Wiki hii dunia inapoadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani, mabinti wanaendelea kufungwa na minyororo ya mimba za udogoni, ndoa za utotoni na kuzamishwa kwenye lindi la kina kirefu cha ujinga na umaskini.
Ni mambo yanayotokea kwenye jamii za wafugaji na wakulima za mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Mwanza na Tabora.
Mwishoni mwa mwaka jana, Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watu (UNFPA), vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kama ndoa za utotoni, ukeketaji na utelekezaji familia katika mikoa 12.
Yaliyojiri kwenye utafiti mkoani Tabora ambako utafiti ulifanyika katika wilaya za Urambo, Tabora Manispaa na Kaliua, ilibainika kuwa wilayani Kaliua baadhi ya familia huishi misituni bila uhusiano na mifumo rasmi ya taratibu za kiserikali.Huko hakuna shule wala uongozi badala yake maamuzi yanayofanywa na familia hivyo wasichana hawa wanaozwa, wanabakwa wengine wanatelekezwa, wanatumikishwa kwenye uzalishaji lakini kwa vile hawana huduma za afya wajawazito hawa wachanga wanakosa huduma hata ya mkunga wa jadi.
Jamii haina uhusiano na mifumo ya kiserikali, hivyo inakuwa vigumu vyombo vya serikali kushindwa kupenya na kufanyakazi, kadhalika taarifa zao hazifahamiki kwa vile wako nje ya utaratibu rasmi.
Pamoja na wasichana kukabiliwa na changamoto hizo wavulana wamenaswa kwenye kilimo, kuchoma mkaa na kuchunga mifugo ndani ya misitu minene wilayani Kaliua.
Akijibu swali kuhusu idadi kubwa ya watoto wa wafugaji wanaotakiwa kuwa shuleni lakini hawasomi badala yake huishi misituni, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya ya Kaliua, Mabula Isambula, anasema familia nyingi zipo ndani ya misitu hiyo.
Anaeleza kuwa zimepenya kwenye misitu mikubwa ya hifadhi na kuishi mbali na vijiji hivyo kuzuia watoto kusoma, wengine kulazimishwa kuozwa mapema au kupewa mimba utotoni bila watuhumiwa kuadhibiwa.
Isambula anasema wafugaji hao hutoka Mwanza, Simiyu na Shinyanga, wanaishi kwenye misitu ya ‘Mpandaline’ yenye mapori na hifadhi ya wanyama pori ya Ugala na misitu ya hifadhi ya Uyumbu.
Mwanahamisi Ali, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilayani Kaliua, anasema katika jamii za kifugaji mabinti wengi wana mimba huna haja ya kuuliza.Wanaonekana mitaani wakiwa wajawazito au wamebeba watoto badala ya kuwa madarasani.” Anafafanua kuwa mimba za utotoni huko msituni ni nying lakini nyingi haziripotiwa kwa vile jamii zinaishi nje ya mfumo rasmi, hata hivyo hakuwa na takwimu.
Anasema katika jamii za kifugaji mfumo dume unawaamisha watu kuwa kuolewa ni kama ‘fasheni’, kuzalishwa na kutelekezwa ni maisha ya wanavijiji wengi, hivyo kubakia kuwa changamoto ya ustawi wa jamii.
Si rahisi kuwaona wasichana hao licha ya kwamba juhudi za operesheni tokomeza ujangili ziliweza kuwafikia wavamizi hao wanaoishi msituni.
CHANZO
Mkurugenzi Isambula pamoja na Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwanahamisi Ali, wanasema tatizo hilo linakuzwa na wafugaji kujitenga hivyo kuwa vigumu kuwafikia na kupata taarifa sahihi zinazowahusu.
Mila zinazowalazimisha wafugaji kuwa na makundi makubwa ya wanyama na kutafuta malisho.
Kadhalika Wasukuma wengi wanaamini kuwa na familia kubwa ya watoto wengi na wake wengi pamoja na ufugaji mkubwa ndiko kufanikiwa kiuchumi.
''Kwa ujumla ufugaji mkubwa na kilimo maporini kunaharibu mazingira na misitu ni changamoto kubwa za Kaliua zinazohitaji ufuatiliaji na usimamizi zaidi. Lakini pia mfumo huo ni hatari kwa afya na ustawi wa watoto''.
