
Wakati mila, desturi na mfumo dume katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara ikiminya haki ya mwanamke kumiliki ardhi, kwa Tanzania Zanzibar ni tofauti.
Visiwani hapa, masharti ya kumiliki wa ardhi haumkwazi mwanamke kumiliki ardhi.
Hata hivyo, pamoja na uhuru huo, idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi ni ndogo ikilinganishwa na wanaume.
Ikumbukwe kuwa, wanawake ni wengi Zanzibar ikilinganishwa na wanaume na takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 51 ya watu visiwani hapa ni wanawake, lakini asilimi 20 pekee ndio wanaomili ardhi na asilimia 31 hawamiliki ardhi.
Mwanasheria kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Hassan Nassor, anasema tatizo ni uelewa mdogo wa sheria za ardhi ambazo husababisha umiliki na utumiaji wa ardhi usio rasmi kiasi cha wanawake kunyang’nywa au kuporwa ardhi na wengine.Anasema uwezo mdogo wa wanawake wa kifedha wa kumiliki ardhi, huwafanya wawategemee ndugu zao wa kiume, watoto au waume zao.
Anaeleza sababu nyingine ni mwamko mdogo wa wanawake wa kumiliki ardhi, uelewa mdogo juu ya taratibu za kuwasilisha madai ya malamiko ya ardhi akitolea mfano wa kutojua kuwa ipo mahakama maalum inayoshughulikia migogoro ya ardhi.
Anasema Zanzibar asilimia 70 ya wanawake wanatoa mchango mkubwa katika nguvu kazi ya kilimo hasa vijijini na kwamba wanachangia katika pato la taifa.
“Umiliki wa ardhi bado ni tatizo kwa wanawake wengi wa Zanzibar, hiyo inatokana na ukweli kwamba ni asilimia 20 tu ya wanawake ndio wanaomiliki ardhi ukilinganisha na asilimia 51 ya wanawake wote wa Zanzibar,” anasema mwanasheria huyo.
Alisema Sheria za kimataifa zinaeleza kuwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume wanahaki sawa za kumiliki mali, akifafanua kuwa haki hizo ni kwa mali zinazohamishika na zisizohamishika.
Anafafanua kuwa kuna njia kadhaa za mtu kumiliki ardhi ikiwa ni kwa kupewa na serikali, urithi, ununuzi au kugaiwa.
Anasema Sheria ya mirathi haimzuwii mwanamke kurithi ardhi, lakini wanawake wengi wananyimwa haki yao hiyo ya kutopewa mirathi na kumiliki ardhi.
“Baadhi ya wanawake wanapofiwa na waume zao au wazazi wao kama wameacha mali huwa wanakoseshwa kwa makusudi haki yake hiyo ya kurithi,” alisema.
Anasema kamisheni ya ardhi imeazisha utaratibu wa uhaulishaji wa ardhi ambao kwa kiasi kikubwa huwasaidia wanawake kuimiliki.
Mkurugenzi wa Idara ya wanawake na Watoto, Rahma Ali Khamis, anasema usawa wa kumiliki mali upo kwa pande kwa mwanaume na mwanamke, lakini kumekuwapo na tabia ya kupuuza jambo hilo ambalo linachangia kuwapo kwa udhalilishaji wa kijinsia.
Akizungumzia ujumbe wa mwaka huu Zanzibar katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani, unahitaji kuendana na vitendo kwa sababu ili ufanikiwe ni lazima kuwapo kwa ushirikiano wa mwanaume na mwanamke.
Aliutaja ujumbe huo kuwa ni ‘Wanawake ni wenza katika kukuza uchumi, toa fursa sawa wamiliki rasilimali’.
Anasema masuala ya wanawake yamekuwa si mageni, lakini kila siku wamekuwa wakiyaeleza ili yaweze kueleweka zaidi na kujua umuhimu wake.
“Huu ni wakati wa kuacha kulaumiana si kwa mwanaume au mwanamke sote ni sawa na tunahaki moja ya kukuza uchumi kwa kujenga taifa imara,” alisema Rahma.
Hivyo aliwataka wanawake kuandaa mazingira bora ambayo yatawasaidia kuyafanya yale ambayo yanafaida kwao ikiwamo kumiliki ardhi.
Anaongeza kuwa fursa za uwezeshaji wanawake zipo nyingi katika masuala mbalimbali kama ardhi, taasisi za mikopo, elimu na taasisi za kusaidia wajasirimali ambazo wakizutumia vizuri maendeleo yataonekana.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tamwa) Zanzibar, Mzuri Issa, anasema Serikali ni lazima itoe ufafanuzi juu ya umiliki wa ardhi ili kuepusha matatizo yaliyopo katika umiliki wa rasilimali hiyo kwa wanawake.
Anasema pamoja na kuwa sheria zinasema kila mwananchi anahaki ya kumiliki ardhi, lakini bado inaonekana kuwapo kwa urasimu mkubwa wa kufanikisha hilo.
Anasema yeye mwenyewe alishawahi kuandika barua ya kuomba hati ya kiwanja, lakini hadi sasa ikiwa ni muda mrefu umepita hajafanikiwa kuipata na kusema urasimu huo unawakwamisha zaidi wanachi wa chini.
Anashauri kuwa ni lazima Serikali itoe ufafanuzi juu ya kumiliki ardhi na mali pia itoe kipaumbele kwa wanawake katika kuhakikisha wanafikia hatua ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa wanaume.
Anafafanua kuwa baada ya kuona wanawake wengi wanadhulumiwa ardhi wameamua kutoa elimu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake.
Anasema elimu hiyo zaidi huitoa vijijini ambako wanaamini ndiko kwenye matatizo zaidi ya wanawake kushindwa kumiliki ardhi.
Mkurugenzi wa Chama Cha wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mtumwa, anasema katika kumkomboa mwanamke ni lazima taasisi za kutetea haki za wanawake ziwe kitu kimoja ili kufanikisha mwanamke kuamka kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Anasema kumekuwa na malalamiko mengi katika suala la mwanamke kumiliki rasilimali na kwamba mashirika yote yanayotetea haki za wanawake wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wanawake ikiwamo kudhulumiwa mali.
Aidha, anasema katika taasisi yao wamepokea malalamiko 204 kwa mwaka jana yanayohusu mirathi na kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo, anasema kuna tatizo la upatikanaji wa haki za wanawake katika kumiliki ardhi kwenye vyombo vya sheria na katika jamii.
“Kiukweli bado mwitiko ni mdogo mahakama bado kutoa haki ni tishio, kwa sababu kuna kesi nyingi zimelalamikiwa na baadhi ya kesi ushahidi wake upo, lakini mwanendo wa mahakama katika utoaji wa hukumu bado unavunja moyo sana,” alisema Jamila.
SOURCE: NIPASHE
No comments :
Post a Comment