yeye aweze kutoa hoja zake mkutanoni akiwa kama mjumbe wa kawaida, na kuepuka kishawishi cha kutumia mamlaka ya kiti kulazimisha wajumbe kukubali mawazo yake.

Kutokana na uwezo wake wa kuridhisha watu kwa nguvu ya hoja, pamoja na kwamba katika mkutano huo kazi hiyo ilikuwa ngumu sana, lakini bado aliweza kuwaridhisha wajumbe wakakubali kushiriki katika uchaguzi huo. Hatua hiyo ilikuwa ni muhimu sana katika kuharakisha kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika.

Hali kadhalika, ni uwezo wake huo wa kuridhisha watu kwa nguvu ya hoja zake, ndio uliofanikisha harakati zake za kuunganisha maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Tanganyika wakaunda umoja na mshikamano katika kudai uhuru wa Tanganyika. 

kwani alifanikiwa kufanya hivyo kwa hotuba zake tu zilizoweza kuwaridha wananchi kubaini ubaya na aibu ya kutawaliwa na wakoloni; kiasi cha kuwafanya wawe tayari kujitolea na kujituma katika harakati hizo. Ilibidi watu wajitolee kwa sababu TANU wakati huo haikuwa na vitendea kazi kama magari wala fedha za kufanyia kazi.

Maoni ya baadhi ya watu kuhusu tabia ya Mwalimu Nyerere.

Tabia njema ya Mwalimu Nyerere imeelezwa kwa namna tofauti tofauti na watu wengi waliomfahamu. Kwa mfano, katika kumkaribisha kuhutubia mkutano ulioandaliwa na African American Institute ya Marekani tarehe 10 Februari, 1960; mshereheshaji wa hafla hiyo alimtambulisha Mwalimu Nyerere kwa maneno yafuatayo: “Mr. Nyerere has won the confidence of all groups in Tanganyika by his wisdom, modesty and humour”.

Naye Mwandishi Peter Haussler, katika kitabu chake kiitwacho “ Leadership for Democratic Development in Tanzania, aliandika kuwa : ‘the leadership style of Nyerere is also refered to as ‘charismatic’ and ‘visionary’. Charismatic leadership is the ability to influence followers based on supernatural gifts and attractive powers. Followers enjoy being with the charismatic leader because they feel inspired, correct and important”.

Aidha, katika kijitabu kinachoitwa ‘Memories of Julius Nyerere” kilichochapishwa mwaka 2009 kama sehemu ya maadhimisho ya miaka kumi ya kifo chake, na kuchangiwa na waandishi kadhaa tofauti; mwandishi mmoja alimueleza kuwa “Nyerere was an iconic leader, a man of principle, intelligence, and integrity”. Mwingine alimueleza kuwa “he was considered a political prophet by many, and a man of intelligence, humour and honesty”.

Mimi mwenyewe vile vile nilipewa nafasi ya kuchangia makala katika kijitabu hicho, ambapo nilliandika kama ifuatavyo: “ Nyerere has been variously described as a humanist, politician, thinker, and statesman. Indeed, Nyerere was all of those things, and much more. He was an ardent believer in peace, and a unique mobilizer of people. He was a devout catholic, but a strong believer in the separation of religion from politics. He was a modest man in his personal life, and hated pomposity in his official life”.

Katika dondoo la kueleza sifa za Nyerere (citation) lililosomwa na Waziri Mkuu wa India, Bi Indira Gandhi, katika sherehe za kumkabidhi tuzo la ‘Jawaharlal Nehru Award for International Understanding’ tarehe 17 Januari 1976, Mwalimu Nyerere alitajwa kuwa “a man of vision, a man of action, and a man of compassion” .

Kabla ya hapo katika sherehe hiyo hiyo, Rais wa India katika hotuba yake alikuwa amemweleza Mwalimu Nyerere kwamba “He is one of the foremost champions of human rights. He is a man of the people, gifted with great commonsense”.

Kwa jumla, katika maisha yake yote, Mwalimu Nyerere alidhihirisha kwamba alikuwa nazo sifa zote hizo.; kwani alitekeleza ipasavyo misingi yote ya maadili mema siyo tu katika maisha yake binafsi; bali pia katika maisha yake ya uongozi, kwa kipindi chote cha uhai wake, kama inavyooneshwa katika maelezo yanayofuatia hapa chini.

Kuhusu maisha yake binafsi.

Mwalimu Nyerere alikuwa na sifa kuu zifuatazo:- Alikuwa ni mtu muadilifu sana, asiyekuwa na makuu; mtu mwenye staha, mtu aliyetosheka; na asiyekuwa na hata chembe ya majivuno.

Kwa mfano, alipoanza kushika wadhifa wa Rais, hakupenda hata kidogo kujihusisha na zile mbembwe ambazo kwa kawaida huambatana na wadhifa huo wa Rais wa nchi.

Baadhi ya mifano inayothibitisha tabia yake hiyo, ni hii ifuatayo: Baadhi ya watu waliomfahamu alipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari ya Tabora, wameeleza kwamba hata wakati huo akiwa bado ni mwanafunzi, tayari alikwisha kujenga tabia ya kuchukia marupurupu ya upendeleo unaotolewa kwa watu wenye nafasi za uiongozi.

Wanaeleza jinsi alivyokuwa akichukia marupurupu ya upendeleo (privileges) yaliyokuwa yakitolewa na wakuu wa shule hiyo kwa viongozi wa wanafunzi, yaani Prefects. Hatimaye msimamo wake huo ulidhihirika wakati yeye mwenyewe alipochaguliwa kuwa Prefect, ambapo alitumia kipaji chake cha ushawishi kupunguza madaraka na marupurupu ya cheo hicho cha ma-prefect wa Wanafunzi.