Hata hivyo halmashauri zinahitaji kujengewa uwezo ili kuwaondoa wafugaji wanaoishi ndani ya misitu. Wanahitaji ndege, magari, vyombo vya dola na maeneo ya kuwahifadhi.
“Hata tukisema tuwakamate ni vigumu. Hakuna mahabusi wala nyumba za kuwahifadhi. Hatuwezi kuwavamia porini hatuna helkopta labda Wizara ya Maliasili na Utalii wanaofuatilia ulinzi wa mapori tengefu, hifadhi za wanyama na misitu,” anasema, Mwanahamisi
Hata hivyo ufuatiliaji unafanyika kwa kushirikiana na Idara ya Maliasili kwa mujibu Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo.
ATHARI
Mwanahamisi Ali, anaeleza kuwa zipo athari nyingi kama kuwa na kundi kubwa la wasio na elimu ambao itakuwa vigumu kujiendeleza hapo mbeleni.
Lakini kwa mabinti kuna uwezekano wa kuongeza vifo vya wazazi na watoto wanaojifungua katika umri mdogo, watoto kukosa chanjo, wasichana kuambukizwa maradhi yatokanayo na kujamiaana kama Ukimwi. Kutelekezwa na kuishi maisha magumu na familia zao.
AJIRA UTOTONI
Utafiti umebainika kuwa watoto wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 ambao wengine hawakumaliza darasa la saba ni waathirika wa kilimo cha tumbaku. Wanadaiwa kusafirishwa kutoka mbali kufanyakazi kwenye mashamba hayo kwa mikataba.
Watoto hawa wa kiume hulimishwa, kunyunyiza dawa na kukausha tumbaku kwenye mashamba yaliyoko Wilaya za Urambo na Kaliua mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa maelezo ya maofisa maendeleo ya jamii, Paul Kahumbi wa Halimashauri ya Urambo na Alfred Msengi wa Kaliua, wanatoka Kagera, Shinyanga na Kigoma.
Wakizungumzia unyanyasaji huo wa ajira za mikataba, kwa nyakati tofauti wanatoa maelezo yanayofanana kuwa watoto wa kiume ndiyo waathirika wakubwa.
VISABABISHI
Umaskini wa familia, kuishi katika mazingira magumu, kuwa na wazazi wagonjwa hasa maradhi yanayodumaza afya mfano Ukimwi na misukumo ya wenza wa rika ni chanzo cha utumikishwaji huo.
Watoto hupewa mkataba wa kulima, kupanda, kunyunyuzia dawa na kukausha tumbaku, anasema Elizabeth Kahurwe, aliyeshiriki kuwafuatilia watoto hao mashambani.
Anasema wanapata ujira mdogo wa kati ya Shilingi 200,000-400,000 kwa vile hawafahamu kuzungumza mikataba.
“Kama huelewi mambo ya mshahara unaweza kuingia mkataba wa Shilingi 200,000 kwa msimu mzima wenye miezi 10, japo wengine hulipwa Shilingi 400,000” anasema.
Anaeleza kuwa watoto hao hupata mshahara ‘kiduchu’; licha ya kutumikishwa mwaka mzima kuanzia Septemba hadi Juni mwaka unaofuata.
“Wanalima, kuweka kemikali za kuua wadudu, kuweka mimea mbolea na viuatilifu, kuvuna na kukausha tumbaku,” anaongeza
Kwa Kiha wafanyakazi hao huitwa ‘wakeraji’ au ‘wakozi’ jina linalotumiwa maeneo mengi ya Tabora.
Kahurwe, anaongeza zaidi kuwa, pia wanatumikishwa kukata magogo na kuni na kukausha tumbaku ndani ya matanuru yaitwayo ‘mabani’.
“Watoto hukaa kwenye ‘mabani’ wakiumizwa na moshi wanapochochea moto kwa viwango vinavyotakiwa.” Anasema ofisa huyo.
ATHARI
Kahumbi na Kahurwe wanasema kukosa elimu, kuendelea kuwa maskini na wasiokuwa na taaluma na kuendelea kunyonywa na wakulima. Hii inatokea kwa sababu ‘wakeraji’ wanapotolewa vijijini wakapewa mikataba hupewa vibanda vya kuishi.
Mwajiri huwapa unga, maharage, mboga na pia huwaruhusu kuchukua mishahara yao kununua mavazi, redio , tochi na simu.
