By Brandy Nelson, wananchi
Mbeya. Wajawazito wa Kata ya Igale wilayani Mbeya, wamelalamikia kufukuzwa na kunyimwa huduma kutoka kwa baadhi ya wahudumu wa afya wa zahanati za vijiji kwa madai wananuka kwa sababu ya kutooga.
Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wa kata hiyo, Lyidia Sankemwa alisema hayo alipowasilisha taarifa ya kero za wananchi alizopokea kwenye kituo chake.
Sankemwa alisema wajawazito wa vijiji vya Itaga, Igale, Horongo, Izumbwe na Shongo, walifika kwenye kituo chake na kulalamika kuhusu kufukuzwa na wahudumu wa afya.
“Tumepokea malalamiko mengi kutoka kwa wajawazito kuwa baadhi ya watoa huduma za afya katika zahanati zetu wanawafukuza kwa madai kuwa wananuka na hatimaye kucheweleshewa kupata huduma,” alidai Sankemwa.
Katibu wa Kituo hicho, Alfred Mwambugu alisema kutokana na tatizo hilo, baadhi ya wajawazito wanakataa kwenda kupata huduma katika zahanati hizo kwa kuhofia kutolewa lugha chafu.
Akizungumzia malalamiko hayo, Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Hamza Mwangomale alisema ameyapokea na kushawasiliana na mratibu wa afya kwa ajili ya kuandaa kikao cha pamoja na watoa huduma za afya wa zahanati zinazotuhumiwa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igale, Alinanuswe Mwakamala alisema kata hiyo yenye vijiji vitano ina zahanati nne ambazo hazikidhi mahitaji.
Alisema kata hiyo ina wakazi 11,800 wanaohudumiwa na zahanati nne na Kijiji cha Horongo hakina zahanati, wakazi wake hulazimika kufuata huduma kwenye zahanati za vijiji vingine kwa umbali wa kilomita tano.
No comments :
Post a Comment