Mfano mwingine nilioushuhudia mimi mwenyewe, ni kwamba alipokwisha kuchaguliwa na kuapishwa kuwa Rais wa Tanganyika tarehe 9 Desemba 1962; shughuli yake ya kwanza ilikuwa ni kulifungua na kulihutubia Bunge la kwanza la Jamhuri ya Tanganyika kesho yake tarehe 10 Desemba, 1962. Mimi nikiwa Katibu wa Bunge ndiye nilikuwa mwandalizi wa ratiba ya shughuli hiyo kubwa.

Nilijaribu kuiga ratiba ambayo hutumika katika Bunge la House of Commons la Uingereza wakati Malkia wao anapokwenda kuhutubia Bunge hilo. Huwa anasindikizwa na ofisa mmoja wa kike ambaye cheo chake kina jina la ‘Lady-in-Waiting’. Kwa hiyo na mimi nikapanga kuweka ndani ya ukumbi wa Bunge sambamba na Kiti cha Rais mwenyewe, kiti cha mke wa Rais Mama Maria Nyerere akisindikizwa na ofisa wa kike kutoka Ikulu, na katika ratiba nikamuonesha ofisa huyo kwa cheo hicho cha ‘Lady-in-waiting’.

Kumbe Rais Nyerere hakupendezwa na taratibu huo wa Lady-in-waiting’ ambao aliuita ni wa kisultani. Mara baada ya tukio hilo alituagiza tuachane kabisa na “mbwembwe za kijinga”.

Wakati huo huo aliagiza pia kwamba asiitwe ‘Mtukufu Rais’ wakati wowote; iwe ni katika mazungumzo ya kawaida, ama katika hotuba, au hata katika maandishi yoyote. Akaelekeza kwamba maneno rasmi katika mawasiliano ya aina hiyo yawe ni ‘Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika’ na si vinginevyo.

Aidha, aliwaelekeza Polisi waache tabia ya kufunga kila barabara anayopita Rais kwa muda usiojulikana hadi hapo Rais atapokuwa amepita. ‘Hii inanifanya niwe kero kubwa kwa watu wa Dar es Salaam’ alisema Mwalimu Nyerere katika maagizo yake hayo.
(ii) Alikuwa ni mtu asiyependa kujilimbikizia mali.

Hii ni tabia yake nyingine ambayo inamtofautisha na viongozi wengine wengi Duniani wa ngazi hiyo kubwa katika Taifa.

Kwa mfano, Mwalimu Nyerere hakuwahi kununua gari lake mwenyewe binafsi; na kwa ajili hiyo, hakuwahi hata kujifunza kuendesha gari. Alipokuwa akifundisha katika shule ya Sekondari ya Pugu na mimi nikiwa mwanafunzi katika shule hiyo, sisi wanafunzi tulimuona siku moja akipanda nyuma ya gari la shule aina ya Pick-up single cabin, alipopata lifti ya kwenda mjini Dar es Salaam, bila shaka kwenye shughuli zaka za kisiasa alizokuwa amezianza wakati huo.

Katika kiti cha mbele kwenye cabin walikuwa wamekaa walimu wenzake mapadre wawili wa Holy Ghost Fathers. Yeye alituambia baadaye kwamba mapadre hao walikuwa wamemwambia akae nao katika kiti cha mbele. Lakini yeye alikataa, kwa sababu hakuona haja ya kubanana kwenye kiti hicho wakati nyuma ya gari palikuwa na nafasi kubwa ya kukaa.

Kwa hiyo akaamua kukaa nyuma ya gari akipigwa na upepo na vumbi la barabarani. Kwa hakika, hakuwa na makuu.

Mfano mwingine ni kwamba mwezi Januari mwaka 1976, Mwalimu Nyerere alitunukiwa tuzo maarufu la “Jawahrlal Nehru Award for International Understanding” Tuzo hilo linaambatana na zawadi ya kiasi kikubwa cha dola za Kimarekani. Yeye baada ya kuzipokea fedha hizo, alizikabidhi zote kwa Chuo cha TANU cha Kivukoni ili zitumike kununulia vitabu vya Maktaba ya Chuo hicho. Hakuwa na tabia ya kujilimbikizia mali.

Halafu tena, Mwalimu Nyerere mwenyewe aliwahi kutusimulia hadithi moja kwamba katika harakati zake za kwenda kudai Uhuru kwenye Umoja wa Mataifa huko New York Marekani, safari moja alikutana na rafiki yake ambaye alikuwa anaishi huko. Rafiki yake huyo akamwambia kuwa angependa kumpa zawadi ya viatu, lakini kwa kuwa alikuwa hajui saizi yake ya viatu, akamshauri waende wote dukani ili akamnunulie viatu vyenye saizi inayomfaa.

Mwalimu Nyerere akakubali zawadi hiyo, wakaenda duka la viatu ambako Mwalimu alichagua jozi moja ya viatu vya rangi nyeusi. Rafiki yake huyo akamshawishi achague jozi ya pili, lakini Mwalimu Nyerere akakataa. 

Rafiki yake alimuuliza kwa nini hataki jozi ya pili, Mwalimu akamjibu kuwa ni kwa sababu ana jozi moja tu ya miguu (I have only one pair of feet !) Kwa hakika hakutaka kujilimbikizia mali, hata kama mali hiyo ni viatu tu.

Makala hii imechukuliwa kutoka katika kitabu cha Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/siku-mwalimu-nyerere-alipokataa-viatu-new-york#sthash.CTXwSEfD.dpuf

No comments :

Post a Comment