“Ukifika mwisho wa msimu anawakata fedha zote akiwadai gharama za pango, chakula na mikopo waliyochukua kununua mahitaji mengine kwani walipotoka vijijini hawakuwa na nayo,” anasema Kahumbi na kuuita unyonyaji.
Anafahamisha kuwa tatizo la kuhadaa watoto lipo na wakati mwingine hata wasichana wanatumika kushona magunia kwa ajili ya kufungasha tumbaku.
Licha ya kuwa na umri mdogo watoto hawa wanaathirika na kemikali za sumu, kadhalika kisaikolojia wanaishi na kujitegemea katika umri mdogo, wanafanya kazi ngumu kwa malipo duni.
USHUHUDA
Akizungumza kwa simu kutoka Buzebazeba Kigoma, kijana aliyewahi kutumikishwa kwenye ajira hiyo, anasema alifikishwa Urambo akiwa na miaka 16.
Anasema aliingizwa kwenye ajira hiyo na wakala aliyefika Buzebazeba kijijini kutafuta wafanyakazi wa mashamba ya tumbaku akiwaahidi mishahara minono na hali bora.
Anakumbusha kuwa baada ya mfanyabiashara huyu kupata wafanyakazi aliowahitaji, vijana wengine walivutiwa na kujitokeza kwenda Urambo na Kaliua , naye alishiriki kuwatafuta marafiki hao alioongozana nao.
Anasema kiasi vijana walivyoitikia wito mfanyabiashara huyu aliwasiliana na wakulima wengine akiwauliza endapo wanahitaji wafanyakazi kutoka Kigoma.
“Wanapokubali ‘bosi’ wao aliwakusanya na kuwafikisha Urambo kwa kuwalipia nauli na chakula na kuwakabidhi kwa wenyeji wao” anaongeza.
Lakini mtoto huyu alifanyakazi kwa miezi mitano na kurudishwa nyumbani baada ya kuugua jipu kubwa mguuni.
Analaumu kilimo hicho kuwa ni cha kinyonyaji na hakimjali mtu kwani alivyokuwa mgonjwa alikosa huduma na kutimuliwa.
Anaeleza kuwa watoto wengi wanaoshiriki kilimo hicho ni ni jamii za makabila madogo lakini pia wapo wengine kutoka Mwanza na Shinyanga wanaosifiwa kwa kuchapa kazi.
UDHIBITI
Kwa ujumla maofisa maendeleo ya jamii wa Urambo na Kaliua wanasema wadau na asasi za kiraia likiwamo shirika la JIDA lililokamilisha mradi huo,limeendesha operesheni ya kuwaondoa watoto shambani.
Wanatahadharisha kuwa inakuwa ngumu kwa vile watoto kutoka mikoa ya jirani na wa ndani ya familia wanatumikishwa kwenye kilimo cha tumbaku.
Ndani ya familia watoto hawana mikataba lakini wanashirikiana na wazazi kuzalisha zao hilo linalouzwa kwa ‘Dola’ za Marekani. Wakati mwingine msimu ukianza wanaacha shule.
Viongozi wa wilaya hiyo wanasifu juhudi za wadau zilizowaondoa watoto mitaani hapo, japo hakuna takwimu za kuonyesha mafanikio kwa vile asasi zilizofanya kazi hiyo zimemaliza miradi hiyo.
Mafanikio ni kuwarudisha shuleni kwenye mikoa na vijiji walikotoka.
Maofisa maendeleo wanasema wananchi wamehamasishwa kuhusu kuacha ajira za kuwatumikisha watoto lakini umaskini ndani ya familia, wanaume kutelekeza familia,magonjwa ni vikwazo.
UFUMBUZI
Viongozi hawa, walimu na wazazi wanashauri halmashauri zitunge sheria ndogo kukataza wafanyabiashara kununua tumbaku inayozalishwa na watoto pia waweke pingamizi magulioni.
Wanawashauri wanavijiji wafuatilie mashambani kuwabaini na kuwakamata wakulima wanaotumikisha watoto.
Maofisa maendeleo hawa wanataka serikali ipeleke maofisa maendeleo ya jamii kwenye kata na vijijini ili kufundisha na kutetea haki za watoto, mabinti na makundi ya wanyonge.
SOURCE: NIPASHE
No comments :
Post a Comment